Na Grace Semfuko, MAELEZO.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye amewataka waimbaji wa nyimbo za Injili kumsifu Mungu na kuliombea Taifa amani na maendeleo.

Ameyasema hayo leo Julai 23 wakati akizindua Tamasha la Mkatoliki lililoandaliwa na kwaya ya Mtakatifu Cecilia ya Parokia ya Mwenyeheri Anuarite Makuburi Jijini Dar es Salaam ambapo pia amezindua na albamu ya 17 yenye nyimbo saba.

Mhe. Nape amesema amani iliyopo nchini Tanzania ni ya mfano wa kuigwa na mataifa mengine hivyo ni muhimu kuendelea kuilinda na kuwasihi Waimbaji kuzidi kuliombea Taifa katika amani iliyopo.

“Tumsifu Mungu wetu lakini apia tuiombee nchi yetu iendelee kuwa na amani, katika kutembea kwangu kwenye baadhi ya nchi nimekutana na nchi ambazo watu wanakaa kwenye vikao vya harusi mezani wameweka bunduki ili kujilinda, sisi Tanzania tuna kila sababu ya kujivunia amani yetu, kwa hiyo kuna kila haja ya kumshukuru mungu” amesema Mhe. Nape.

Amesema ipo haja kwa viongozi wa siasa kuunga mkono juhudi za watu wanaomkumbuka Mwenyezi Mungu kwani wao ndio chanzo kikubwa cha amani kutokana na kuliombea Taif ana watu wake.

”Ukiona watu wanamkumbuka Mungu hao ni wakuungwa mkono, sisi wanasiasa unaweza kuwa na majeshi yote ya kukulinda, lakini Mwenyezi Mungu akisema anyooshe mkono wake, hayo majeshi yabaki kuulinda mwili” amesema Mhe. Nape.

Aidha Waziri Nape amekubali ombi la Mwenyekiti Msaidizi na Mwalimu Kiongozi wa Kwaya ya Mtakatifu Cecilia Bw. Barnabas Majige la kuwa Mlezi wa Tamasha kubwa la kwanza la Mkatoliki linalotarajia kufanyika Mwezi Desemba mwaka huu.

”Mmeomba niwe Mgeni rasmi kwenye hilo tamasha naomba niwatafutie Mgeni rasmi ambaye yupo juu yangu, na niwaahidi nitamleta Makamu wa Rais awe mgeni rasmi, kazi ya kumleta niachieni mimi” amesema Mhe. Nape




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...