Na Rahma Khamis Maelezo

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amewataka Mawaziri wa Wizara husika za Serikali zote mbili zinazoshuhulikia ajira kuandaa mikakati ya kutengeneza nafasi za ajira za kusomesha lugha ya Kiswahili nje ya nchi.

Ameyasema hayo katika Ukumbi wa Ziwani Polisi wakati akifungua maadhimisho ya siku ya Kiaswahili Duniani ikiwa ni shamrashamra za kuelekea siku hiyo.

Waziri Majaliwa amesema katika kuhakikisha kuwa kiswahili kinawanufaisha Watanzania ipo haja ya kuweka mikakati iliyo wazi na kushajihisha wanafunzi wanaofanya vizuri katika masomo yao ya kiswahili.

Amesema kuwa Serikali zote mbili kwa kushirikiana na Taasisi mbali mbali pamoja na Shirika la Elimu na Sayansi na Utamaduni (UNESCO) watahakikisha kufanya kazi kwa pamoja ili kutanua kiswahili hadi kufika mipaka ya Tanzania na kutengeneza fursa ya ajira ikiwemo kusomesha na kutangaza nje ya nchi.

"Ni lazima tukienzi kiswahili chetu na kwa wale tunaofanya utafiti wa kiswahili katika Vyuo Vikuu tuendelee kuitumia lugha hiyo ili tuweze kwenda mbali zaidi,"alifahamisha Waziri Mkuu.

Majaliwa amewataka wadau mbali mbali wa lugha ya Kiswahili kufanya juhudi za kuhakikisha kuwa lugha hiyo inapiga hatua zaidi na kuendelea na kuimarika mikononi mwa Watanzania.


“Ni dhahiri kuona maarifa ya wataalamu wa kiswahili yatawasadia wanafunzi kuweza kutambua lugha yao ya kitaifa kwani kiswahili ni lugha inayozungumzwa mpaka duniani na kuwataka kutoacha kujifunza na lugha nyengine ili kupata fursa zaidi duniani”, amefahamisha.

Aidha ameeleza kuwa mada zilizotewa katika mashindano ya insha ni muhimu sana kwani zinakwenda sambamba mazingira yaliopo nchini katika uandishi hivyo wanafunzi wataweza kutumia lugha ya Kiswahili sanifu ili kutatua changamoto zinazowakabili.

"Leo hii nchi za Umoja wa Afrika zinatumia lugha ya Kiswahili hivyo tunazidiwa na wenzetu wa nje kwa kukitumia zaidi hebu na sisi tuitumie nafasi yetu ili tuweze kupata ajira zaidi", alisema Waziri Mkuu.

Aidha Waziri majaliwa amewapongeza washindi waliopata zawadi na kusisitiza kuwa mashindano hayo yawe endelevu ili kuwashajihisha wanafunzi katika kuwajengea uwezo kushirika mashindano ya kimataifa.

"Tunapoweka mikakati ya kuongeza juhudi za kusomesha Kiswahili tunatarajia kufika mbali zaidi basi na tujitahidi ili tufikie malengo”, alisisitiza Waziri Majaliwa.


Nae Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Tabia Maulid Mwita amefahamisha kuwa kuna mafanikio makubwa yamepatikana kwani kiswahili kimekuwa ni bidhaa duniani na kuna walimu wanasomesha lugha hiyo ndani na nje ya nchi.

Aidha Waziri Tabia amesema kuwa wanaendelea kusimamaia sheria na kanuni za Mabaraza ya Kiswahili ili kiweze kufika mbali na kupaa duniani kote.

Kwa upande wao Katibu Mkuu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Zanzibar

(BAKIZA) Dkt Mwanahija Ali Juma na Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) Consolata Pita Mushi wakitoa ufafanuzi kuhusu mashindano ya uwandishi wa Insha waliyoyaandaa kwa wanafunzi wamesema kuwa lengo la mashindano hayo ni kuwajengea uwezo wanafunzi kuweza kutumia lugha kwa ufasaha.

Wamesema kuwa katika mashindano hayo wameona makosa mengi katika uwandishi wao na kufafanua kuwa wanafunzi wengi hawakuzingatia vigezo na matumizi ya uandishi wa lugha ya kiswahili ikiwemo kiswahili sanifu na fasaha ambapo asilimia 60 hawakuzingatia matumizi ya vituo na tahajia ,hivyo Kamati imependekeza mashindano hayo yafanyike mara kwa mara ili kuwepo na Vijana wenye uwezo katika lugha hiyo.

Aidha wamefahamisha kuwa Mabaraza yote mawili yamedhamiria kuendesha semina na mafunzo mbalimbali kwa wanafunzi Unguja na Pemba ili kuwa na waandishi wazuri wa baadae.

Hata hivyo Makatibu hao wamefafanua kwamba katika mashindano ya uandishi huo mada tatu zimetolewa ikiwemo dhalilishaji wa Jinsia, Uchumi wa Buluu na Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani ambapo katika mashindano hayo Skuli ya Mtopepo kutoka Mjini Magharib na Skuli kutoka Mkoa wa Manyara wamepata nafasi ya kwanza.

Kilele cha maadhimisho hayo kinatarajiwa kufanyika kesho katika Ukumbi wa Ziwani Polisi ambapo Kaulimbiu ya mwaka huu Kiswahili chetu ni Umoja wetu.



Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na viongozi na wananchi waliojitokeza katika Hafla ya Ufunguzi wa Siku ya Kiswahili duniani, Iliyofanyika katika Ukumbi wa Polisi visiwani Zanzibar. Julai 06, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...