Na Said Mwishehe, Michuzi TV
SERIKALI ya Tanzania imeahidi kwamba iko tayari kuhakikisha inamaliza maambukizi mapya ya VVU kwa watoto ifikapo mwaka 2030 huku akitumia nafasi hiyo kuziomba nchi za Afrika kuimarisha sera, rasilimali fedha , kuondoa unyanyapaa na ndoa za utotoni ili kufikia lengo hilo.
Akizungumza leo jijini Dar Salaam kwenye uzinduzi wa mkakati wa kidunia wa kutokomeza UKIMWI kwa watoto ifikapo 2030 Kanda ya Afrika ,Makamu wa Rais Dk.Philip Mpango aliyekuwa mgeni rasmi kwenye mkutano huo akimwakilisha Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amesisitiza Tanzania imeajiandaa kukomesha maambukizi mapya kwa watoto ifikapo mwaka huo wa 2030.
Pamoja na mambo mengine Dk.Mpango ametumia mkutano huo kuwaomba wadau mbalimbali wakiwemo wa sekta binafsi kuongeza nguvu kuwafikia watoto wanaoishi na virusi vya UKIMWI kwani takwimu zinaonesha kati ya watoto milioni 1.7 wenye maambukizi watoto 800,000 hawajafikiwa na huduma za matibabu hali inayosababisha vifo kwa watoto hao.
"Tanzania inaahidi kufikia lengo hilo la kumaliza maambukizi ya VVU kwa watoto ifikapo 2030 na mkutano huu kupitia muungano wa nchi 12 za Afrika na wengine watakaokuja ulete chachu kufikia malengo haya,”amesema Dk.Mpango na kuongeza ili kufikia mpango huo lazima utoaji huduma za matibabu uwe kwenye uwiano ulio sawa kijinsia.
Awali akizungumza kwenye mkutano huo Makamu wa Rais wa Zimbabwe Dk.Constantine Chiwenge amesema kwenye nchi yao wameweka mikakati madhubuti ya kumaliza maambukizi na kwa sasa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI ni milioni 1.1 na wengi wao ni watoto wenye umri wa miaka 14.
"Kutokana na changamoto iliyopo tulikaa na kuweka mkakati madhubuti ili kukabiliana na maambukizi ya virusi vya UKIMWI na miongoni mwa mkakati tuliyochukua ni kumlinda mama mjazito anayeishi na VVU atakapojifungua mtoto awe salama kwa kutokuwa na maambukizi.
Wakati huo huo Mkurugenzi Mtendaji wa UN AIDS Winnie Byanyima amesema ripoti iliyotoka mwaka 2022 inaonesha watoto 96000 wamefariki dunia kutokana na ugonjwa huo na waliopata maambukizi mapya ni kwa watoto 160,000 hali ambayo inatisha na iko haja ya kuchukua hatua sahihi za kumaliza changamoto hiyo ifikapo mwaka 2030.
"Wadau wa sekta ya afya kutoka nchi mbalimbali za Afrika wamekutana kwa lengo la kutafuta suluhu ya kuondoa maambukizi ya vizuri vya UKIMWI kwa watoto.Kuondoa maambuzi kwa watoto ni jambo linalowezekana kwani Sayansi ipo na madaktari wapo, vifaa tunavyo lakini kilichokuwa kinakosema ni dhamira ya kweli, hivyo kupitia mkutano huu kila nchi imeeleza mkakati wake ili kufikia malengo hayo.”
Kwa upande wake Waziri wa Afya nchini Tanzania Ummy Mwalimu amesema Tanzania iko tayari kuondoa HIV kwa watoto na mpango uliopo uliopo ifikapo mwaka 2025 maambukizi yawe yamefikia asilimia nne na mwaka 2030 maambukizi yawe asilimia zero.
“Kudhibiti maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ni asilimia 11 kwa sasa pamoja na changamoto zilizopo mafanikio ni makubwa na watu ambao wamebainika kuwa na virusi vya UKIMWI wameendelea kupata matibabu,”amesema na kusisitiza kwa mikakati iliyopo Tanzania inakwenda kufikia lengo hilo.
Awali Mwakilishi wa vijana wanaoishi na virusi vya UKIMWI Pudensiana Mbwiliza amesema ili kukabiliana na maambukizi mapya ya VVU ni vema vijana wa kiume wasiachwe nyuma kwani ndio wazazi wa kesho na mara nyingi wamekuwa nyuma huku akitumia nafasi hiyo kusisitiza umuhimu wa kuendelea kuelimisha jamii kuhusu ugonjwa huo.“Pia jamii iondoe unyanyapaa wa kijinsia katika mapambano ya kukabiliana na UKIMWI.”
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...