Na Faustine Gimu Galafoni,Kagera
Katika kuhakikisha maeneo mbalimbali ya mipakani yanakuwa salama dhidi ya magonjwa ya mlipuko kutoenea zaidi kutoka nchi moja hadi nyingine,Wizara ya Afya imejidhatiti kwa kuweka sheria na taratbu mbalimbali za afya kwa maeneo ya mipaka na mwingiliano mkubwa wa watu ikiwemo kituo cha utoaji wa huduma kwa pamoja Rusumo mkoani Kagera kinachounganisha nchi ya Tanzania na Rwanda.
Akizungumza na waandishi wa Habari mara baada ya kutembelea katika mpaka huo,Afisa Afya mfawidhi kutoka Mpaka wa Rusumo Oswad Kimasi amesema katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo Ebola abiria wote wanaofika mpaka wa Rusumo hatua ya kwanza ni kunawa mikono kwa maji tiririka na taratibu zingine kufuatwa ikiwemo kupimwa joto na kupatiwa vipeperushi vyenye ujumbe kuhusu masuala ya afya.
“Abiria anapofika hapa kwanza kabisa ananawa mikono kwa maji tiririka na hatua zinazofuata ni vipimo kisha tunatoa vipeperushi pamoja na elimu ya afya kwa wasafiri wote wanaoingia katika mpaka huu”amesema.
Kwa upande wake meneja wa mpaka, kituo cha utoaji wa huduma kwa pamoja Rusumo ambaye pia ni Afisa kutoka mamlaka ya mapato Tanzania[TRA]kituoni hapo Mohammed Mnonda amesema kitengo cha afya kituo cha utoaji wa huduma kwa pamoja Rusumo kimepewa majukumu ya kuratibu shughuli zote zinazohusu afya ikiwemo kupima abiria na wajibu wa kutoa elimu juu ya magonjwa mbalimbali ya mlipuko .
“Katika mpaka wetu kila idara inawajibika mfano kuhusu suala la upimaji wa abiria kitengo cha afya kinahusika kituoni hapa kuhakikisha kila abiria anapimwa “amesema.
Naye mmoja wa abiria aliyekuwa anapita katika mpaka huo kati ya Tanzania na Rwanda Semakura Athuman amesema amekuwa na uelewa mkubwa kuhusu ugonjwa wa Ebola kutokana na serikali kupitia Wizara ya Afya ,Idara ya Kinga ,Kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma kuweka mkazo mkubwa wa utoaji wa elimu kila kona ya Tanzania.
“Kuhusiana na Ebola hii,mwanzoni nilikuwa sielewi lakini sasa najua dalili zake,mfano kutapika ,kutokwa damu,na pia nimejua sasa unaweza kuenezwa kwa kula wanyamapori kama vile nyani,na mara tu ya kufika hapa nimeona vipeperushi ,nikapatiwa elimu ya afya”amesema Athuman.
Afya mfawidhi kutoka Mpaka wa Rusumo Oswad Kimasi akizungumzia namna kituo cha utoaji wa huduma kwa pamoja kilivyojidhatiti katika utoaji wa huduma kwa kuzingatia taratibu na kanuni za afya kuepukana magonjwa ya mlipuko.
Tenki la maji lililowekwa kwa ajili ya kunawa maji tiririka mara abiria wanapofika kituo cha huduma kwa pamoja Rusumo
Meneja wa mpaka, kituo cha utoaji wa huduma kwa pamoja Rusumo ambaye pia ni Afisa kutoka mamlaka ya mapato Tanzania[TRA]kituoni hapo Mohammed Mnonda akizungumzia namna vitengo mbalimbali vinavyoshirikiana utoaji wa huduma kituoni hapo.
Mmoja wa abiria akipata akipimwa afya mara tu ya kufika kituo cha huduma kwa pamoja Rusumo na akihakikiwa yupo salama anaruhusiwa kuendelea na safari.
Sehemu ya daraja la Rusumo linalotenganisha mpaka baina ya nchi ya Tanzania na Rwanda.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...