NA YEREMIAS NGERANGERA, NAMTUMBO
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma Chiriku Hamis Chilumba alisema amekamilisha ujenzi wa madarasa 17 kwa shule 11 zilizokuwa na upungufu wa vyumba vya kusomea katika Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo.
Chilumba alitanguliza shukrani zake kwa Raisi wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia Halmashauri ya Namtumbo fedha kiasi cha shilingi milioni 340 ili kuondoa changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha kwanza kwa mwaka 2023.
Michael Lyambilo Afisa elimu sekondari wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo alizitaja shule za sekondari zilizokamilisha ujenzi wa madarasa hayo kuwa ni shule ya sekondari Korido,Narwi,Nasuli /Suluti ,Luchili,Nahimba,Lisimonji na shule ya sekondari Msindo.
Lyambilo alizitaja shule zingine za sekondari zilizokamilisha ujenzi huo wa madarasa kuwa ni shule ya sekondari Nanungu,Selous,Namabengo pamoja na shule ya sekondari Magazini ambapo kwa sasa zipo tayari kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza pasipo kuwa na wasiwasi wa upungufu wa madarasa.
Afisa manunuzi wa Halmashauri hiyo Willy Ndabila kwa upande wake alidai pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika kukamilisha ujenzi wa madarasa 17 ya shule za sekondari 11 katika Halmashauri hiyo alizitaja changamoto alizokumbana nazo katika utekelezaji wa ujenzi kwa kutumia local fundi.
Ndabila alifafanua changamoto ya mafundi kuomba kazi ya ujenzi kwa kiasi kidogo cha fedha na wakishapata kazi ya ujenzi kwa kiwango alichokiomba na kubainika kuwa fundi huyo aliyepitishwa na kamati ya ujenzi kuwa ameomba kwa kiwango cha chini anategemea sehemu kubwa ya uendeshaji wa kazi hiyo kutegemea malipo kutoka Halmashauri licha ya mikataba kueleza bayana kuwa awe na uwezo kufanyakazi bila kutegemea malipo ya awali kutoka Halmashauri.
Lakini pia Ndabila alifafanua changamoto nyingine ya manunuzi ya bei ya soko katika jamii bado inawapa wakati mgumu na kutoeleweka katika jamii ,kwa madai kuwa wazabuni waliopewa zabuni kuhudumia vifaa vya viwandani hulipwa kwa cheki na hizo cheki zinakatwa kodi hali inayosababisha wakati mwingine kutonunua kwa bei ya soko kulingana na mazingira .
Hali hiyo kamati za ujenzi ,manunuzi,na usimamizi za vijiji hawaelewi hilo na kuelekeza lawama zao kwenye kitengo cha manunuzi cha Halmashauri na kudai watumishi wa kitengo hicho kuingia lawamani mara kwa mara kwa hoja ya kununua vifaa vya viwandani bei isiyo ya soko .
Hata hivyo Ndabila alisema Halmashauri inaendelea kutoa elimu kwenye kamati za ujenzi,manunuzi na usimamizi za vijiji ili ziweze kuelewa hilo na kushirikishana katika manunuzi ya vifaa vya viwandani ili kuondoa sintofahamu zinazojitokeza .
Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo ina jumla ya shule 33 za sekondari ambapo kati ya shule hizo, 25 ni za serikali , na 8 zisizo za serikali na shule 17 kati ya hizo 25 zilikuwa na upungufu wa madarasa na sasa zimekamilisha ujenzi wa madarasa kuondoa upungufu uliokuwepo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...