Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
Taasisi mbalimbali katika Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi zimeaswa kutoa kibali na kuwaruhusu Watumishi wao kushiriki katika mazoezi yanayoandaliwa kupitia Mabonanza mbalimbali ili Watumishi hao wafanye mazoezi na kuimarisha afya zao.
Agizo hilo limetolewa leo, Januari 21, 2023 na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Mhe. Atupele Mwakibete katika Bonaza la Sekta ya Uchukuzi lililodhaminiwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) lililofanyika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
“Kumekuwa na changamoto kwa Wakuu wa Taasisi kutowaruhusu Watumishi kushiriki Mabonanza ambayo yanaandaliwa mahsusi kufanya mazoezi, naomba nitoe rai kwa Wakuu wa Taasisi katika Wizara ya Uchukuzi, muwaruhusu Watumishi Wanamichezo washiriki mazoezi,” amesema Mhe. Mwakibete.
“Miaka ijayo tutaongeza fedha kwenye Bajeti zijazo ili wale wanaopenda michezo waruhusiwe kushiriki kwa manufaa ya afya zao,” ameongeza Mwakibete
Aidha, Mhe. Mwakibete amewapongeza Watumishi wa Sekta ya Uchukuzi kwa kuandaa na kushiriki Bonanza hilo ambalo limeonyesha dhahiri namna wanavyotekeleza agizo la Mhe. Rais Dkt. Samia Suhuu Hassan la kuhamasisha Watumishi na Wananchi mbalimbali kufanya mazoezi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) CPA. Habibu Suluo amemshukuru Mhe. Mwakibete kwa kujumuika nao pamoja kwenye bonanza hilo, huku akisisitiza kuwa michezo ni afya, inaleta umoja na inaongeza ufanisi katika maeneo ya kazi.
“Ushiriki wako hapa leo umetupa nguvu kubwa ya kuendeleza michezo hii na tunaahidi kuendeleza ushirikiano huu uliopo miongoni mwetu kupitia michezo,” ameeleza CPA Suluo .
Naye Katibu wa Klabu ya Uchukuzi Bw. Mbura Tenga amesema hilo ni bonanza la tano kuandaliwa na Sekta ya Uchukuzi na ameishukuru LATRA kwa kudhamini kwa asilimia 100.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Mhe. Atupele Mwakibete akizungumza na Watumishi mbalimbali wa Sekta ya Uchukuzi katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) CPA. Habibu Suluo akizungumza kwenye Bonanza hilo lililofanyika katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) CPA. Habibu Suluo akizungumza kwenye Bonanza hilo lililofanyika katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...