Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
Wawakilishi wa Tanzania katika Michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika (CAFCC), Young Africans SC wamepagwa kucheza dhidi ya Rivers United ya Nigeria katika mchezo wa hatua ya Robo Fainali ya Michuano hiyo.
Yanga SC wataanzia ugenini katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa hatua hiyo utakaopigwa Aprili 23, 2023 nchini Nigeria wakati mchezo wa mkondo wa pili utachezwa jijini Dar es Salaam kwenye dimba la Benjamin Mkapa, Aprili 30, 2023.
Yanga SC, waliwahi kupoteza michezo miwili katika Michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika (CAFCL) hatua za awali, ambapo walifungwa bao 1-0 kwenye dimba la Benjamin Mkapa, Septemba 12, 2021 na mchezo wa marudiano Yanga SC walifungwa bao 1-0 nchini Nigeria.
“Walitufunga nyumbani na ugenini kwa sababu timu yetu ilikuwa pungufu kwa baadhi ya Wachezaji wetu kukosa vibali, lakini safari hii tunaenda kulipa kisasi, tutawafunga ndani na nje michezo miwili yote tutashinda,” amesema Rais wa Yanga SC, Mhandisi Hersi Said akihojiwa na Kituo cha Runinga cha Azam TV, Salamander Tower katika Ofisi za GSM, mtaa wa Samora jijini Dar es Salaam.
Yanga SC wamefika hatua hiyo baada ya kumaliza kwenye nafasi ya kwanza wakiwa na alama 13 kwenye Kundi D la Michuano hiyo ya CAFCC, wakiwa na timu za US Monastir ya Tunisia, US Real Bamako ya Mali na TP Mazembe ya DR Congo.
Endapo, Yanga SC watashinda mchezo huo wa Robo Fainali kwa matokeo ya jumla (nyumbani na ugenini), katika hatua ya Nusu Fainali ya Michuano hiyo watakutana na mshindi kati Pyramids FC ya Misri au Marumo Gallants FC.
KILA LA KHERI TANZANIA, KILA LA KHERI YANGA SC KWENYE MICHUANO YA KOMBE LA SHIRIKISHO AFRIKA.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...