Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV

Bingwa mtetezi wa Michuano ya Kombe la Dunia, timu ya taifa ya Ufaransa imetinga hatua ya Nusu Fainali ya Michuano hiyo inayoendelea nchini Qatar baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya timu ya taifa ya Uingereza.

Mchezo huo wa Robo Fainali ya mwisho uliopigwa kwenye dimba la Al Bayt, Ufaransa walifanikiwa kupata bao la kwanza kupitia kwa Kiungo Mkabaji, Aurélien Tchouaméni katika dakika ya 17’ baada ya kupiga ‘shuti’ kali lililomshinda Golikipa wa Uingereza, Jordan Pickford na kujaa wavuni.

Uingereza walisawazisha bao hilo kwa mkwaju wa Penalti kwenye dakika ya 54’ kupitia kwa Mshambuliaji wao, Nahodha Harry Kane ikiwa baada ya Mshambuliaji Bukayo Saka kuchezewa ‘rafu’ na Tchouaméni kwenye eneo la hatari.

Bingwa mtetezi, Ufaransa ameendelea na dhamira yake ya kubeba tena ubingwa wa Kombe la Dunia baada ya kupata bao la pili katika dakika ya 77’ kupitia kwa Mshambuliaji Olivier Giroud ambaye alifunga bao safi kwa kutumia Kichwa chake.

Nahodha wa Uingereza, Harry Kane hakuwa na bahati katika mchezo huo baada ya kukosa mkwaju wa Penalti katika dakika ya 83’ ya mchezo, akipaisha juu ya lango la Ufaransa na kushindwa kusawazisha bao la hilo katika dakika hizo za majeruhi.

Kwa matokeo hayo, Ufaransa watacheza dhidi ya Morocco katika Nusu Fainali ya pili, Desemba 14, 2022 kwenye dimba la Al Bayt wakati Nusu Fainali ya kwanza, Desemba 13, 2022 itawakutanisha Argentina dhidi ya Croatia kwenye dimba la Lusail.

Fainali ya Michuano hiyo ya dunia itachezwa Desemba 18, 2022 kwenye dimba la Kimataifa la Lusail lenye uwezo wa kuchukua Watazamaji 80,000 (Elfu themanini).



 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...