Na Mbaraka Kambona, Kilombero.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amewataka Wavuvi Wilayani Kilombero kujiepusha na matumizi ya zana haramu kama vile nyavu za nailoni na makokolo kwani ni hatari kwa maendeleo ya uvuvi.

Mhe. Ulega aliyasema hayo wakati akiongea na Wavuvi wa Kivukoni, Ifakara alipofanya ziara Wilayani Kilombero, Mkoa wa Morogoro Julai 5, 2023.

Alisema matumizi ya zana haramu yamekuwa ni chanzo cha uharibifu wa mazalia ya samaki na kupelekea rasilimali hiyo kupungua na kama matumizi hayo yakiendelea yatapelekea athari kubwa kwa sekta ya uvuvi nchini.

Aidha, aliielekeza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) kushirikiana na Serikali za vijiji Wilayani humo katika kuelimisha Wavuvi na Wananchi kwa ujumla juu ya umuhimu wa uvuvi endelevu ikiwemo ulinzi wa mazalia ya samaki.

Halikadhalika, Mhe. Ulega aliwaeleza wavuvi hao pia kuwa na shughuli mbadala ili kujiongezea kipato ikiwemo kufanya ufugaji wa samaki katika Mto Kilombero.

Aliongeza kuwa Wizara yake itaendelea kushirikiana na wavuvi ikiwemo kuwawezesha zana na utaalam mbalimbali ili shughuli zao ziweze kuwa na tija zaidi.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Malima wakiangalia  samaki waliovuliwa na mmoja wa wavuvi katika Mto Kilombero muda mfupi baada ya kuongea na Wavuvi wa Kivukoni, Ifakara alipofanya ziara Wilayani Kilombero, Mkoa wa Morogoro Julai 5, 2023.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...