MAMLAKA ya Masoko ya Mtaji na Dhamana (CMSA) imewaalika wananchi wote wanaotamani kujua kuhusu masoko ya mitaji na fursa zake kufika katika banda lao lililopo jengo la Wizara ya Fedha na Mipango kwenye Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) ili kupata elimu ya namna ya kutimiza malengo yao.
Imeelezwa kuwa mtu yoyote anayetamani kuwa mtendaji wa masoko ya mitaji katika eneo lolote akifika katika banda hilo atasikilizwa pamoja na kupatiwa ushauri kulingana na mpango wake wa kuomba leseni ya aina gani.
Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni katika maonesho hayo yanayoendelea kwenye viwanja vya sabasaba jijini Dar es Salaam, Afisa Uhusiano na Elimu kwa Umma kutoka katika mamlaka hiyo Stella Anastazi amesema, wamekuwa wakiendesha kozi fupi kila mwaka ili kuwaongezea ujuzi watendaji wa masoko.
"Mamlaka katika jitihada za kuhakikisha mtendaji wa soko anafanya kazi kwa weledi katika viwango vya kimataifa vinavyoleta tija kwa sekta ya masoko ya mitaji na nchi kwa ujumla ndio maana tynaendesha kozi hizo ambazo mpaka zimeishafanyika kadhaa kwa zaidi ya miaka mitano tangu kuanzishwa kwake" amesema Stella.
Ameongeza kuwa, mamlaka hiyo pia imefanikiwa kuanzisha masoko mawili ya mitaji ambayo ni Soko la Hisa la Dar es salaam (DSE), ambalo lilianzishwa mwaka 1998 na soko la Bidhaa Tanzania lililoanzishwa mwaka 2016.
Stella ameeleza kuwa pamoja na masoko hayo Mamlaka pia inatoa leseni kwa watendaji mbalimbali wa masoko mfano leseni ya Meneja Mfuko, leseni ya mshauri mwekezaji na leseni ya mtunza amana kwa ujumla na kuna leseni sita ambazo zinatolewa na mamlaka.
Taasisi yetu ni ya serikali iliyoanzishwa kwa sheria ya mitaji ya mwaka 1994 kifungu namba 79 ambapo sheria hiyo imetoa majukumu mbalimbali yakiwamo kuanzisha, kusimamia na kuendeleza masoko ya mitaji, kumlinda mwekezaji anayewekeza kwenye soko hilo pia kuishauri serikali katika masuala yanayohusu uwekezaji wa masoko ya mitaji.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...