Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imetambulisha mfumo wa Usajili wa Watu kwa njia ya Mtandao (Online Registration) utakaowezesha Wananchi wenye sifa za kuomba Vitambulisho vya Taifa kwa Kujaza fomu mtandao mahali popote walipo bila kulazimika kwenda Ofisi za Usajili za Wilaya au vituo vya Usajili wa NIDA.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Desema 21,2022 jijini Dar es Salaam Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano NIDA, Geofrey Tengeneza amesema ili kujisajili kwa njia ya mtandao Mwombaji ataandika eonline.nida.go.tz katika mtandao wa internet na kufuata maelekezo.

"Mfumo huu unalenga kupunguza usumbufu kwa Woambaji wa Vitambulisho vya Taifa ambao kwa sasa wanalazimika kufika Ofisi za NIDA kuchukua fomu za maombi ya Vitambulisho vya Taifa kwani kupitia mfumo huu ujazaji wa fomu na kuweka viambatisho utafanyika mahali popote kwa kutumia kifaa chenye uwezo wa kupokea mtandao wa Mawasiliano (Intaneti)" ,amesema Tengeneza.

Amesema kuwa baada ya kujaza fomu mwombaji atatakiwa kuchapa fomu (print) na kuipeleka serikali ya Mtaa anapoishi kwa ajili ya kuthibitisha ukaazi wake kisha atatakiwa kupeleka fomu yake ofisi ya NIDA iliyoko katika Wilaya anayoishi akiwa na nakala ngumu za viambatisho alivyopakia katika mfumo ili kukamilisha utaratibu wa usajili kama vile kuhojiwa na Uhamiaji,kupigwa picha na kuchukuliwa alama za vidole.

Tengeneza amefafanua kuwa mfumo huo utapunguza muda unaotumika katika kusajili taarifa za mwombaji kwa kuwa usajili wa taarifa za mwombaji utakuwa umefanywa na Mwombaji mwenyewe.

"Pamoja na kurahisisha huduma ya usajili kwa Raia na Wageni Wakaazi,utapunguza pia gharama zinazotumika katika kuchapisha fomu za usajili na gharama za uchakataji wa taarifa",amesema Tengeneza

Amesema kuwa usajili kwa njia ya Mtandao utaongeza idadi ya Watu wanaojisajili kwa kuwa huduma hiyo itapatikana mahali popote badala ya kufika katika ofisi Ya NIDA kufuata huduma hiyo.

Kwa upande wake Meneja Usajili na Utambuzi (NIDA), Bi.Julien Mafuru amesema kumekuwa na malalamiko ya kukosewa kwa taarifa za uombaji vitambulisho hivyo kupitia mfumo huu utasaidia kupunguza kero hiyo kwani mwombaji atajaza taarifa zake mwenyewe.

Amesema wanaenda kupanua wigo wa kuwaandikisha watanzania ambao watakuwa nje ya nchi kwahiyo na wenyewe watapata faida ya kujaza foma moja kwa moja kwenye mtandao.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Bw.Geofrey Tengeneza akifafanua zaidi  mbele ya  waandishi wa habari leo Desemba 21,2022 katika ofisi za NIDA Jijini Dar es Salaam namna ya kujisalijili mtandaoni ili kupata kitambulisho cha Taifa.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Bw.Geofrey Tengeneza (katikati) akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 21,2022 Jijini Dar es Salaam, kushoto kwake ni Meneja Usajili na Utambuzi (NIDA), Bi.Julien Mafuru na kulia kwake ni Kaimu Mkuu Uratibu Ofisi za Wilaya NIDA, Bi.Brenda Kileo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...