Na. Damian Kunambi, Njombe.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Ludewa Wise Mgina ambaye pia ni diwani wa kata ya Mundindi ambako ndiko kwenye mradi wa chuma cha Liganga, ameishukuru serikali kwa kuwalipa fidia wanachi wanaozunguka mradi huo huku akiiomba serikali kujenga viwanda vya kuchakata chuma katika kata ya hiyo ya Mundidi.

Mwenyekiti huyo amewasilisha ombi hilo mbele ya mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga mara baada ya kuwasili katika kata hiyo na kufanya mikutano ya hadhara katika vijiji vitatu ambavyo ni Amani, Njelela na Mundimdi.

Wise amesema wananchi wa kata hiyo wamekuwa wakikilinda chuma hicho kwa miaka mingi hivyo ni vyema wakawa wanufaika wakwanza kwani viwanda hivyo vitakapojengwa vitawasaidia katika kufanya biashara mbalimbali kwakuwa kutakuwa na mwingiliano mkubwa wa watu sambamba na vijana kupata ajira katika viwanda hivyo.

" Mheshimiwa mbunge, tunaomba utufikishie salamu hizi kwa Rais wetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan mwambie tunashukuru sana kwa kutulipa fidia, lakini wanufaika wa fidia hizi si wote ni wachache tu! Hivyo kuna wengine ambao wanahitaji kunufaika na mradi huu kwa kutumia fursa mbalimbali zitakazotokana na viwanda vitakavyo anzishwa". Amesema Diwani Wise.

Aidha ombi hilo linaungwa mkono na wananchi wa kata hiyo akiwemo Donesia Luoga ambaye amesema kuwa tayari serikali imewajengea chuo cha ufundi stadi (VETA) kilichopo katika kijiji cha Shaurimoyo kata ya Lugarawa ambacho kinatarajiwa kuanza kutoa mafunzo mapema mwaka ujao hivyo vijana watakao hitimu chuoni hapo viwanda hivyo vitawasaidia kupata ajira kwa urahisi.

" Sisi wananchi tumesha jipanga kwa kila kitu kwani tumetenga maeneo tayari ya kujengwa kiwanda hicho, barabara nayo ipo hivyo tunaomba viwanda vijengwe huku nasi tunufaike na mradi huu", amesema Bi. Luoga.

Naye mbunge wa jimbo hilo Joseph Kamonga amesema hoja hiyo ni ya msingi hivyo ameipokea na atahakikisha anaifikisha bungeni kwani wilaya hiyo imejaaliwa madini ya chuma pamoja na makaa ya mawe ya kuyeyushia chuma hicho.


"Nitaenda kulisemea hili bungeni na ninatumai Rais wetu mama Dkt. Samia Suluhu Hassan atasikia kilio hiki cha wana Ludewa kwani chuma hiki hakiko peke yake bali ndani yake kuna madini aina tatu yenye thamani zaidi kuliko hata hicho chuma hivyo kutakuwa na ajira mbalimbali ikiwemo kutenganisha chuma na madini na ni vyema wananchi wakanufaika na fursa za ajira zitakazo jitokeza", Amesema Kamonga.

Mbunge huyo anafanya ziara vijijini kwa lengo la kutoa mrejesho wa aliyo agizwa sambamba na kupokea changamoto za wananchi ambapo mpaka sasa tayari amekwisha tembelea vijiji 22 kati ya 77 vya jimbo hilo na anaendelea na ziara hiyo ili kuvifikia vijiji vyote 77.







 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...