Na MWANDISHI WETU

Mali za kampuni ya uzalishaji wa maji ya chai ya Rift Valley Tea Solution Limited ambayo ni mitambo ya uzalishaji majani ya chai zimepigwa mnada na Kampuni ya udalali wa Mahakama FreedomPath Tanzania Limited kwa idhini ya Mahakama ya Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam katika shauri la madai namba 93/2022.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, leo Januari 23, 2023, Mkurugenzi Mtendaji wa FreedomPath Tanzania Limited, Deusdedit Kabunduguru, alisema katika shauri hilo mdai ni Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) dhidi ya kampuni hiyo ya Rift Valley Tea Solution Limited ambaye alishindwa kuwasilisha fedha za michango ya wafanyakazi wake NSSF ambapo Mfuko uliamua kufungua kesi Mahakamani ili mwajiri huyo aweze kulipa michango ya wafanyakazi wake ambayo ipo kwa mujibu wa sheria.

“Leo tulikuwa tunashughuli ya kuendesha mnada wa hadhara kwa maelekezo ya Mahakama ya Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam, ambapo ilikuwa ni kesi namba 93/2022 mdai akiwa ni Bodi ya NSSF dhidi ya kampuni ya Rift Valley Tea Solution Limited ambapo mdaiwa huyo alishindwa kuwasilisha fedha za michango ya wafanyakazi wake na NSSF iliamua kufungua kesi Mahakamani ili aweze kulipa michango ya wafanyakazi,” alisema.

Kabunduguru alisema wanashukuru wameweza kupata mshindi wa mnada huo na  kuwa NSSF inaweza kupata fedha za michango ya wanachama na hatimaye wafanyakazi wa kampuni hiyo wataweza kupata haki zao.

“Nitoe rai kwa waajiri kuhakikisha wanawasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa wakati ili kuepuka madhila kama haya,” alisema.

Kabunduguru alisema NSSF ilikuwa inaidai kampuni hiyo michango ya zaidi ya Shilingi milioni 226 ambapo wafanyakazi wa kampuni hiyo walikuwa hawajaingiziwa michango kwa zaidi ya miaka mitatu.

Naye, Geofrey Sikira ambaye ni Kaimu Meneja Mwendesha Mashauri wa NSSF, alisema Mfuko kwa amri ya Mahakama imeuza mali ya mwajiri huyo baada ya kushindwa kulipa michango ya wanachama wake kwa mujibu wa sheria.

“Tunachofanya ni utaratibu wa kawaida kabisa, kwani mwajiri anaposhindwa kulipa michango ya wafanyakazi wake tunampeleka Mahakamani na tukishinda kesi hatua za kimahakama zinafuata ambazo ni kuuza mali za mwajiri kwa kutumia dalali wa Mahakama,” alisema Sikira.

Sikira alifafanua kuwa, mwajiri anapaswa kuwasilisha michango ya wanachama wake kila mwezi, na kwamba akikaa kwa miezi sita bila kuwasilisha michango ya wanachama anakuwa ni mdaiwa hivyo anachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa Mahakamani.

“Natoa wito kwa waajiri wa sekta binafsi kutii sheria kwa kulipa michango ya wafanyakazi wao kwa wakati ili waweze kuendelea na shughuli mbalimbali za uzalishaji kwenye kampuni zao,” alisema.

Kwa upande wake, Ramadhani Juma ambaye ameshinda mnada huo, alisema amenunua mtambo huo kwa shilingi milioni 167 na kuwa unaenda kuongeza thamani ya zao la chai kwa sababu utaenda kuchakata chai na kuiweka katika soko la kimataifa.Mkurugenzi Mtendaji wa FreedomPath Tanzania Limited, Deusdedit Kabunduguru akipiga mnada Mali za kampuni ya uzalishaji wa majani ya chai ya Rift Valley Tea Solution Limited ambayo ni mitambo ya uzalishaji majani ya chai.  NSSF kwa amri ya Mahakama imeuza mali ya mwajiri huyo baada ya kushindwa kulipa michango ya wanachama wake kwa mujibu wa sheria ili fedha hizo ziweze kutumika kulipa michango ya wanachama hao.
Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...