Na Mwandishi Wetu

RAIS mstaafu Dk. Jakaya Kikwete kesho  Julai 14,  2023 anatarajiwa kuwaaga jumla ya washiriki 61 watakaopanda mlima Kilimanjaro kupitia kampeni ya ‘GGML KiliChallenge -2023’.

Kampeni hiyo  inalenga kukusanya fedha kwa ajili ya kutunisha Mfuko wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi (ATF) na kuendeleza mapambano ya kutokomeza Virusi Vya Ukimwi (VVU) na iliasisiwa mwaka 2002 na Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML kwa ushirikiano na Tume ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS).

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari  na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Tixon Nzunda amesema baada ya Dk. Kikwete kuwaaga washiriki hao katika lango la Machame kesho Julai 14, watapokewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu katika lango la Mweka Kibosho Julai 20 mwaka huu saa 3 asubuhi.

Akifafanua kuhusu kampeni hiyo, Makamu Rais wa AngloGold Ashanti- GGML anayeshughulikia miradi endelevu Ghana na Tanzania, Simon Shayo amesema mwaka huu jumla ya washiriki 35 watapanda mlima huo kwa njia ya kawaida ilihali washiriki 26 wataupanda mlima kwa kutumia baiskeli.

Amesema katika kampeni hiyo kutakuwa na utolewaji wa huduma bure za upimaji wa VVU, ushauri nasaha na kujitolea kutoa damu.

Mbali na kuishukuru Serikali kwa kuunga mkono kampeni hiyo iliyoasisiwa mwaka 2002, Shayo amesema  wakiwa wadau wa mapambano hayo ya UKIMWI na VVU, GGML imepokea msaada ambao uliiwezesha Kili Challenge kupiga hatua kubwa hadi kufikia kuwa mfuko wa kimataifa, wenye kushirikisha wapanda mlima na waendesha baiskeli kutoka mabara yote na zaidi ya nchi 20.

Fedha hizo ambazo hukusanywa kila mwaka, hulenga kuchangia juhudi za Serikali ya Tanzania katika jitihada zake kufikia malengo ya sifuri tatu yaani kupunguza kabisa kwa kufikia asilimia sifuri ya maambukizi mapya, sifuri ya unyanyapaa pamoja na sifuri katika vifo vitokanavyo na UKIMWI.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...