Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

KATIBU Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi Zena Said amesema vikao vya Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) vimekuwa na ufanisi mkubwa kwa kutoa mapendekezo yenye kutatua migogoro na kuweka mazingira bara ya kufanya biashara na uwekezaji Tanzania.

“Napenda kuchukua nafasi ya kipekee kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Mwenyekiti wa TNBC kwa kulifanya baraza kuwa chombo cha utatuzi wa vikwazo na kero za kufanya biashara,” alisema.

Akizungumza pembezoni mwa ya Mkutano wa 14 wa TNBC kilichofanyika Jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Mhandisi Zena amesema mikutano ya Baraza inaongeza afya na kuimarika kwa ubia kati ya sekta za umma na binafsi (PPP)hapa nchini.

Alisema kupitia mikutano ya Baraza, wajumbe kutoka sekta za umma na binafsi wanapata nafasi ya kujadiliana kwa uwazi zaidi mambo yanayokwamisha biashara kusonga mbele na kupatiwa ufumbuzi wake.

“Tumejifunza mengi kutoka Mkutano wa 14 wa TNBC na hasa katika kushughulikia utatuzi wa migogoro na vikwazo vya kibiashara. Tutawaalika pia kwenye mkutano wetu utakaofanyika Zanzibar,” alisema Mhandisi Zena.

Naye, Mjumbe wa Baraza kutoka sekta bianfsi anayewakilisha sekta ya madini, Bw Peter Shayo mbali ya kumpongeza Rais Samia kwa kutambua mchango wa sekta ya madini alisema Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (MKUMBI) utasaidia kuimarika kwa sekta binafsi.

“Tumeshuhudia takribani ya miaka miwili chini uongozi wa awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan tumeona serikali ikitoa leseni kubwa za uchimbaji madini na makampuni makubwa,” alisema Bw Shayo.

Kuhusu suala la fedha za kigeni, Bw Shayo alisema Tanzania ina vyanzo vingi vya kujiingizia mapato kwa fedha za kigeni na hivyo kupitia mikutano ya Baraza wajumbe kutoka sekta za umma na binafsi kujadili mbinu mbalimbali za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Bi Rosemary Senyamule alisema ameweza kujifunza mbinu na namna bora ya kuongoza vikao vya mabaraza ya biashara sambamba na kuweka mazingira bora kufanya biashara.

“Dodoma tunajivunia kukua kwa sekta za biashara na uwekezaji. Sekta ya ujenzi inakua kwa kasi kubwa sambamba na ongezeko la watu,” alisema RC Rosemary na kupongeza mafanikio ya mkutano wa 14 wa TNBC.

Dhima ya Mkutano wa 14 wa Baraza ilikuwa “Mazingira Bora ya Biashara kwa Uchumi Himilivu na Shirikishi.

Naye, Kaimu Rais wa Chemba ya wenye Viwanda, Biashara na Kilimo (TCCIA), Bw Edmund Mkwawa alipongeza yaliyofikiwa kwenye mkutano kwani inatoa fursa kubwa ya kuendeleza viwanda hapa nchini.

“Tunahitaji kuongeza juhudi katika uzalishaji viwandani na kilimo ilituweze kupeleka bidhaa nyingi nje ya nchi,” alisema Bw Mkwawa.

TNBC kimekuwa ni chombo muhimu cha majadiliano kati ya sekta ya umma na binafsi katika kufikia maazimio ya pamoja (Consensus Resolutions) kuhusu masuala ya kuchochea biashara, uwekezaji kwa ajili ya kukuza uchumi na maendeleo ya kijamii kwa ajili ya mustakabali wa ustawi, maslahi mapana na maendeleo jumuishi ya Taifa letu.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...