Na Munir Shemweta, WANMM NGARA

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewatahadharisha wananchi wanaosubiri kulipwa fidia kupisha mradi wa uchimbaji madini wa Tembo Nickel wilayani Ngara mkoa wa Kagera kujiepusha na mikopo umiza.

Dkt Mabula alisema hayo tarehe 23 Julai 2023 katika kijiji cha Bugarama wilayani Ngara mara baada ya kutembelea mradi wa uchimbaji madini ya Tembo Nickel kwa lengo la kupata taarifa ya maendeleo ya ulipaji fidia kwa wananchi wanaopitiwa na mradi huo akiwa katika ziara yake ya siku moja mkoani Kagera.

Alisema, anawasikitia wale wananchi wote walioingia katika mikopo umiza kwa kueleza kuwa watalazimika kulipa kiasi kikubwa cha fedha na hivyo kutoona faida ya fidia ya mali zao.

‘’Hela yako yote umeshaikopa unakwenda kulipa pesa nyingi kwa pesa ndogo uliyoichukua mwisho wa siku unarudi katika umasikini bila sababu, niwaombe msikimbilie kukopa pesa unayokwenda kulipa ni asilimia kubwa ya kile ulichochukua’’ alisema Dkt Mabula

Alisema, wanaowakopesha washajua muda mfupi ujao wananchi hao wanapata pesa hivyo wanajaribu kuwawahi watoe pesa leo lakini watakuja kulipa kiasi kikubwa cha fedha kuliko ilivyostahili jambo litakalowafanya kurejea kwenye umasikini.

Amewataka viongozi wa vijiji vyote vinavyopotiwa na mradi huo kutoa elimu ili wananchi wasije wakasikitika na kulia hapo baadaye kwa kuwa mara watakapopokea fedha za fidia basi waliowakopesha watakuja kudai fedha zao.

Aliwataka wananchi ambao hawajakopa kuacha kufanya hivyo kwa kuwa wanahitaji kuwa na maisha endelevu, kuwekeza ambapo alisema iwapo wanahitaji mikopo basi waende benki kwenye riba nafuu.

Awali Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alipata taarifa ya maendeleo ya ulipaji fidia wananchi wanaopisha mradi katika eneo la mradi.

Akiwa katika eneo hilo, Waziri Dkt Mabula alielezwa na kiongozi wa mahusiano ya jamii Bernard Sefu wa Kampuni ya Tembo Nickel kuwa, mgodi huo uko ndani ya kata tatu zenye vijiji vitano vinavyopisha mradi wa uchimbaji madini ya Nickel ambapo jumla ya wananchi 1,339 wanatarajiwa kulipwa fidia huku 349 kati ya hao wakijengewa nyumba kutokana na kuwa na makazi kwenye eneo la mradi huo.

Sefu alisema kuwa, mgodi huo umechukua hatua mbalimbali kwa kushirikisha viongozi, wataalamu na wananchi wanaopitiwa na mradi huo lengo likiwa kuhakikisha kila mwananchi anayehamishwa kupisha mradi anapata fidia stahiki kwa kufuata sheria za Tanzania na kanuni za kimataifa (IFC).

‘’Katika mchakato mzima wa kufanya ukokotovu wa malipo kwa wafidiwa, tuliwaonesha wahusika jedwali kabla ya kupeleka kwa mthamani mkuu wa serikali’’ alisema Sefu

Kwa upande wake, Waziri Dkt. Mabula mbali na kuipongeza kampuni ya Tembo Nickel kuandaa utaratibu mzuri wa kulipa fidia wananchi wanaopisha mradi pamoja na kusaidia huduma mbalimbali za jamii. Hata hivyo, aliitaka kampuni hiyo kuhakikisha wale wananchi wanaoenda kujengewa nyumba na kampuni hiyo wanawekewa mpango wa makazi utakaokuwa katika mpangilio wa kimji.

‘’Wale wananchi mtakaowajengea nyumba muangalie namna ya kuwapanga, tunahitaji upangaji wa kimji walau ufanane na mahali pale, mkiweza kuwasaidia mtawafanya wafanane kimji’’ alisema Dkt Mabula.

Kampuni ya Tembo Nickel Corporation Limited inatarajia kuchimba Madini ya Nickel katika eneo la Kabanga, Wilayani Ngara Mkoa wa Kagera ambapo zaidi ya hekta 4,000 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Januari 19 mwaka 2021 Serikali ya Tanzania na kampuni ya LIfezone Metals Nickel Limited zilisaini Mikataba uliowezesha kuanzishwa Kampuni ya Tembo Nickel Corporation Limited ambayo ni ya ubia kati yake na Serikali.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na wananchi wa Bugarama wilayani Ngara mkoa wa Kagera wakati wa ziara ya siku moja mkoani humo tarehe 23 Julai 2023. Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Ngara Kanali Mathias Kahabi.
Wananchi wa Bugarama wilayani Ngara mkoa wa Kagera wakimsikiliza Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alipofanya ziara wilayani humo tarehe 23 Julai 2023.Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (wa pili kushoto) na Mkuu wa wilaya ya Ngara Kanali Mathias Kahabi (wa kwanza kushoto) wakipata maelezo mara baada ya kuwasili katika mgodi wa uchimbaji madini ya Nickel wilayani Ngara mkoa wa Kagera tarehe 23 Julai 2023.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (kushoto) akizngumza na Mthamini Mkuu wa Serikali Evelyne Mugasha (katikati) alipowasili katika mgodi wa uchimbaji madini ya Nickel wilayani Ngara mkoa wa Kagera tarehe 23 Julai 2023.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza mara baada ya kupata taarifa ya maendeleo ya ulipaji fidia wananchi wanaopisha mradi wa uchimbaji madini ya Nickel wilayani Ngara mkoa wa Kagera tarehe 23 Julai 2023. Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Ngara Kanali Mathis Khabi.
Mthamini Mkuu wa Serikali Evelyne Mugasha (kulia) akifuatilia uwasilishwaji taarifa ya ulipaji fidia wananchi wanaopisha mradi wa uchimbaji madini ya Nickel wilayani Ngara mkoa wa Kagera wakati wa ziara ya Waziri wa Ardh Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula tarehe 23 Julai 2023.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (kushoto) na Mkuu wa wilaya ya Ngara Kanali Mathias Kahabi wakipata maelezo ya mradi wa uchimbaji madini ya Nickel wilayani Ngara mkoa wa Kagera tarehe 23 Julai 2023. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...