Na Karama Kenyunko Michuzi TV
Shahidi wa 22 katika kesi ya Mauaji inayowakabili aliyekuwa mke wa Bilionea Erasto Msuya, Miriam Mrita na mwenzake ameieleza mahakama kuwa, aliyekuwa msichana wakazi wa Anenth Msuya alimwambia kuwa mke wa aliyekuwa bilionea Msuya, alimuahidi kumpatia sh. milioni 50 ili aondoke nyumbani kwa bosi wake lakini mwisho aliambuliwa kupewa sh. elfu 20.
Shahidi huyo, ambaye ni Mkuu wa Upelelezi wa makosa ya jinai mkoani Arusha, Mrakibu Mwandamizi wa polisi ((SSP) David Mhanaya ameeleza hayo leo Agosti 28, 2023 wakati akitoa ushahidi wake mbele ya Jaji Edwin Kakolaki wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Washtakiwa katika kesi hiyo namba 103 ya mwaka 2018 ni wifi wa marehemu, Aneth, mjane wa Bilionea Msuya; Miriam Mrita na mfanyabiashara Revocatus Muyella.
Aneth alifariki dunia Kwa kuchinjwa shingoni ĺMei 25, 2016, usiku nyumbani kwake, Kibada Kigamboni, wilayani Temeke (wakati huo).
Akiongozwa na wakili wa serikali Mwandamizi Paul Kimweri kutoa ushaidi wake, Mhanaya amedai kuwa, Julia 12,2023 akiwa na ASP Jumanne wakati huo na yeye akiwa ASP aliitwa kwa Mkurugenzi wa upelezi wa makosa ya jinai, Kamishna Diwani Athumani.
Anadai kuwa na Diwani aliwataka kwenda kuongeza nguvu katika kufanya upelelezi wa kesi ya mauaji ya Aneth Msuya iliyokuwa ikipelelezwa kwa RCO Temeke.
"Mkurugenzi hakupendezwa na upelelezi ulivyokuwa unaendelea hivyo akatutaka tukaongeze nguvu kule"
Mhanaya akadai kuwa, DCI aliwaelekeza wakaripoti kwa Mkuu wa Polisi Temeke SSP Mchomvu ambaye aliwapa melekezo kwa kifupi juu ya tukio hilo na jinsi linavyoshughulikiwa kisha akawakabidhi jalada la kesi na kutuongezea nguvu ya wapelelezi wengine.
Anadai kuwa waliweka mikakati ya kazi ambapo kwa kuanzia walienda eneo la tukio huko Kibada nyumbani kwa marehemu Aneth Msuya na kwamba waliangalia muonekano wa nyumba ambayo ilikuwa imezungushiwa ukuta na mlango mmoja tu wa kuingilia
"Mlango wa kuingi sebuleni ulionekana umevunjwa ndipo baada ya kuangalia, tulitoka na kupata maelekezo ya mashahidi wanaozunguka eneo la tukio".
Anadai walielezwa kuwa marehemu alikuwa anafanya kazi wizara ya fedha na alikuwa akiishi mtoto wake Allen (4) na binti wa kazi aliyetajwa kwa jina la Getruda Mfuru ambaye alitoweka siku moja kabla ya tukio.
Akadai kuwa baada ya kupata taarifa hizo yeye na timu yake waliona kazi ndio imeanza hivyo wameanza na kumtafuta binti huyo wa kazi kwa kutumia vyombo vyote.
"Baada ya siku chache jitihada zetu zilifanikiwa kwani Julia 27,2016 nikiwa ofisini Temeke, niliitwa na afande Mchomvu akasema binti wa kazi amepatikana, nikaagiza aletwe ambapo Ditektivu koplo Easter alemleta na tutakaa nae kwa mahojiano ambayo yalichukua saa moja na nusu.
Kabla ya mahojiano Getruda huyo wa kazi alionekana mwenye wasi wasi mkubwa mbele yangu akamuomba kama anaweza kumlinda ndipo akamtoa mashaka na kumtaka amueleze yaliyojiri katika tukio hilo mwanzo mpaka mwisho hadi kumpelekea yeye kutoroka.
Mhanaya anadai Getruda alimueleza kuwa Mei 15, 2016 akiwa anaelekea dukani bila kutarajia akakutana na gari aina ya pickup Ford Range rangi ya Dark bluu, ambapo ile gari ilisimama miguuni kwake na kioo kilipofunguliwa akamuona mama mmoja mweupe mnene mwenye sura ya mviringo huku pembeni yake kukiwa na mwanaume mweusi mnene kiasi aliyekuwa akiendesha gari ambaye alikuwa na kipara kidogo huku akiwa ameweka miwani juu ya kichwa.
Akaendelea kueleza kuwa Getruda alimwambia yule mama alimuuliza hujambo, naomba kukuuliza hivi kwa Aneth Msuya ni sehemu gani? anadai binti kwa ishara akamuonesha nyumba kisha akamwambia yeye ndio anaishi nae pale, akamuuliza sasa hivi yupo akamwambia bado hajarudi kutoka kazini.
Akadai Getruda alimwambia kuwa yule mama alimwambia 'Kuna kazi nataka kufanya na wewe lakini hakumwambia ni kazi gani ila alimwambia nitakuja kesho ila naomba uwe msiri usimwambie mtu ' anadai alimwambia aliporudi aliogopa hata kumwambia dada yake.
Anadai Gertrude alimwambia siku iliyofuata akiwa anatoka kuchota maji na amekaribia kuingia ndani aliwaona watu wale safari hii wakiwa wameshuka kwenye gari, mwanamke alikuwa mnene na miguu mwembamba kwani alikuwa amevaa kimini huku mwanaume akiwa amevaa suti nyeusi na viatu vyeupe huku mkononi alishika briefcase.
Anadai aliwafuata hadi pale na wakamtaka kuingia ndani ya gari, ambapo alipoingia alikuta kuna vijana watatu waliokuwa wameficha nyuso zao na alipowaangalia mmoja alikuwa na bastola ambayo alimuwekea begani.
Mhanaya anadai Getruda alimwambia yule mama akisema kwa sauti amri "unaangalia huko nyuma nini nasikiliza mimi " kisha akasema mali nitafute mimi wazitumie wengine, dereva aliguna.
Getruda akamwambi Mhanaya kuwa yule mama alifungua pochi na kumpa simu ndogo aina ya Nokia na kumwambia kuwa kwenye simu kuna laini ya airtel kwamba watakuwa wakiwasiliana ila asimuoneshe mtu na wataendelea kumfuatilia kisha wakamuonyesha brifcase wakamwambia hizi ni milioni 50 ni za kwako kama kazi hii itafanikiwa.
Akadai yule mama alimuuliza Getruda kama amemfahamu akamwambia hajamfahamu akamwambia nimekupa hii simu, ila anasema katika kuvuta kumbu kumbu akakumbuka kuwa aliwahi kumuona yule mama kwani alikuwa anaenda Mererani kwa bibi Msuya ( Alikuwa mke wa marehemu bilionea Erasto Msuya, kaka yake Aneth).
Mhanaya anadai, Getruda alimwambia kuwa, Mei 23,2016 majira ya saa nane hadi saa kumi jioni, alipigiwa simu kupitia ile simu waliyompa wakamtaka waonane, siku hiyo walisimama mbali na nyumbani kwa Aneth, alipofika walimtaka aondoke nyumbani kwa Aneth ama sivyo na yeye watampitia kisha wakamtaka ile simu aiharibu ili mtu yeyote asiweze kuipata.
Anasema wale watu walimpatia shilingi elfu 20 ili imsaidie.
Anadai Getruda alimwambia asubuhi alichukua simu hiyo aliyokuwa anaificha chini ya kochi kisha akaondoka nayo na alipofika katikati ya bahari wakati navuka feri aliitupa ile simu.
Alipofika Feri alikutana na mpenzi wake Thabit Kombo ambapo aliniomba amuhifadhi nyumbani kwake chanika ambae alimkubalia, Lakini kabla hajaenda Chanika akakumbuka kwamba alikuwa na funguo za geti kubwa za Aneth hivyo alirudi tena Kibada na kurudisha funguo kwa kumuomba mwanafunzi aliyekuwa anapita azipeleke nyumba ya jirani kwani yeye hakutaka kuonana na Aneth ambaye aliona kwa mbali gari yake ikiwa imepaki nje ya geti.
Mhanaya anadai, Getruda alimwambia kuwa, Mei 26, 2016 alipigiwa simu na ndugu yake anayeishi Mererani anayeitwa Neema akamwambia kuwa Aneth amefariki dunia kwa kuchinjwa kinyama na yeye Getrude anatafutwa.
Getruda akamwambia Mhanaya kuwa baada ya kusikia hivyo, aliamua kumueleza mpenzi wake ambaye alimshauri aende kutoa taarifa polisi lakini yeye akamuomba amtafutie nauli arudi kwao Moshi kwani alikuwa na hofu ndipo mpenzi wake akampa elfu 50 akarudi kwao.
Kesi hiyo inaendelea kesho Agosti 29, 2023.
Home
MAHAKAMA
BINTI WA KAZI WA ALIYEKUWA DADA WA BILIONEA MSUYA ALIAHIDIWA MILIONI 50/= AKAISHIA KUPEWA ELFU 20/=
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...