Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax ametoa wito kwa Taasisi mbalimbali nchini kuendelea kutunza kumbukumbu za historia ya Tanzania na mchango wake katika medani za kikanda na kimataifa ili kuvirithisha vizazi vya sasa na vijavyo.

Kauli hiyo ameitoa jijini Dodoma hivi karibuni wakati wa hafla fupi ya kikabidhi Machapisho ya Hashim Mbita kwa Taasisi 18 zikiwemo za elimu.

Mhe. Dkt. Tax amesema kuwa, Tanzania ina historia kubwa na nzuri katika medani za kikanda na kimataifa ikiwemo mchango wake katika harakati za ukombozi kusini mwa Afrika hivyo ni jukumu la wadau mbalimbali kuunganisha nguvu ya kutunza kumbukumbu ya historia hiyo nzuri na kuvirithisha vizazi vya sasa na vijavyo.

Ameeleza kuwa, Wizara imeamua kuyakabidhi machapisho hayo kwa Taasisi hizo ili yasaidie kurithisha historia iliyomo kwa vizazi vijavyo, na kujenga hamasa ya uzalendo kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

“Wizara inawakabidhi nyinyi machapisho haya kama wawakilishi wa wengi. Tunaamini kupitia Vyuo na Taasisi zenu machapisho haya yatawafikia na kusomwa na Watanzania wengi. Vilevile kupitia machapisho haya historia kuhusu mchango uliotolewa na Tanzania katika harakati za ukombozi wa Kusini mwa Afrika na Afrika kwa ujumla itatunzwa na kukumbukwa daima” amesisitiza Mhe. Dkt. Tax.

Pia ameziomba taasisi hizo kuwa chachu katika kueneza historia adhimu iliyomo kwenye chapisho hilo kwa kuhakikisha linasomwa. “Pamoja na kulitumia chapisho hili kama rejea, na kuhamasisha lisomwe, niwaombe wadau mbalimbali nchini kuona uwezekano wa kuandaa simulizi au filamu ya chapisho ili kuweza kuwafikia watu wengi hususan vijana” alisisitiza Mhe. Dkt. Tax.

Aidha, amefafanua kuwa, Chapisho hilo ambalo pamoja na mambo mengine linaeleza harakati za ukombozi katika nchi za Angola, Namibia, Afrika ya Kusini, Zimbabwe na Msumbiji na mchango wan chi za Tanzania, Zambia, Botswana, Lesotho, Malawi na Swaziland, lilipewa jina la Hashim Mbita kutoka na mchango thabiti na uongozi mahiri wa Hayati Brigedia Generali Hashim Mbita alioutoa akiwa Katibu Mtendaji wa Kamati ya Kupigania Uhuru Afrika kuanzia mwaka 1972 hadi 1994.

Mhe. Dkt. Tax pia ameshukuru na kupongeza mchango uliotolewa na Viongozi mbalimbali wa Tanzania akiwemo Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kamabarage Nyerere kwenye harakati za ukombozi kusini mwa Afrika kwani fikra na mtazamo wake kuhusu umuhimu wa uhuru kwa nchi za Afrika zilifanikisha nchi zote za Afrika kujikomboa dhidi ya ukoloni.

Pia Mhe. Dkt. Tax alitumia fursa hiyo kuipongeza Kampuni ya Kitanzania ya Uchapishaji ya Mkuki na Nyota kwa kuchapisha chapisho hilo kwa umahiri.

“Nawashukuru wadau wote waliofanikisha uchapishaji wa Chapisho la Hashim Mbita ikiwemo Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa kuandaa Chapisho hilo lenye Volume 9 na kwa kutambua mchango wa Tanzania katika harakati za Ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika. Pia kipekee namshukuru Rais Mstaafu wa wa Awamu ya Nne wa Tanzania, Hayati Benjamin William Mkapa kwa kuniagiza nikiwa Katibu Mtendaji wa SADC na kunisisitiza kuhakikisha chapisho hili linakamilika baada mchakato wa awali kusimama ambapo mwaka 2014 kufuatia maagizo hayo, mchakato ulitekelezwa katika awamu tatu na kukamilika mwaka 2020” alifafanua Dkt. Tax.

Awali akimkaribisha Mhe. Waziri, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo amesema kwamba, Wizara imepokea makasha 28 ya Chapisho la Hashim Mbita lenye Volume 9.

Pia aliongeza kusema Sektretarieti ya SADC inaendelea na mchakato wa kutafsiri Chapisho la Hashim Mbita kwa lugha ya Kiswahili ili kuwawezesha watanzania wengi zaidi kulisoma na kuijua historia ya nchi yao hususan mchango wa Tanznaia katika Harakati za Ukombozi Kusini mwa Afrika.

Hafa hiyo ilihudhuriwa na viongozi na wawakilishi kutoka Taasisi mbalimbali zikiwemo Ofisi ya Rais, Bunge, Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), Maktaba ya Taifa, Chuo Kikuu cha Dodoma na Taasisi ya Mwalimu Nyerere.



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi Machapisho Hashim Mbita kwa Taasisi mbalimbali za hapa nchini. Hafla hiyo ambayo ilizishirikisha Taasisi 18 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar ilifanyika jijini Dodoma hivi karibuni




Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi machapisho ya Hashim Mbita kwa Taasisi mbalimbali nchini. Katikati ni Mhe. Dkt. Tax na kulia ni Mhe. Vincent Mbogo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.



Sehemu ya wageni waalikwa walioshiriki hafla hiyo wakiwemo Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama



Sehemu nyingine ya washiriki




Wawakilishi wa Taasisi zilizoshiriki hafla ya kukabidhi machapisho ya Hashim Mbita wakifuatailia tukio. kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri



Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi machapisho ya Hashim Mbita kwa Taasisi mbalimbali.







Mhe. Dkt. Tax akimkabidhi Bw. Mbwana Msingwa kutoka Ofisi ya Rais Kasha lenye Volume 9 za Machapisho ya Hashim Mbita



Mhe. Dkt. Tax akiwakabidha Kasha lenye Volume 9 za Machapisho ya Hashim Mbita Wawakilishi kutoka Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakiwemo Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Mabo ya Nje, Ulinzi na Usalama wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Mbogo (kulia)



Makabidhiano yakiendelea kwa wawakilishi wa taasisi mbalimbali ikiwemo Maktaba ya Taifa.



Makabidhiano ya Machapisho ya Hashim Mbita yakiendelea


Mwakilishi kutoka Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) naye akikabidhiwa amachapisho ya Hashim Mbita



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...