Adeladius Makwega-MAKOLE


Mwaka 2001 nikiwa mwanachuo wa chuo cha Ualimu Kasulu kozi ya Stashahada ya Ualimu, mimi na wanachuo wezangu tulifundishwa somo linalofahamika kama Misingi ya Upimaji. Somo hili lilikuwa na malengo ya kumuandaa mkurufunzi wa ualimu kufahamu namna ya umuhimu wa matokeo ya mwanafunzi wake baada ya kusahihisha mitihani na tafsri ya matokeo hayo.

Somo hili lilikwenda mbali kabisa na lilielekeza kanuni ya namna ya kuyaweka vizuri matokeo hayo kabla ya kuwa hadharani. Kanuni ilieleza kuwa matokeo ya wanafunzi yanapaswa kuwa na taswira hii; wachache sana watafaulu sana kwa ngazi ya juu, wengi wao watafaulu kwa ngazi ya wastani na huku wachache sana watafeli. Somo hili tulifundishwa na mkufunzi aliyefahamika kama kama Mwalimu Rashid Ndashikiwe alisema bayana kuwa,”Haiwezekai matokeo ya wanafunzi yakawa darasa nzima limefaulu kwa alama za juu, pia haiwezekani darasa nzima wakawa wamefaulu kwa alama za kati na mwisho haiwezekani darasani nzima wakafeli.”

Mkufunzi huyu alibainisha kuwa ukiona jambo moja kati mambo haya matatu limetokea katika matokeo yako, hakikisha matokeo hayo kabla hayajabandikwa katika mbao za matangazo au kuwekwa hadharani kuonesha upimaji wa wanafunzi hao lazima matokeo hayo alama ya kila mwanafunzi ipitie katika kanuni ya kurekebisha matokeo. 

(Leo siijadili kanuni hii kwa kina hii ni mada ya siku nyengine). Kama matokeo hayo yakibakia katika taswira hizo moja kati ya tatu inatoa picha mbaya kuwa mwalimu, mkufunzi na taasisi iliyosimamia haya matokeo maana yake ina shida na kwa taratibu za ualimu lazima mwalimu, mkufunzi, viongozi wanaosimamia taasisi hiyo wachukuliwe hatua haraka kwa kuwa hawakutimiza wajibu wao kama wataalamu wa masuala ya elimu na shida hiyo isijirudie tena.

Dhana ya wengi ni kuwa matokeo yakiwa mabaya ni kwamba wanafunzi hawakutimiza wajibu wao, dhana hiyo ina ukweli kiasi, msimamizi wa taaluma anawajibu wa kufanya maboresho ya alama hizo kabla hajayawekwa hadharani. Kama somo husika lilikuwa halieleweki basi mhadhiri alipaswa kuondolewa haraka na wale waliokuwa wakimsimamia wakati wa tathimini za mhadhiri huyo za kila wiki na kila mwezi . Kwa hiyo kuyaruhusu hadharani matokeo ya aina hiyo lazima uwajibikaji wa kila muhusika ufanyike haraka.

Nilipokuwa nasoma shahada ya Sanaa ya Habari nilikuwa mjumbe wa Seneti ya chuo Kikuu cha Iringa nikiingia kwa niaba ya serikali ya wanachuo katika kikao kimoja chini ya Uenyekiti wa Profesa Nicouls Bangu na katibu wake Profesa Andongisye Katule kuna siku iliibuka hoja ya matokeo mabaya ya kozi mojawapo ya wanafunzi wa shahada ya kwanza ya sheria. Mjadala ulikuwa mkubwa sana maelezo ya mhadhiri wa kozi hiyo aliyekuwa raia wa Kenya yalikuwa kwamba wanafunzi wake hawakufanya vizuri.

Nakumbuka mwakilishi wa wanachuo waliokuwa wakisoma sheria katika kikao hicho alikuwa Philip Philikunjombe Haule(Sasa ni Daktari wa Falsafa) alipingana na hoja hiyo kwa kina na kwa ushahidi kuwa wanachuo walikuwa na uwezo mkubwa kitaaluma alitumia sampuli ya mwanachuo mmoja wa darasa hilo aliyefanya vizuri mno kwa kozi zote lakini kozi hiyo alifeli, huku mitihani ya majaribio akifanya vizuri sana na kidato cha nne na cha sita akifanya vizuri sana . Kwanini afeli kozi hiyo?

“Mhadhiri ameajiriwa atoe elimu yake, kwanini wanachuo wote wafeli? Shida inawezekana ni mhadhiri mwenyewe, matokeo ya haki lazima wachache wafaulu sana, wengi wafaulu kwa wastani na wachache wafeli lakini kwa taswira ya matokeo haya wengi wamefeli hapa pana shida,kikao hiki kikiyabariki matokeo haya na sisi kulinyama hilo itakuwa ni kosa kubwa .” Mwanakwetu alisema, maamuzi yalifanyika dhidi ya mhadhiri na dhidi ya matokeo hayo. Maprofesa hawa wawili walikubaliana na hoja za wajumbe hao wawili na walifanya uamuzi wa kisomi katika hili.

Mwanakwetu kwa nini leo ninaeleza haya? Hivi karibuni Shule ya Sheria Tanzania –The Law School of Tanzania imetangaza matokeo yake ya wanachuo wake na kubainika kuwa wanachuo 265 wamefeli moja kwa moja huku wanachuo 342 wamefeli baadhi ya masomo wanatakiwa kurudia na wanachuo 26 tu ndiyo waliofaulu kati ya wanachuo 633.

 Hilo likiwa jambo la kushangaza mno.“Shule yetu ya sheria waadhiri wake wanafundisha vizuri sana lakini maswali mengi yanatungwa kwa mitego mikubwa na vitu vinavyofundishwa darasani siyo vile vinavyotunga katika mitihani hiyo, unajibu jibu hili wakati mwezako alitaka ujibu jibu hili na katika sheria jibu ni moja tu, kwa kweli wanachuo wengi wanalalamika, wengine wanasema mbona walijibu mtihani vizuri lakini matokeo mbona yamekuwa hivyo?”

Pale kwa kweli kuna kitu, kwanini waliofaulu wawe 26? Lakini pia Mkuu wa Chuo hiki hazungumzi na wanachuo, huonekana mara moja tu wakati wa kuanza masomo, hilo nalo ni shida kubwa sana. Kama mkuu wa chuo angekuwa jirani na wanachuo hilo lingekuwa jepesi na haya matatizo yasingekuwapo, niliambiwa. Ada ni shilingi 1,570,000/-na masomo yote kwa miezi 6 ya darasani na miezi sita ya vitendo. Hakuna mabweni, chakula tunajitegemea wenyewe ambapo kwa mwezi mmoja kupanga na chakula ni karibu shilingi 400,000/-na bado nauli inategenea na chuo hiki na kibaya zaidi kila somo linalorudiwa mara ya pili mwanachuo anapaswa kulipa shilingi 30,000/-“

Mwanakwetu nilijuliza swali hivi hayo yanayofundishwa kwa miezi sita katika shule yetu ya sheria ni yepi? Nilipofuatilia hilo nilibaini kuwa yote ni marudio yaliyofundishwa huko Chuo Kikuu kwa miaka mitatu au minne. Kweli mwanafunzi afaulu masomo aliyojifunza miaka minne na kufeli marudio? Nia ya shule hii ilikuwa ni kuwawekewa kizingiti wasomi wapya wa sheria na wasomi wa zamani kutawala soko la sheria nchini? “Tunasoma miezi sita, tunafanya maigizo ya mahakama na miezi sita ya mwisho tunakwenda kwenye mazoezi.”

Mwanakwetu kama mzazi hali hii ya shule ya sheria inasikitisha sana. Nikiwa Chuo Kikuu cha Iringa miongoni mwa wahadhiri wa sheria walikuwapo walikuwa ni Jaji Raymond Mwaikasu na Jaji Agustino Ramadhan ndugu hawa wote ni marehemu leo hii, wakati huo hawakuwa wakilalamikiwa katika utoaji wa alama japokuwa hawakusoma Misingi ya Upimaji. 

Majaji hawa walijitambua wao kama wazazi na kama Watanzania walipaswa kuwafundisha vijana wa taifa hili mpaka leo hii binafsi ninawatambua majaji 10 na wanasheria kedekede ninaowakumbuka kwa majina yao wakipitia kwa ndugu hawa katika kufundishwa masomo ya shahada ya kwanza za sheria. Mhadhiri kama mzazi hilo lazima atambue , kama hatambui basi hapaswi kuwa mlezi wa vijana wetu katika mafunzo yoyote yale.

Namshauri Mkuu wa Shule ya Sheria Tanzania ajiondoe mwenyewe katika nafasi hiyo kwa kushindwa kutimiza majukumu yake ipasavyo katika taasisi hii ya umma. Kama akishindwa kufanya hivyo basi aondolewa mapema maana uwepo wake una madhara makubwa kwa jamii ya Watanzania katika taaluma ya sheria.

Ajiuliza hili, wazazi wamewekeza pesa kwa watoto wao na taifa limewekeza rasimali kadhaa chuoni hapo nia siyo kutoa sifuri kwa wanachuo zaidi ya 600, kumbuka ada ya shilingi 1,570,000/- kwa wanachuo 600 karibu shilingi 942,000,000/- na pia shilingi 400,000/- kwa mwezi zidisha kwa miezi 12 mara idadi ya wanachuo 600 jumla kuu ikiwa ni shilingi 2,880,000,000/-kwa kodi ya chumba na chakula pekee, hapo tu jumla kuu ni shilingi 3,828,000,000/- zimepotea bila ya kupata cheti cha mafunzo hayo kwa wanachuo 600.Huo ni mzigo mkubwa lazima mwanakwetu huyu awajibike tena haraka mno.

Kitendo cha kufelisha namna hiyo kinaweza kuwavunja moyo wazazi na wanafunzi wengine kutokusoma kozi hii na hilo siyo jambo zuri na binafsi naamini siyo kusudio la serikali yetu kugaramia kuanzishwa kwa shule hii ya sheria. Baada ya kuondolewa mkuu wa chuo hiki mafunzo yasitishwe kwa muda alafu wahadhiri wote wa chuo hiki wapelekwe Chuo KIkuu cha Dar eS Salaam Idara ya Elimu wafundishwe mafunzo ya ualimu kwa muda hasa hasa kozi ya Misingi ya Upimaji huku mkuu wa chuo hiki mpya na yeye akiwemo mafunzoni hapo alafu shule ya sheria ifunguliwe upya na hali ya kufelisha wanachuo kama hawa haitojirudia tena.

Nimalizie kwa kusema kuwa sasa ni wakati sahihi kuchunguza zaidi wale walioishawishi serikali kuanzishwa shule hii kama walikuwa na nia njema au la? Hoja hii ya shule ya sheria imenikumbusha kumsimulia msomo wangu juu ya somo la Misingi ya Upimaji.


makwadeladius @gmail.com

0717649257



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...