Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imetangaza kufunga mauzo ya hati fungani yake iliyofahamika kama NBC Twiga Bond kwa mafanikio makubwa ambapo benki hiyo imefanikiwa kukusanya kiasi cha sh Bil 38.9 ikilinganishwa na sh bil 30 zilizotarajiwa kukusanywa hapo awali. Mafanikio hayo ni asilimia 130 ya malengo yaliyotarajiwa..
Akizungumza kwenye hafla fupi ya utangazaji wa matokeo ya mauzo ya hati fungani hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam leo na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta fedha nchini wakiwemo wawakilishi kutoka Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mkurugenzi wa Biashara wa Benki ya NBC, Elvis Ndunguru alisema dhamana hiyo ya mwezi mmoja ilifungwa rasmi Disemba 7 mwaka huu kwa mafanikio makubwa ikilinganishwa na matarajio ya benki hiyo.
“Awali lengo letu lilikuwa ni kukusanya takribani kiasi cha bilioni 30 na tumefunga hati fungani hii tukiwa tumefanikiwa kukusanya kiasi cha sh Bil 38.9 ambayo ni sawa na asilimia 130 ya malengo yetu ya awali. Kiasi kilichopatakana kimetoka kwa wawekezaji takribani 661 kutoka sekta mbalimba ikiwemo wawezekazi binafsi wakubwa kwa Watoto chini ya usimamizi wa wazazi ,taasisi na mashirika mbalimbali kutoka kila kona ya nchi,’’ alibainisha Bw Ndunguru.
Kwa mujibu wa Bw Ndunguru, hiyo ni mara ya kwanza kwa Benki kutoa hati fungani kwa ajili ya umma na ikiwalenga Wajasiriamali, wakulima na wafanyabiashara wadogo ambao ndio sehemu kubwa ya ajira za vijana nchini Tanzania.
“Wawekezaji katika Hati fungani ya NBC Twiga Bond watapata riba kubwa ya 10% kwa mwaka, inayolipwa nusu mwaka katika kipindi chote cha miaka mitano hadi Novemba 2027. Kiwango cha riba kinacholipwa hakina punguzo la kodi.’’ Alisema.
Hati fungani ya Twiga ni ya kwanza kutolewa na Benki ya NBC na inatarajiwa kushughulikia sekta nyingine muhimu za uwezeshaji kiuchumi, changamoto ya ufadhili wa mikopo midogo midogo na ya kati nchini.
Kwa mujibu wa Bw Ndunguru benki hiyo itaendelea kutangaza hati fungani zaidi kwa kuwa lengo ni kukusanya kiasi cha Sh 300Bn ambazo zitatumika katika kufadhili sekta ndogo na za kati, Kilimo na sekta nyinginezo muhimu kiuchumi nchini.
Akizungumzia zaidi mafanikio hayo Mkurugenzi wa Hazina na Masoko Benki ya NBC,Bw Peter Nalitolela alisema hati fungani hii imekua sehemu ya fursa kwa watanzania kuwa sehemu ya ukuaji wa benki hiyo huku akiongeza;“Mafanikio haya yanaonyesha imani kubwa waliyonayo watanzania kwa benki ya NBC na zaidi wanavutiwa na huduma za benki hii kongwe katika huduma za kifedha.,’’
Bw Nalitolela alitumia fursa hiyo kuwashukuru baadhi ya wadau ikiwemo Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana nchini (CMSA), Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Wakala wa mauzo ya dhamana hiyo, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) pamoja na wawekezaji wote kwa kufanikisha mchakato mzima wa mauzo ya dhamana hiyo.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Muwakilishi kutoka BoT, Bw Lameck Kakulu pamoja na kuipongeza benki hiyo kwa mafanikio hayo, alisema BoT imevutiwa zaidi na malengo ya Hati fungani hiyo inayolenga kupanua uwezeshaji (mikopo) wa bei nafuu kwa Wafanyabiashara wadogo na wa kati, Sekta ndogo na Kilimo nchini.
“Wito wangu kwa taasisi nyingine za kifedha ni wao kuiga mfano huu wa NBC. Mafanikio haya hayaishii kwa benki husika bali yanakwenda kugusa wadau wengi zaidi wakiwemo wawekezaji wa hati fungani hii lakini kiupekee zaidi fedha hizi zitawafikia Wafanyabiashara wadogo na wa kati, Sekta ndogo na Kilimo nchini makundi ambayo ni muhimu sana katika uchocheaji wa ukuaji wa uchumi,’’ alisema.
Naye Mwakilishi Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) Bw Emmanuel Nyalali aliitaja alisema hivi karibuni hati fungani hiyo itaorodheshwa kwenye soko la hisa, hatua itakayotoa fursa kwa wadau mbalimbali kuweza kushiriki katika mauzo na manunuzi ya hisa za hati fungani hiyo.

Mkurugenzi wa Biashara wa Benki ya NBC, Elvis Ndunguru (wa tatu kushoto) sambamba na maofisa wengine kutoka benki hiyo pamoja na wawakilishi kutoka Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wakionesha takwimu za mafanikio yaliyopatikana kwenye mauzo ya hati fungani ya Benki hiyo ijulikanayo kama NBC Twiga Bond ambapo benki hiyo ilikukusanya kiasi cha sh Bil 38.9 ikilinganishwa na sh bil 30 zilizotarajiwa kukusanywa hapo awali. Hafla ya kutangaza matokeo ya mauzo ya hati fungani hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam leo

Mkurugenzi wa Biashara wa Benki ya NBC, Elvis Ndunguru (wa pili kushoto) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusiana na mafanikio yaliyopatikana kwenye mauzo ya hati fungani ya Benki hiyo ijulikanayo kama NBC Twiga Bond ambapo benki hiyo ilikukusanya kiasi cha sh Bil 38.9 ikilinganishwa na sh bil 30 zilizotarajiwa kukusanywa hapo awali. Hafla ya kutangaza matokeo ya mauzo ya hati fungani hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam leo. Sambamba nae ni pamoja na maofisa wengine kutoka benki hiyo pamoja na wawakilishi kutoka Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...