Na. Damian Kunambi, Njombe

Kufuatia kuanza kwa miradi midogo ya uchimbaji madini ya makaa ya mawe wilayani Ludewa mkoani Njombe huku miradi mikubwa ya Liganga na Mchuchuma ikitarajiwa kuanza hivi karibuni shirika lisilo la kiserikali Umbrella of Women and Disabled organization (UWODO) limewasili wilayani humo kwa lengo la kuendesha mradi wa utoaji elimu juu ya utunzaji mazingira na uoto wa asili katika maeneo hayo ya miradi.

Akizungumza mara baada ya kuzindua mradi huo wa utunzaji mazingira na uoto wa asili Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo Sunday Deogratias amelipongeza shirika hilo kwakuwa limekuja katika kipindi ambacho kuna uhitaji hasa wa elimu hiyo.

"Niwapongeze sana UWODO kwa kuleta mradi huu katika Halmashauri yetu, kwani jambo hili lilipaswa kuwa la serikali lakini nanyi pia kwa kutambua umuhimu wake mmeona vyema kuiunga mkono serikali hivyo niwaahidi kuwa mimi na watendaji wangu tuko tayari kushirikiana nanyi katika kila hatua ili tuweze kufanikisha hili". Amesema Deogratias.

Hamis Kassapa ni Mkurugenzi wa shirika hilo la UWODO amesema mradi huo umefadhiliwa na ubalozi wa ujerumani kupitia shirika la PELUM TANZANIA ambapo unatarajiwa kutekelezwa kwa kipindi cha mwaka mmoja wilayani humo.

"Huu mradi utakuwa na awamu mbili ambapo awamu ya kwanza tutaanzia kutoa elimu katika kata ya Luilo na Nkomang'ombe na awamu ya pili tutatoa katika kata ya Mundindi". Amesema Kassapa.

Amesema tayari wamekwisha zungukia baadhi ya maeneo ambayo yameanza uchimbaji na kukuta tayari kuna athari ndogo ndogo ambazo zimekwisha anza kujitokeza hivyo kupitia elimu hii itawawezesha wananchi pamoja na kamati za mazingira kutambua wajibu wao katika kuhakikisha mazingira hayo hayapati uharibifu zaidi.

"Mara nyingi wawekezaji wamekuwa wakijali zaidi faida wanayopata pasipo kuangali athari wanazowaachia wananchi kwani wamekuwa wakiharibu uoto wa asili,vyanzo vya maji samamba na kuacha mashimo katika machimbo kitu ambacho ni uharibifu wa mazingira kwa ujumla". Amesema Kassapa.

Aidha mradi huo umeonekana kupokelewa vyema na viongozi mbalimbali wa wilaya na kata husika akiwemo diwani wa kata ya Nkomang'ombe John Maganga pamoja na diwani wa kata ya Luilo Mathei Kongo huku wakisema kuwa elimu hii itasaidia kuleta mabadiliko makubwa kwa jamii na kufanya uwekezaji usio na madhara..Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...