Na Janeth Raphael - MichuziTv - Dodoma.
Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salamu (DAWASA) imejipanga kuendelea na kuboresha upatikanaji wa huduma ya majisafi kupitia utekelezaji wa miradi ya kimkakati saba ikiwemo mradi wa ujenzi wa bwawa la Kidunda, mradi wa ujenzi wa mtambo wa kuzalisha maji wa Rufiji na mradi wa maji Kwala.
Mikakati hiyo imeelezwa na Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka Hiyo Kiula Kingu wakati akizungumza na waandishi wa Habari leo Jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa Majukumu kwa Mwaka wa Fedha 2023/24 na kusema Miradi hiyo itakayotekelezwa kwa jumla ya shilingi bilioni 425.9 inalenga katika kuongeza wingi wa maji yanayozalishwa na DAWASA, kuongeza uwezo wa kuhifadhi maji, kuimarisha mfumo wa usambazaji maji na kuimarisha huduma katika maeneo ambayo hayana mtandao hasa yale ya pembezoni.
Aidha, Kingu amebainisha miradi hiyo itasaidia wananchi kupata huduma za usafi wa mazingira kwa gharama nafuu karibu na maeneo wanayoishi na Wakandarasi wanaotekeleza miradi wanaendelea na ujenzi Gharama za miradi hii ni jumla ya shilingi bilioni 25.7 na wanufaika wa miradi hii wanakadiriwa kufikia milioni 1.8.
Hata hivyo katika hatua nyingine amesema Mradi mwingine unaotekelezwa ni wa kujenga mfumo wa kukusanya majitaka na maeneo nufaika ambapo katika awamu hii ni Mbezi beach, Kilongamwima, baadhi ya maeneo ya Kawe na Salasala. Utekelezaji wa mradi umeanza na Wakandarasi wanaendelea na shughuli za maandalizi ya ujenzi.
Miradi hiyo ni ya kisasa na katika mfumo wake wa uchakataji majitaka itatoa gesi asilia kwa ajili ya kupikia, itatoa mbolea itakayoweza kutumika katika kustawisha bustani za miti na majani pia maji yatakayochakatwa yataweza kutumika kwa ajili ya shughuli za umwagiliaji, usafishaji wa barabara na mitaro ama kupoozea mitambo.
Kaimu Afisa Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira ( DAWASA) Kiula Kingu akizungumzia na wanahabari (hawapo pichani) wakati akieleza utekelezaji na vipaumbele vya majukumu ya DAWASA kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Leo Jijini Dodoma.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...