NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
UJUMBE
wa Kamati ya Kudumu ya Sheria Ndogo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar,
ukiongozwa na mwenyekiti wake, Mhe. Mihayo Juma Nunga umetembelea ofisi za
Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) jijini Dar es Salaam hivi karibuni kwa nia
ya kubainisha masuala muhimu ya Fidia kwa Wafanyakazi.
Akizungumza
baada ya kukutana na Watendaji wa WCF wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu, Dkt. John
Mduma, Mwenyekiti huyo amesema ziara hiyo imewawezesha kupata uelewa mpana wa
namna Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi inavyotekelezwa.
“Kwetu
jambo hili ni geni bado halijatengenezewa utaratibu bora zaidi wa kuwalipa
fidia wafanyakazi waliopata changamoto kwenye maeneo ya kazi, Zanzibar tuko
katika maandalizi ya kutengeneza utaratibu wa jinsi gani Mfanyakazi atapata
fidia pindi anapoumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi, kwahivyo tukaona
tutembelee Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ambao wana uzoefu mkubwa katika
masuala haya.” Alifafanua Mhe. Nunga.
Alisema
wameona jinsi watu wengi walivyonufaika na uwepo wa WCF kwa hivyo ni wakati
muafaka kwa Zanzibar kuwa na Mfuko utakaotoa huduma bora kama ambavyo
wameshuhudia hapo WCF.
Naye
Mkurugenzi Mwendeshaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), Bw.Ali Nassor
Shaaban, alisema Mfuko huo uko katika maandalizi ya kuanzisha huduma kama hiyo
ya kufidia wafanyakazi wanaoumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi.
“Tumeona
kabla ya kuanzisha chombo hicho ni vema kujifunza kwa wenzetu WCF ili kujua
sheria na kanuni zake zilivyo ili tuwe katika nafasi nzuri ya kuanzisha chombo
chetu kitakachotoa huduma kulingana na mazingira ya Zanzibar.” Alifafanua.m
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dtk. John
Mduma amesema , WCF ina uzoefu wa miaka saba (7) katika masuala ya utoaji fidia
kwa wafanyakazi na imekuwa ni wakati mzuri wa kubadilishana mawazo ya namna
bora ya kuendesha vyombo hivi vya Fidia kwa Wafanyakazi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Sheria Ndogo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe. Mihayo Juma Nunga (kulia), akizungumza mbele ya Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dtk. John Mduma wakati wa ziara ya kamati hiyo na watendaji wa ZSSF kwenye ofisi kuu za WCF jijini Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...