Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
Wekundu wa Msimbazi, Simba SC wanatarajiwa kucheza michezo miwili ya kirafiki wakiwa katika ardhi ya Falme za Kiarabu 🇦🇪, Dubai katika kambi yake ya kujiandaa na muendelezo wa Ligi Kuu Soka Tanzania msimu huu, Michuano ya Kombe la Shirikisho (ASFC) sanjari na Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF CL).
Simba SC wametoa ratiba ya kucheza na timu inayoshiriki Ligi Kuu katika Falme za Kiarabu, Al Dhafra FC katika mji wa Abu Dhabi, Januari 13, 2023 majira saa 11:00 jioni sawa na Saa 10:00 jioni nchini Tanzania huku mchezo wa pili wakitarajia kucheza majira kama hayo, mjini Abu Dhabi dhidi ya miamba ya soka nchini Urusi, CSKA Moscow.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally amenukuliwa akisema kuwa Kocha Mkuu wa Kikosi hicho, Roberto Oliveira (Robertinho) anataka kutumia michezo hiyo miwili ili kukiweka sawa Kikosi chake ambacho amekabidhiwa hivi karibuni kikiwa chini ya Kocha Juma Mgunda.
Ahmed amesema Kocha Robertinho anataka kutumia mchezo wa kwanza dhidi ya Al Dhafra FC ambao hawapo vizuri katika msimamo wa Ligi Kuu (UAE Pro League) huku akibainisha kuwa anataka kutumia mchezo wa pili dhidi ya CSKA Moscow kuwaweka sawa vijana wake katika siku hizo chache wakiwa katika Falme za Kiarabu.
Kikosi cha Al Dhafra FC kinaburuza mkia kikiwa nafasi ya 14 katika msimamo wa Ligi Kuu kwenye Falme za Kiarabu (UAE Pro League) yenye timu 14 msimu huu wa 2022-2023. Al Dhafra FC wana alama nne (4) pekee kwenye michezo 12 waliyocheza hadi sasa, wamepoteza michezo 10, wameshinda mchezo mmoja (1) pekee na kupata sare mchezo mmoja (1).
CSKA Moscow wapo katika Falme za Kiarabu (UAE) kwa kambi maalum, katika msimamo wa Ligi Kuu nchini Urusi, CSK Moscow wanashika nafasi ya tano wakiwa na alama 29, wamecheza michezo 17 katika Ligi hiyo, wameshinda michezo nane (8), sare tano (5) na kufungwa michezo minne (4) pekee.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...