Na Damian Kunambi, Njombe.
Wananchi wa vijiji 20 vya kata ya Mlangali, Lupanga, Madope,Madilu, Lubonde pamoja na Lugarawa wameishukuru serikali kwa kuwaingiza katika mfumo wa umeme wa Wakala wa Umeme Vijijini(REA) na kuwapunguzia adha ya mgao mkali waliokuwa wakikabiliana nao hapo awali.
Wakitoa Shukrani hizo kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi wa vijiji hivyo mbele ya mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga mara baada ya kufanya ziara katika vijiji hivyo kwa lengo la kutoa mrejesho na kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi hao.
Wananchi hao ambao kwa takribani miaka 7 walikuwa wakitumia mradi wa umeme wa maji kwa ufadhili kutoka Duren Ujerumani uliokuwa chini ya usimamizi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Njombe (Madope Hydro Power) ambapo umeme huo ulikuwa ukizalishwa kiasi cha Mw 1.7 lakini uliokuwa ukitumika ni Mw. 0.3 na kupelekea wananchi kupata umeme huo kila baada ya siku tatu.
Miongoni mwa wananchi hao amesema umeme huo ulikuwa ukikwamisha shughuli nyingi za kimaendeleo ambapo ili kufanya shughuli zao ziweze kusonga iliwabidi kutumia umeme wa sola lakini kwa sasa baada ya kuunganishwa katika umeme wa gridi ya Taifa wanapata umeme huo kwa masaa 24.
Aidha kwa upande wake mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga amesema kutokana na changamoto hiyo kwa wananchi alifanya jitihada za kumuomba waziri wa Nishati January Makamba kufika katika eneo la mradi huo ambapo alifika na kisha kuwatuma wataalam ambao walitembelea vijiji vyote 20 na kubaini sababu ya tatizo hilo.
" Wataalamu hawa walibaini kuwa aliyetengeneza mitambo ya mradi huo ambaye ni mjerumani alikuwa anaidai pesa kiasi cha zaidi ya sh. Mil. 100 hivyo kutokana na hayo madai aliweka neno la siri( password) katika mitambo ili umeme usitoke kwa kiwango kilicho kamilifu hivyo hua ana udhibiti umeme huo kwa rimoti akiwa hukohuko ujerumani" Alisema Kamonga.
Amesema kwa sasa serikali ipo katika mchakato wa kuingia mkataba wa kuununua umeme unaozalishwa na kampuni hiyo na kuuingiza TANESCO ili uweze kuendelea kuhudumia wananchi hao kikamilifu.
Mbunge huyo anaendelea na ziara hiyo aliyoianza mnamo Julai 7 mwaka huu akiwa na lengo la kuvifikia vijiji vyote 77 vya jimbo hilo ambapo mpaka sasa tayari amekwisha tembelea vijiji 15 kati ya 77 ambavyo ni Madilu, Ilawa, Ilininda, Manga, Mfalasi, Iwela, Madope, Mangalanyene, Luvuyo, Masimbwe, Mkiu, Kiyombo, Lupanga, Utilili, Lusala, Ligumbilo na Lufumbu
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...