Dkt. Geoffrey Hinton, ambaye ni mwanasayansi bingwa katika uwanja wa akili bandia (Artificial Intelligence - AI) duniani , amejiondoa katika nafasi yake kwenye kampuni ya Google ili aweze kuzungumzia kwa uhuru zaidi hatari za teknolojia hiyo. 

 

Dkt. Hinton amekuwa  “maarufu duniani kama Baba wa AI" kutokana na kazi yake kwenye mitandao ya neva, ambayo  dnio hii inayotumiwa sasa kwa kiasi kikubwa kufanikisha mifumo mbalimbali ya AI. 

 

Ingawa alikuwa akifanya kazi kwa mkataba hapo Google kwa miaka kumi katika maendeleo ya AI, Hinton amekuwa na wasiwasi juu ya hatari  na athari za AI , akisema kuwa ameondoka Google ili aweze kujadili hatari za AI kwa uhuru zaidi, bila kuwa na mipaka kutokana na athari za Google. 

 

Jeff Dean, mwanasayansi mkuu wa Google, ametoa shukrani yake kwa mchango wa Hinton kwa kampuni ya Google na maendeleo yake ya msingi katika uwanja wa AI.

 

Dkt. Hinton, ambaye  ni mwanasayansi bingwa wa kompyuta na utafiti wa ujifunzaji wa mifumo ya kidijitali ya akili bandia, amezaliwa tarehe 6 Desemba 1947, huko London, Uingereza. Yeye anaheshimiwa sana kama mmoja wa waanzilishi wa ujifunzaji wa kina, kundi dogo la ujifunzaji wa mashine ambalo limeendeleza tasnia ya akili bandia katika miaka ya hivi karibuni.

 

Uamuzi wa Dkt. Hinton kujiweka kando toka Google na kuzungumza juu ya teknolojia hio unakuja wakati idadi ya malalamiko na wasiwasi vikiongezeka, ambapo wanasiasa, makundi ya utetezi na wataalamu wa teknolojia wameonya juu ya uwezekano wa kikundi kipya cha “Watundu wa Mitandao” kinachotumia AI kueneza habari potofu na kuathiri kazi za binadamu. 

 

Wimbi la tahadhari kuhusu mtandao wa ChatGPT mwishoni mwa mwaka jana limesaidia kubuniwa kwa  mbinu za kujihami  kati ya makampuni ya teknolojia ili kutengeneza  na kutumia zana sawa za AI katika bidhaa zao. Kampuni za OpenAI, Microsoft na Google wako mstari wa mbele katika  mwelekeo huu, na pia IBM, Amazon, Baidu na Tencent wanafanya kazi kwenye teknolojia kama hizo.

 

Mwezi Machi mwaka huu, baadhi ya watu maarufu katika tasnia ya teknolojia walitia saini waraka maalumu unaotaka maabara za kutengeneza akili bandia kusitisha mafunzo ya mifumo yenye nguvu zaidi ya AI kwa angalau miezi sita, wakibainisha "hatari kubwa kwa jamii na ubinadamu." 

 

Barua hiyo, iliyochapishwa na Taasisi ya Future of Life, shirika lisilo la faida linaloungwa mkono na Elon Musk, ilitolewa wiki mbili tu baada ya OpenAI kutangaza GPT-4, toleo lenye nguvu zaidi hata ya teknolojia inayoendesha ChatGPT. 

 

Katika majaribio ya awali na demo ya kampuni, GPT-4 ilitumiwa kutunga mashitaka, kupitia mitihani iliyoratibiwa na kujenga wavuti inayofanya kazi kutoka kwa skrini iliyochorwa kwa mkono.

 

Mwanasayansi Hinton ni mmoja wa wanazuoni wakuu katika teknolojia, ambapo alipata Shahada yake ya  Uzamili katika akili bandia kutoka Chuo Kikuu cha Edinburgh tangia mwaka 1978. Kisha akajiunga na Kitivo cha Chuo Kikuu cha Carnegie Mellon na baadaye akahamia Chuo Kikuu cha Toronto, ambapo kwa sasa ni Profesa mhadhiri katika Idara ya Sayansi ya Kompyuta.

 

Dkt. Hinton ametoa mchango mkubwa katika uwanja wa ujifunzaji wa kina, ikiwa ni pamoja na maendeleo ya algorithmu ya backpropagation, ambayo ni sehemu muhimu ya mtandao wa neva wa kisasa. Pia ameendeleza mifano kadhaa ya ujifunzaji wa kina ambayo imekuwa na ushawishi mkubwa, ikiwa ni pamoja na mtandao wa imani wa kina na mitandao ya neva ya upakiaji, ambayo imekuwa ikitumiwa katika njia mbalimbali, kutoka kutambua picha na sauti hadi usindikaji wa lugha ya asili.

 

Dkt. Hinton amepokea tuzo na heshima nyingi kwa kazi yake katika akili bandia, ikiwa ni pamoja na Tuzo ya Turing mnamo 2018, ambayo mara nyingi huitwa "Tuzo ya Nobel ya Kompyuta." Pia ni mshirika wa Royal Society, mshirika wa Chama cha Ukompyuta, na mshirika wa Royal Society ya Canada.

 

 



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...