Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MWENYEKITI
wa CCM Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Kiria Ormemei Laizer
amewapongeza walimu wa shule ya sekondari Naisinyai kwa kuwapatia zawadi
ya kitita cha shilingi milioni 2 baada ya wanafunzi 33 wa kidato cha
sita wa shule hiyo kufaulu mtihani wao na kuchaguliwa kujiunga na vyuo
vikuu.
Pia, Diwani wa
Kata ya Mirerani, Salome Nelson Mnyawi, pia amewakabidhi walimu wa shule
hiyo sh300,000 ili kumuunga mkono Kiria katika kuwapongeza walimu hao.
Kiria
amesema amejitolea Sh2 milioni kwa walimu hao ili wakanywe soda za
pongezi kutokana na ufaulu mzuri wa wanafunzi wa kidato cha sita wa
shule hiyo.
"Najua shule
ya sekondari Naisinyai imefaulisha vyema wanafunzi wa kidato cha sita,
hivyo fedha hizo zitachangia furaha yangu kwa walimu kutokana na ufaulu
huo mzuri," amesema Kiria
Mkuu
wa shule ya sekondari Naisinyai, William Ombay amesema wanafunzi 33 wa
shule hiyo walifanya mtihani wa kuhitimu kidato cha sita na wote
wamefaulu kwenda chuo kikuu.
"Kati
ya wanafunzi hao 33, watatu wamepata daraja la kwanza, 27 daraja la
pili na watatu daraja la tatu, hivyo hakuna mwanafunzi aliyepata daraja
la nne wala sifuri," amesema mwalimu Ombay.
Diwani
wa kata ya Naisinyai, Taiko Kurian Laizer amewapongeza walimu hao kwani
wanafunzi wasingefaulu ingekuwa lawama kwao ila hivi sasa pongezi ni za
watu wote.
"Kwenye
kufanya vizuri tunakuwa tunapata sifa wote pamoja ndiyo sababu hata mimi
nimepongezwa kwenye magurupu ya Whatsapp ila wanafunzi wangefeli
ingekuwa aibu yenu walimu," amesema Taiko.
Diwani
wa kata ya Mirerani, Salome Mnyawi amemuunga mkono Mwenyekiti wa CCM wa
Wilaya kwa kuwapongeza walimu hao kwa kuwapatia Sh300,000 kwa
kufanikisha ufaulu huo.
"Hii
natoa changamoto kwa walimu wa shule yangu ya sekondari Tanzanite
iliyopo kata ya Mirerani kuhakikisha wanaendelea kufundisha vyema ili
wanafunzi wafaulu nao tuwazawadie," amesema Salome.
Katibu
mwenezi wa CCM Wilaya ya Simanjiro, Mosses Makeseni amesema wanafunzi
hao wamefaulu vyema, ingawa ndiyo mara ya kwanza wanafunzi wa Naisinyai
kufanya mtihani wa kidato cha sita.
Mwenyekiti
wa kijiji cha Naisinyai, Merika Makeseni amesema walimu wanastahili
kupongezwa kutokana na matokeo hayo kwani wao ndiyo wanaowafundisha
wanafunzi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...