Na Mwandishi wetu Dodoma
Serikali kupitia Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) imesema katika kipindi cha mwaka wa Fedha 2021/2022, Imeanzisha madarasa 406 ya kisomo ambapo yamenufaisha jumla ya wanakisomo 5,777.
Madarasa hayo yalifunguliwa katika shule za msingi za umma katika mikoa mbalimbali ya Tanzania bara na yamekuwa yakitumika kama vituo vya mafunzo kwa vitendo na utafiti kwa walimu wanafunzi wa TEWW.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 24,2022 jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Taasisi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023, Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) Dkt. Michael Ng'umbi
amesema kuwa wanaendelea kutoa elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi na kuboresha miundombinu ya ufundishaji na ujifunzaji katika mikoa 26 ya Tanzania Bara, ambapo jumla ya wanafunzi 15,130 (wakike 8,550 na wakiume 6,580) wanaendelea kupatiwa mafunzo hayo.
Dkt.Ng'umbi amesema kuwa TEWW Imeanzisha vituo vinane (8) vipya vya mafunzo na mitihani kwa walimu na wasimamizi wa elimu ya watu wazima wanaojifunza kwa njia huria na masafa katika ngazi za astashahada na stashahada, na kufikisha vituo 77 nchi nzima.
Pia Taasisi hiyo Imefanikiwa kuboresha mazingira ya tafiti kwa kuanzisha jukwaa la kuwasilisha mapendekezo pamoja na ripoti za tafiti.
"Kupitia jukwaa hilo takribani ripoti 12 za tafiti zilizofanywa na wanataaluma wa TEWW ziliwasilishwa. Aidha, baadhi ya tafiti hizi zimezalisha makala zilizochapishwa katika Toleo Na.23 la jarida la elimu ya watu wazima “JAET” lenye ISSN 2738-9243,"Amesema Dkt.Ng'umbi
Aidha,Mkurugenzi huyo amesema kuwa wamekusanya takwimu za hali ya kisomo kutoka mikoa yote ya Tanzania bara na inaendelea na uchambuzi wa taarifa na takwimu hizo ikiwa ni hatua ya mwanzo ya utafiti wa hali ya kisomo na elimu kwa umma nchini.
"Katika mwaka 2022/2023 TEWW itaendelea kutekeleza majukumu yake katika eneo hili, ikiwa ni pamoja na kuendelea kuwatumia wanachuo wake katika kufungua vituo vya kisomo nchi nzima ikiwa ni sehemu ya mafunzo kwa vitendo,"Ameeleza Dkt.Ng'umbi
Na kuongeza kuwa " kwa 2022/2023, TEWW itaendelea kushirikiana na Wizara ya Elimu Sayansi na Tekonolojia katika kuandaa Juma la Elimu ya Watu Wazima kwa mwaka 2023. Vile vile, TEWW itahamasisha, kusajili na kufundisha wanafunzi 3,000 wa mradi wa SEQUIP kwa mwaka 2023,"Dkt.Ng'umbi
Hata hivyo,Dkt.Ng'umbi ametoa wito kwa wananchi kujiunga na programu za elimu ya watu wazima zinazotolewa na TEWW kwa sababu ni taasisi inayotoa elimu kwa nadharia na vitendo kwa kumjengea mwanafunzi uwezo wa kuwa mtu bora, mwenye uwezo wa kujiendeleza na kupambana na changamoto za maisha.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) Dkt. Michael Ng'umbi,akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 24,2022 jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Taasisi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...