Benki Kuu ya Tanzania imetawazwa Mshindi wa Kwanza Kitaifa katika Kundi la Taasisi za Udhibiti, Ubora na Viwango katika Maonesho ya Wakulima - Nanenane yaliyohitimishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 8 Agosti jijini Mbeya.

Aidha, Benki Kuu imeshiriki katika Maonesho ya Nananane Zanzibar na katika Kanda zaa Kati jijini Dodoma, Kaskazini jijini Arusha, Kusini huko Lindi na Kanda ya Ziwa jijini Mwanza. Katika kanda zote, BoT imeibuka Mshindi wa kwanza katika Kundi la Mamlaka za Udhibiti na Usimamizi.

Maonesho hayo ya kimataifa yaliyofanyika katika viwanja vya John Mwakangale yalifunguliwa rasmi tarehe 01 Agosti 2023 na Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Mpango, ambaye pia alitembelea banda la Benki Kuu na kujionea namna wataalamu wake wanavyotoa elimu kwa wananchi.

Banda la Benki Kuu lilikuwa mojawapo ya vivutio muhimu katika maonesho hayo, na lilipokea wageni wengine mashuhuri wakiwemo Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge, Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Waziri Mkuu Mstaafu, Bw. Mizengo Pinda, pamoja na Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge ya Bajet, na Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo. Naibu Gavana, Bw. Julian Banzi Raphael, aliongoza ujumbe wa Benki Kuu katika kushiriki maonesho hayo, na pia alikuwa mwenyeji wa wageni hao mashuhuri.

Benki Kuu ilichukua fursa ya maonesho hayo kuwaelimisha wananchi kuhusu masuala mbalimbali ya kiuchumi na fedha. Elimu hiyo ilihusu utafiti na sera za uchumi, uwekezaji katika dhamana za serikali, usimamizi wa mifumo ya malipo ya taifa na sekta ya fedha.

Aidha, walijifunza kuhusu kazi za Bodi ya Bima ya Amana, mafunzo yanayotolewa na Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania, utatuzi wa malalamiko ya watumiaji wa huduma za fedha, na utambuzi wa alama za usalama katika noti zetu.

Zaidi ya hayo, Benki Kuu ilipata maoni na ushauri muhimu kutoka kwa wadau na wananchi mbalimbali kuhusu jinsi ya kuwafikia na kuwahudumia vyema, huku ikiendelea kuboresha utendaji wake katika kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya nchi.

Ushindi huu wa Benki Kuu ya Tanzania katika Maonesho ya Nanenane kitaifa na kikanda ni uthibitisho wa juhudi zake za kuchangia katika maendeleo ya nchi kwa kutoa elimu na huduma bora kwa wananchi na wadau wa sekta ya fedha
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella wakikabidhiwa zawadi baada ya kutembelea banda la BoT kwenye Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kaskazini yaliyofanyika katika viwanja vya Themi, Njiro jijini Arusha.

Mkuu wa wilaya ya Muleba Dkt. Abel Nyamahanga, akipewa maelezo na Mkurugenzi wa Tawi la BoT Mwanza, Bi. Gloria Mwaikambo, alipotembelea banda la BoT kwenye Maonesho ya Nanenane Kanda ya Ziwa Magharibi yaliyofanyika katika viwanja vya nyamhongolo jijini Mwanza.
Mhasibu Mwandamizi kutoka Tawi la BoT Mwanza, Bw. Amon Mwambonda, akifafanua jambo kwa mwananchi aliyetembela banda la BoT kwenye Maonesho ya Nanenane Kanda ya Ziwa Magharibi yaliyofanyika katika viwanja vya nyamhongolo jijini Mwanza.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, akipewa maelezo na Meneja Idara ya Uchumi Tawi la BoT Arusha, Bw. Stanslaus Mrema alipotembelea banda la BoT kwenye Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kaskazini yaliyofanyika katika viwanja vya Themi, Njiro jijini Arusha. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo wakipewa maelezo na Mchambuzi Mkuu wa Masuala ya Fedha kutoka Kurugenzi ya Masoko ya Fedha BoT, Bw. Ephraim Madembwe kuhusu uwekezaji katika dhamana za serikali walipotembelea banda la BoT kwenye Maonesho ya Nanenane jijini Mbeya. Wapili kutoka kulia ni Naibu Gavana, Bw. Julian Banzi Raphael.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Bw. Peter Serukamba akipewa maelezo na Meneja Msaidizi, Idara ya Uchumi na Takwimu,Tawi la BoT Dodoma, Bi. Angella Abayo, akifafanua jambo kwa alipotembelea banda la BoT kwenye Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kati, yaliyofanyika viwanja vya Nzuguni, Dodoma.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...