Na Mwandishi Wetu
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imeridhishwa na matumizi ya fedha pamoja na maendeleo ya utelezaji wa mradi wa kufua umeme wa bwawa la Julius Nyerere.
Akizungumza na waandishi wa abari baada ya kukagua mradi huo, Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Bajeti Daniel Silo amesema kuwa Kamati imefurahishwa na hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa Mradi huo.
“Kamati imekuja kujionea utekelezaji wa mradi, na tunashukuru kufahamishwa kuwa kwa sasa mradi umefikia asiliamia 90.19,” amesema Silo.
Amesema Kamati ya Bajeti inajukumu la kusimamia mapato na matumizi ya fedha za Serikali, na ni faraja kusikia tayari mkandarasi ameshalipwa shilingi trilioni 5.5 kati ya Shilingi trilioni 6.5 ambayo ni jumla ya gharama ya mradi.
“Zaidi ya asilimia 84 ya fedha za mradi zimekwisha lipwa, na sisi kama Kamati ya Bajeti tumejionea fedha tunazozitenga zinavyofanya kazi kubwa” alisema Silo.
Ameongeza katika ziara hiyo kamati imejionea maeneo mbalimbali ya mradi na kwa kasi ya utekelezaji wa mradi ilivyo, kamati inamatumaini mradi utakamilika kwa wakati na umeme utakaopatikana utachochea maendeleo ya uchumi nchini.
Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati hiyo Subira Mgalu (Mb) amekiri hakuna kilichosimama katika utekelezaji wa mradi tangu Serikali ya awamu ya sita iingie madarakani.
“Ni kweli kwamba kazi kubwa imefanyika chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani wakati uongozi wake unaingia madarakani ulikuta utekelezaji umefikia asilimia 36 na kwa sasa mradi umefikia asilimia zaidi ya 90” alieleza Mgalu.
Aidha ameipongeza Serikali kwa kuhakikisha kodi za Watanzania zinafanya kazi iliyostahili, kwani mradi unatekelezwa kwa asilimia 100 na fedha za ndani.
Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Mhandisi, Felchesmi Mramba amesema Kamati ya Bajeti inajukumu la kupitisha Bajeti za miradi, hivyo ni faraja kubwa kutembelea ili kujionea Bajeti iliyopitishwa na Bunge inavyofanya kazi.
“Wajumbe wa kamati wametembelea na kuridhika na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi, sisi kama wasimamizi wa mradi ni jambo linalotupa faraja na nguvu ya kuendelea kusimamia mradi huu na kuhakikisha unakamilika, "amesema Mhandisi Mramba.
Mradi wa bwawa la kufua umeme wa Julius Nyerere utakapokamilika unatarajia kuzalisha megawati 2115 na unagharamiwa na fedha na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...