Taasisi ya Kimataifa ya Heifer imeendelea kuunga mkono jitihada za Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha vitendea kazi vijana wanaofanya shughuli za unenepeshaji wa mifugo katika kituo cha Mabuki kilichopo Wilayani Misungwi, Mkoani Mwanza.
Akiongea na vijana katika hafla fupi ya kupokea vitendea kazi hivyo ikiwemo Lori moja na pikipiki Nne, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega aliwashukuru Wadau hao wa Heifer huku akisema kitendo hicho ni uungaji mkono jitihada za Mhe Rais Samia za kuwawezesha vijana na kina mama kujiajiri na kukuza kipato chao kupitia programu ya BBT Mifugo na Uvuvi.
Alisema kuwa Dkt. Samia anataka kuifanya programu hiyo ya BBT kuwa ya kielelezo ambapo vijana wengi waweze kujikomboa kwa kujiajiri kupitia shughuli za Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Aliongeza kwa kusema kuwa ni wakati sasa kwa vijana hao kuanza kufanya ubunifu wa kufanya biashara yao hiyo kidigitali kupitia mifumo ya biashara mtandao ili kupunguza kutegemea kuuza mifugo yao kupitia masoko ya kawaida.
Aidha, aliwataka vijana hao wanaopata mafunzo ya unenepeshaji wa mifugo katika kituo hicho cha mabuki kuwa mstari wa mbele katika kufanya mapinduzi ya uchumi kupitia ufugaji wa kisasa ili vijana wenzao wengine waweze kuona na kuamini kwamba inawezekana.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkaazi,
Heifer International Tanzania, Mark Tsoxo alisema wataendelea kufanya kazi na Serikali hasusan katika programu zinazohusu vijana ili kuunga mkono uwezeshaji wa vijana na kina mama kupitia programu ya BBT.
"Hivi sasa tuna mpango wa kufikia vijana laki moja kupitia programu ya kopa ng'ombe lipa ng'ombe ambayo tunaamini itawezesha vijana wengi kujiajiri", alisema tsoso
Aliongeza kwa kusema kuwa wametoa vitendea kazi hivyo kufuatia ombi la Waziri Ulega ambapo aliwaomba kuona namna ya kuunga mkono programu hiyo ya kielelezo ya Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akisoma risala ya vijana hao wa mabuki waliokabidhiwa vitendea kazi hivyo, Joyce Lemanda alisema kuwa wanamshukuru Rais Samia kwa kuwapa fursa hiyo ya kufanya ufugaji wa kisasa huku wakitoa ahadi kuwa wataendelea kufanya vizuri kwa lengo la kuunga mkono jitihada hizo za Mhe. Rais na kwamba hawatamuangusha.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...