Na Immaculate Makilika – WHMTH

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa, Mhandisi Kundo Mathew amesema kuwa Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) inatarajia kutumia zaidi ya shilingi bilioni mbili kujenga minara ya huduma za mawasiliano katika kata za Jimbo la Kilombero lililopo mkoani Morogoro.

Ambapo gharama ya ujenzi wa mnara mmoja wa huduma za mawasiliano unakadiriwa kuwa takribani shilingi milioni 300. Aidha, gharama ya ujenzi huongezeka kutokana mazingira ya eneo husika.

Akizungumza jana (Januari 7, 2023) wakati alipokuwa akihutubia wananchi wa Kijiji cha Katurukila kilichopo Kata ya Mkula mkoani Morogoro, Naibu Waziri huyo, amesema kuwa lengo la ziara yake kijijini hapo ni kukagua upatikanaji wa huduma ya mawasiliano na kueleza nia ya Serikali ya kutatua changamoto ya mawasiliano iliyopo katika kata hiyo. Aidha, Jimbo la Kilombero limepata zaidi ya minara saba ya huduma za mawasiliano itakayojengwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni mbili.

“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha kwa ajili ya kujenga minara ya huduma za mawasiliano katika Kata ya Mkulo yenye vijiji sita na idadi ya wakazi wanaokadiriwa kufikia 9,000 kabla ya majibu ya Sensa ya mwaka 2022, ambavyo ni vijiji vya Mgombera, Katurukila, Sole, Msafiri, Sonjo pamoja na Mkulo ili kutatua changamoto ya mawasiliano inayowakabili”. Amesema Naibu Waziri Mheshimiwa Mhandisi Kundo.

Ameongeza kuwa zabuni ya miradi ya maeneo hayo ilitangazwa na Serikali kupitia UCSAF mwezi Oktoba mwaka 2022 na zabuni hiyo inatarajiwa kufunguliwa Januari 31, 2023 ambapo kampuni ya simu za mkononi itakayoshinda zabuni hiyo itapewa kazi ya kujenga minara na kuhakikisha huduma ya mawasiliano imeimarika katika kata hizo.

Aidha, Naibu Waziri Mheshimiwa Kundo amesisitiza kuwa Serikali inatambua changamoto ya mawasiliano iliyopo na kuwa imedhamiria kutatua changamoto hiyo ili wananchi waweze kutumia fursa za mawasiliano katika shughuli mbalimbali ikiwemo za biashara na uchumi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Bw. Khasim Nakapala amemshukuru Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya kutatua changamoto ya mawasiliano inayowakabili wananchi wa Kilombero.

“Namshukuru Mheshimiwa Rais na pia nakipongeza Chama cha Mapinduzi kwa kuwa kinaisimamia Serikali kutekeleza Ilani yake ili kutatua kero za wananchi. Changamoto hii ya mawasiliano imekuwepo hapa na viongozi mbalimbali wamepita, lakini Mbunge wa Jimbo la Kilombero, Mheshimiwa Abubakar Asenga alipoisema changamoto yetu hii, leo Serikali imekuja kutatua, namshukuru sana Mbunge wetu Mheshimiwa Asenga”. Amesema Bw. Nakapala.

Ameongeza kuwa mawasiliano ni huduma muhimu hivyo huduma za mawasiliano zitakapokamilika wananchi wa jimbo hilo watanufaika na huduma bora za matibabu pamoja na kusaidia wakulima kujisajili kwa kutumia mtandao ili kupata ruzuku ya mbolea.

Naye, Mratibu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Kanda ya Pwani, Mhandisi Mwandamizi Baraka Elieza amesema “Kata hii ya Mkula ilijumuishwa katika mradi wa Tanzania ya Kigiditali (DTP) ili kuboresha zaidi mawasiliano katika vijiji sita. Aidha, katika zabuni hii itakayofunguliwa Januari 31, 2023, UCSAF itahakikisha mtoa huduma atakayepata kata hii atatekeleza mradi huo kwa wakati ili kutatua changamoto za huduma za mawasiliano hasa Kijiji cha Katurukila na vijiji vingine”.



Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Mhandisi Kundo Andrea Mathew (MB) akiongea pamoja na kujibu maswali katika mikutano ya hadhara na Wananchi wa Kijiji cha Katurukila kilichopo Kata ya Mkula, pamoja Kijiji cha Mbalaji Kitongoji cha Mbalaji vilivyopo katika Jimbo la Kilombero Mkoa wa Morogoro katika ziara yake ya kukagua miradi ya mawasiliano, ubora na upatikanaji wa huduma za mawasiliano, usikivu wa TBC na uhakiki wa Anwani za Makazi Januari 7, 2023

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...