-Mto Ruaha washindwa kutiririsha Maji kwa siku 130.

Na Leandra Gabriel, Michuzi TV

FAMILIA 12 zimetajwa kuhusika na uharibifu wa Mto Ruaha Mkuu na kusabisha Mto huo kushindwa kutiririsha maji kwa siku 130 hadi sasa.

Akizungumza leo Mjini Iringa wakati wa kongamano la Wahariri na Wadau wa Uhifadhi Mazingira na Utunzaji wa vyanzo vya Maji lililoratibiwa na Kituo cha Wanahabari Watetezi wa Rasilimali na Taarifa (MECIRA,) Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF,) Deodatus Balile amesema familia 12 haziwezi kuitesa nchi kwa kukosa maji, umeme na kuharibu mazingira kwa ujumla hivyo watakabidhi majina hayo kwa Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango kwa hatua zaidi ili kunusuru Mto huo na vyanzo vingine.

Ameshauri mambo mawili kufanyika, moja ikiwa kuondoa familia hizo kumi na mbili na kujenga tuta kubwa litakalozuia wakulima na wafugaji kuingia na kutumia maji ya bonde la Ihefu.

Awali Mwenyekiti wa MECIRA Habibu Mchange alieleza, Serikali imetakiwa kufanya uamuzi mgumu ili kuokoa chanzo cha maji cha Bonde la Ihefu lililovamiwa na wawekezaji wakubwa wanaochepusha maji hayo kwenye mashamba yao.

Uchepushaji huo wa maji unadaiwa kuwa chanzo kikubwa cha kukauka kwa Mto Ruaha Mkuu unaotegemewa ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na kuzalisha umeme kwenye mabwawa ikiwamo Mtera, Kidatu na Mwalimu Nyerere.

Amesema ripoti ya mwaka 2019 zinaeleza asilimia 63 ya ardhi ya Tanzania imeharibiwa.

"Katika tafiti hiyo inaeleza asilimi 16 ya ardhi ya Tanzania ni jangwa...kwa ripoti hii Ruaha, Ruvuma, Malagalasi, Ruvuma na mito mingi hali itakuwa mbaya zaidi." Amesema.

Aidha amemwomba Makamu wa Rais kuzielekeza mamlaka zinazohusika na Uhifadhi kushirikiana na waandishi wa habari kwa kuhakikisha wanapata taarifa sahihi na kwa wakati.

Mchange amesema, kukutana na wadau hao kutatoka na maadhimio ya kutunza na umuhimu wa mazingira pamoja na kuandika taarifa sahihi.

Aidha MNEC Richard Kasesera amemwelekeza Mwenyekiti wa TEF kukabidhi majina hayo na wahusika wakamatwe na kushugulikiwa na atalipeleka katika baraza ili hatua zaidi zichukuliwe na kila mmoja ashiriki katika Uhifadhi na Utunzaji wa mazingira pamoja na vyanzo vya Maji.

Kongamano hilo limebeba kauli mbiu ya "Mazingira Yetu ni Uhai Wetu, Tuyalinde, Tuyatunze Tuishi."

Mwenyekiti wa Kituo Cha Wanahabari Watetezi wa Rasilimali na taarifa (MECIRA),
Habibu Mchange akiwasilisha taarifa kwenye Kongamano la Wahariri na Wadau wa Uhifadhi, Mazingira na utunzaji wa vyanzo vya maji lililofanyika leo Desemba 19,2022 katika ukumbi wa Masiti Gangilonga Mkoani Iringa, ambapo Mgeni rasmi alikuwa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Philip Isdori Mpango.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...