Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na ongezeko la ubunifu katika mifumo ya uendeshaji wa shughuli za kifedha duniani kote kutokana na maendeleo ya teknolojia. Mojawapo ya ubunifu unaotawala katika mijadala ya kisasa ya kisera ni fedha ya kidijitali ya benki kuu (Central Bank Digital Currency [CBDC]).
Ijapokuwa
inafafanuliwa kwa njia mbalimbali, CBDC ni aina ya fedha ya kidijitali
katika nchi inayotolewa na kudhibitiwa na benki kuu. Kwa hiyo,
inapotolewa, CBDC inakuwa fedha halali, sawa na fedha ya kawaida
inayoshikika. Kulingana na maandiko mbalimbali ya kitaalamu, CBDC
inaelezwa kuwa na faida nyingi kwa uchumi.
Kwa kuzingatia ukweli
kwamba CBDC inaweza tu kutolewa na benki kuu, hivyo, kuwa chini ya
mamlaka yake, Benki Kuu ya Tanzania imekuwa ikitafiti uwezekano wa kutoa
CBDC yake. Katika hatua hii ya utafiti, Benki Kuu ya Tanzania iliunda
timu ya wataalamu wa fani mbalimbali kuchunguza vipengele vya
kiutendaji vya CBDC na kuijengea uwezo timu hiyo kwa njia mbalimbali.
Pia, katika kuongeza uelewa wa CBDC kwa umma, Benki Kuu ya Tanzania iliandaa Mkutano wa 20 wa Taasisi za Fedha nchini Tanzania mwaka 2021 ukiwa na mada kuhusu CBDC na fedha za kidijitali (crypto). Aidha, Benki Kuu ya Tanzania ilikutana na wadau wa sekta ya fedha nchini ili kupata maoni yao kuhusu suala hili.
Pia,
Benki Kuu imenufaika na mikutano mbalimbali ya kimataifa kama vile ya
Kamati ya Magavana wa Benki Kuu ya Sekretarieti ya Jumuiya ya Maendeleo
Kusini mwa Afrika (SADC), Kamati ya Masuala ya Fedha ya Sekretarieti
ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF)
kupitia Kituo cha IMF cha kanda (IMF AFRITAC), na Muungano wa Benki Kuu
za Afrika. Benki Kuu ya Tanzania pia ilifanya vikao kadhaa na kampuni
binafsi za kimataifa zinazotoa miundombinu na ufundi kwa CBDC.
Mambo
muhimu yaliyozingatiwa wakati wa hatua hii ya utafiti ambayo Benki Kuu
ya Tanzania inaendelea nayo ni kuchagua namna inayofaa katika kutumia
CBDC
kulingana
na muktadha wa Tanzania. Hii inahusisha aina ya CBDC itakayotolewa
(jumla, rejareja au mchanganyiko wa zote mbili), miundo ya utoaji na
usimamizi (ya moja kwa moja, isiyo ya moja kwa moja, au ya mseto), aina
ya CBDC (token-based au account based), muundo (remunerated au
non-remunerated) na kiwango cha uwazi au ufuatiliaji. Aina
itakayochaguliwa inapaswa kuzingatia vihatarishi vya utoaji wa fedha ya
kidijitali ya benki kuu na njia za kudhibiti hivyo vitahatarishi katika
utoaji na utumiaji wa fedha hiyo.
Matokeo ya utafiti uliofanywa
na Benki Kuu ya Tanzania yalibainisha kuwa zaidi ya nchi 100 duniani
ziko katika hatua tofauti za kutaka kutumia fedha ya kidijitali ya benki
kuu, 88 zikiwa katika utafiti, 20 katika uthibitisho wa dhana, 13
katika majaribio na 3 katika uzinduzi. Uchambuzi wa matokeo haya
unaonyesha kuwa benki kuu nyingi duniani zinakwenda kwa tahadhari
katika utekelezaji wa mpango wao wa kutaka kutumia fedha ya kidijitali
ya benki kuu (CBDC) ili kuepuka hatari zozote zinazoweza kuvuruga
utulivu na usalama wa uchumi wao.
Pia, ilionekana kuwa, nchi 6
zilighairi kutumia CBDC hasa kutokana na changamoto za kimuundo na
teknolojia katika awamu ya utekelezaji. Changamoto za kimuundo ni
pamoja na kutumia fedha taslimu katika kufanya miamala, kuwepo kwa
mifumo isiyofaa ya malipo, gharama kubwa ya utekelezaji na viashiria
vya hatari vya mfumo wa utoaji wa fedha uliopo.
Katika
kuzingatia hili, Benki Kuu ya Tanzania imeamua kutumia mbinu ya kwenda
hatua kwa hatua, ikichukua tahadhari na kuzingatia vihatarishi katika
kutumia fedha ya kidijitali ya benki kuu. Benki Kuu ya Tanzania
itaendelea kufuatilia, kutafiti na kushirikiana na wadau, zikiwemo
benki kuu nyingine, katika jitihada za kufikia matumizi ya fedha ya
kidijitali ya benki kuu na kuchagua teknolojia stahiki kwa ajili ya
utoaji wa
shilingi ya Tanzania katika mfumo wa kidijitali. Baada
ya kuhitimisha awamu ya utafiti, Benki Kuu ya Tanzania itatoa taarifa
kwa umma kwa ujumla juu ya namna ya kusonga mbele. Taarifa hiyo inaweza
kujumuisha mpangokazi katika kuanzisha fedha ya kidijitali ya benki
kuu (CBDC) nchini.
KURUGENZI YA USTAWI NA UJUMUISHI WA KIFEDHA
BENKI KUU YA TANZANIA
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...