NA
MWANDISHI WETU
BARAZA
la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA-CCC)
limesema litaendelea kuhakikisha ya kwamba watumiaji wa huduma za usafiri wa
anga Tanzania wanapata huduma kwa wakati na kufurahia safari zao.
Hayo
yamesemwa na Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Bw. Innocent Paul Kyara katika
Salamu zake za Mwaka Mpya wa 2023.
“Kama
kauli mbiu yetu inavyosema Haki zako, Maslahi yako ndiyo lengo letu, Mwaka 2023
tumejipanga zaidi kuendelea kuwawezesha na kuwawakilisha watumiaji kwa weledi
wa hali ya juu na tunategemea huduma bora zaidi kama watumiaji wa huduma za
usafiri wa anga Tanzania.” Alisisitiza Bw. Kyara.
Alisema
katika mwaka 2022 sekta ya usafiri wa anga iliendelea kuboreka baada ya kupitia
katika kipindi kigumu kutokana na athari za mlipuko wa ugonjwa wa Homa ya Uviko
19 (Covid19). Ikumbukwe sekta ya usafiri wa anga ni miongoni mwa sekta
zilizoathirika kwa kiasi kikubwa na ugojnwa huu.
Alisema
kwa wakati huu ambao TCAA-CCC inaelekea mwishoni mwa mwaka 2022 na kuanza mwaka
mpya 2023, ni wakati sahihi wa kufanya tathmini ya yale yaliyotokea katika
mwaka unaoisha na kubaini maeneo ambayo taasisi ilifanya vizuri na maeneo
ambayo palijitokeza changamoto kwa lengo la kuweka mikakati ya kuboresha katika
mwaka ujao.
Katika
mwaka huu tumeshuhudia kuongezeka kwa idadi ya watumiaji kwa maana ya abiria na
mizigo bila kusahau miruko ya ndege hapa nchini kwetu kulinganisha na kipindi
kilichopita,
Hatua
hii inatokana na jitihada mbalimbali zilizofanywa na Serikali ikiwemo Kampeni
iliyoendeshwa na Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, ya kuvutia watalii nchini kwetu kupitia filamu ya Royal Tour.
Jitihada
nyingine zilizofanywa na Serikali ni kuweka mazingira mazuri ya kufanya
biashara na kuvutia wawekezaji katika sekta mbalimbali. Ikumbukwe Sekta ya
usafiri wa anga ni sekta muhimu ya kuchochea ukuaji wa sekta nyingine.
Aidha,
ujenzi na upanuzi wa viwanja vya ndege unaohusisha njia za kurukia ndege na
majengo ya abiria ni hatua zinazohitaji pongezi kubwa kwa Serikali.
Tukichukulia mfano mmoja, kuanza kwa Ujenzi wa Kiwanja cha Kimataifa cha
Msalato Mkoani Dodoma, uwanja wa ndege ambao utaruhusu ndege kubwa zinazochukua
abiria wengi kwa wakati mmoja kuweza kutua katika mkoa huu wa Dodoma, ambao
ndio makao makuu ya Serikali na Nchi yetu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...