Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) Ndugu Kiula Kingu amefanya ziara katika Kata za Kwembe, King'azi na Msigani ili kuanza utekelezaji wa mpango maalumu wa kuboresha huduma za majisafi katika maeneo hayo ikiwa ni agizo la Waziri wa Maji, Mheshimiwa Jumaa Aweso kuhakikisha huduma ya maji katika maeneo hayo inaboreshwa.
Mpango huo una lengo la kutekeleza miradi miwili inayolenga kutatua changamoto iliyopo ya msukumo mdogo wa maji na ukosefu wa huduma kwa baadhi ya maeneo.
Awamu ya kwanza itahusisha ulazaji wa bomba kutoka eneo la Kwembe maduka tisa hadi jirani na Shule ya sekondari ya Barbara Johanson. Mradi huu utakaoanza Jumatatu ijayo (10 /7/2023) utahusisha ulazaji wa bomba la inchi 12 kwa umbali wa mita 200 ambapo kukamilika kwa kazi hii kutanufaisha wakazi wa maeneo ya Kwembe, King'azi B, Kwembe Mpakani, Kwa Bush na Mzalendo. Mradi utakamilika baada ya wiki mbili.
Na awamu ya pili ya mradi itahusisha kazi ya ulazaji wa bomba za inchi 8 kwa umbali mita 3,200. Mradi huu ukikamilika utanufaisha wakazi wa Njeteni, Mlimani City, King'azi B, Mzalendo, Kwembe Mpakani, Mama Poa, Maduka tisa, Mitiki, Kwembe Kijijini, Tawalani na Mwangosi. Mradi huu utaanza hivi karibuni.
Ndugu Kingu amesema Mamlaka tayari ina mabomba na vifaa muhimu vya utekelezaji wa awamu ya pili inatarajiwa kuanza mwisho wa Mwezi Julai baada ya kukamilisha upatikanaji wa vifaa muhimu vya utekelezaji wa mradi huo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...