Na Said Mwishehe,Michuzi TV
JUMLA ya Sh.bilioni 85 zimetolewa kama gawio na Kampuni ya Tanzania Breweries Public Limited(TBL) kwa wanahisa wake ambapo thamani ya hisa moja ni Sh.290.
Akizungumza leo Julai 19 jijini Dar es Salaam kwenye Mkutano Mkuu wa 50 wa Wanahisa wa TBL, Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi wa kampuni hiyo Leonard Mususa amesema kutokana na faida waliyoipata gawio kwa wanahisa limeongezeka kutoka Sh.255 kwa hisa moja hadi Sh.290 kwa hisa moja.
“Tunalipa zaidi kutokana na faida tunayoipata , kampuni yetu tumetoka kupata faida ya Sh.bilioni 134.7 mpaka Sh.bilioni 153.4 na ndio maana tumeweza kulipa kiasi hicho cha Sh.290 kwa wanahisa wetu.Mwaka 2022 kidunia ulikuwa na changamoto nyingi tumeona vita kati ya Urusi na Ukraine.
“Misukosuko na kutoelewa kwa mataifa mbalimbali , mfumo wa bei duniani kote umekuwa mkubwa, hapa kwetu nafuu kidogo , riba ziko juu, hizo changamoto zote tunaziona hata sisi.
“Ukiangalia katika utendaji gharama zetu utakuta ziko juu kutokana na usafirishaji wa bia lakini ukiangalia ripoti yetu ya mwaka ya utendaji, ukiangalia mauzo yetu mauzo yameongezeka kwa asilimia 12,”amesema.
Ameongeza pamoja na changamoto hizo hali ya utendaji ya TBL iko vizuri, mauzo yameongezeka , faida imeongezeka zaidi na hiyo inatokana na udhibiti wa gharama kwenye utendaji, wanafanya kazi kwa tija zaidi lakini bado wameongeza faida na hiyo imesababisha wanahisa kulipwa gawio lenye ongezeko la asilimia 14.
Kupitia mkutano Mkuu wa mwaka wa wanahisa wa TBL, Mususa ameeleza kampuni hiyo inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha wanaendelea kuwa imara katika soko la vinywaji kwa kufanya ubunifu kweny utengenezaji wa vinywaji vyao pendwa hapa nchini.
“Tunaendelea kuwa wabunifu kwa kuleta vinywaji kwa ajili ya wanywaji wetu wote, kuna vijana na wazee na wote wanapenda vinywaji tofati, hivyo kwa ujumla tunaangalia jamii inapenda nini kwa kufanya tafiti kwenye soko.”
Pamoja na hayo amezungumzia mkakati wa TBL wa kuanzisha kiwanda cha kuchakata Shairi ambacho kinajengwa Moshi mkoani Kilimanjaro na matarajio yao Machi mwakani kitaanza uchakataji wa shairi.
“Unaweza kwani inakuaje kiwanda cha kuchakata shairi? Iko hivi unapotengeneza pombe unahitaji kimea hivyo tunachosema tutakuwa tunatengeneza kimea ambacho kitatumika kutengeneza bia hapa nchini.
“Hivi sasa tunatumia shairi tani 5000 lakini kiwanda kikianza uzalishaji tutafika tani 12000 na katika kipindi cha miaka mitano ijayo tutakuwa tumefika uzalishaji wa shari tani 3200 na zote hizo itabidi zipatikane.
“Hivyo tutaongeza uzalishaji kwa wakulima, kwa sasa shairi inapatikana Arusha ,Manyara na West Kilimanjaro lakini tunatarajia pia ianze kulimwa katika mikoa ya nyanda za juu Kusini ambako nako hali yake inaruhusu.”
Ameongeza wanategemea huko mbeleni wasiagize shairi kutoka nje ya Tanzania , bali iwe inapatikana nchini hivyo ombi lao ni kwa Serikali kuendelea kutoa ushirikiano na kuboresha mazingira ya uwekezaji.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TBL Jose Moran amehakikishia wanahisa wote kuwa kampuni hiyo iko makini katika kuhakikisha wanaendelea kutengenezwa vinywaji vinavyopendwa huku akifafanua anatambua kuwa Konyagi ni kichwaji kinachopendwa ndani na nje ya Tanzania.
Aidha amesema katika kuendelea kuliteka soko la vinywaji wameendelea kufanya tafiti kuangalia jamii inapenda nini na kwa kutambua hilo wameendelea kutoa vinywaji kulingana na makundi mbalimbali.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya TBL Jose Moran (katikati) akizungumza wakati wa mkutano wa Wanahisa wa kampuni hiyo.Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi Leonard Mususa na kulia ni Mkurugenzi wa kampuni hiyo Focus Laswai
Baadhi ya wanahisa wa Kampuni ya TBL wakifuatilia taarifa kuhusu masuala mbalimbali ya kampuni hiyo walipokuwa wakifanya marejeo ya mkutano mkuu uliopita
Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya TBL Leonard Mususa( katikati) akizumgumza na wanahisa wakati wa Mkutano Mkuu wa 50 wa mwaka uliofanyika leo Julai 19, 2023 jijini Dar es Salaam
Wajumbe wa bodi ya Kampuni ya TBL waliokaa wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wanahisa baada ya kukamilika kwa Mkutano Mkuu wa 50 wa mwaka uliofanyika leo Julai 19 jijini Dar es Salaam
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...