Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog MARA

Wakati Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI - The U.S. President’s Emergency Plan for AIDS Relief (PEPFAR) ukitimiza miaka 20 tangu uanzishwe, juhudi za kuyafikia makundi ya watu yaliyo katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya VVU kutokana na sababu za kitabia, kijamii na kimazingira zimezaa matunda Mkoani Mara.


Katika Mkoa wa Mara, Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI - The U.S. President’s Emergency Plan for AIDS Relief, Kupitia Kituo cha udhibiti na uzuiaji wa Magonjwa cha nchini Marekani (CDC) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Amref Health Africa Tanzania inayotekeleza Mradi wa Afya Kamilifu wamefanikiwa kuyafikia makundi yaliyo katika hatari ya kupata Maambukizi ya VVU wakiwemo wavuvi, wachimbaji madini, wasichana rika balehe na wanawake vijana watoto wa mama wanaoishi na VVU na madereva wa malori ya masafa marefu, wajidunga wa dawa za kulevya kwa wale wanaoishi na maambukizi ya VVU (WAVIU).


Akizungumza na Waandishi wa Habari waliotembelea migodi katika eneo la Nyangoto wilaya ya Tarime,  Muelimishaji rika kutoka Kituo cha Afya Nyangoto Wilaya ya Tarime, Cleopatra Daje amesema matumizi ya waelimishaji rika katika usambazaji wa vitepe vya Jipime (HIVST) yamesaidia kuongeza idadi ya watu wanaojua hali zao za VVUna uibuaji wa wateja wenye maambukizi ya VVU miongoni mwa jamii yenye uhatarishi ambayo haifikiwi kwa urahisi wakiwemo wachimbaji madini.

“Kupitia hivi vitepe vya Jipime tumekuwa tukitumia njia ya upimaji wa mitandao ya marafiki kwa wateja wenye uhatarishi kupitia ushauri na nasaha, uchunguzi na uibuaji wa maambukizi ya VVU miongoni mwa vijana. Tunatembelea migodi pia nyakati za usiku ili kuwafikia wachimbaji wengi hapa Nyangoto kwani wengine nyakati za mchana wanakuwa shimoni”,ameeleza Cleopatra.

Muelimishaji rika kutoka Kituo cha Afya Nyangoto Wilaya ya Tarime, Cleopatra Daje akionesha kitepe cha Jipime VVU wakati akitoa elimu ya VVU na kuhamasisha upimaji VVU katika jamii ya Nyangoto wilaya ya Tarime.

“Tumekuwa tukihamasisha, kuelimisha na kuwafikia walengwa katika vijiwe kwa vikundi pamoja na njia ya mtu mmoja mmoja juu ya huduma za upimaji VVU, Dawa Kinga (PrEP), Jipime (HIVST), TB, Magonjwa ya ngono (STI) na unyanyasaji wa kijinsia (GBV) na kugawa kondomu. Tunaishukuru PEPFAR kwa kutupatia mafunzo ambayo yametuwezesha wananchi wengi ambao wamekuwa wakijitokeza kujua hali za afya na wale wanaobainika kuwa na maambukizi tunawaunganisha kwenye vituo ili waanze kupata huduma”,ameongeza Cleopatra.


HUDUMA ZA VVU KWA WAVUVI

Wakiwa katika Mwalo wa Makoko Ziwani, Manispaa ya Musoma, waandishi wa habari wameshuhudia Huduma za Upimaji wa VVU zikitolewa kwa wavuvi, wachuuzi na wananchi mbalimbali waliofika katika Mwalo huo.
Kushoto ni hema/banda la Amref Health Africa Tanzania kupitia CDC kwa ufadhili wa PEPFAR, huduma za utoaji elimu na upimaji wa VVU zikiendelea katika Mwalo wa Ziwani Manispaa ya Musoma.

Muelimishaji rika kutoka Kituo cha Afya Mwisenge Manispaa ya Musoma, Bi. Nyangeta Lucas amesema wamekuwa wakielimisha wavuvi na jamii kuhusu masuala ya VVU na UKIMWI pamoja na kutoa vitepe vya Jipime , kugawa kondomu na PreP.

“Hapa Mwaloni kupitia Amref Health Health Africa Tanzania tumeweka hema, wavuvi na wananchi kwa ujumla wanajitokeza kwa wingi kwenye banda hili kupata elimu na kupima VVU kwa kutumia vitepe vya Jipime. Kwa kweli Wavuvi wanapenda sana kondomu hivyo tunagawa sana kondomu hapa Mwaloni”, amesema Nyangeta ambaye alianza kutoa elimu kwa jamii kuhusu VVU na UKIMWI baada ya ndugu yake kufariki dunia kutokana na UKIMWI.

Naye Muuguzi katika Kituo cha Afya Mwisenge Manispaa ya Musoma, Aisha Shaban amesema huduma za kituo zimepanuliwa kuifikia jamii inayoizunguka mfano hapo Mwaloni na kuwafikia wateja lengwa mahali waliopo kulingana na mapendekezo ya siku na muda rafiki kwa mteja hali iliyochangiakuboresha na kuongeza wanufaika katika huduma hizo.
Muuguzi katika Kituo cha Afya Mwisenge Manispaa ya Musoma, Aisha Shaban akielezea namna wanavyotoa huduma za Upimaji VVU katika Mwalo wa Ziwani ili kuwafikia wavuvi na wananchi wanaofika katika Mwalo huo wenye mwingiliano wa watu wengi.

“Hapa Mwaloni huwa kuna watu wengi nyakati za asubuhi na kila siku, tunapata matokeo chanya ya uibuaji wa wateja wenye maambukizi ya VVU ambao hapo awali walikuwa hawawezi kufuata huduma hizi kituoni zimeongezeka mara dufu”,amesema Aisha.

Naye Joyce Mwita (jina siyo halisi) ambaye ni mmoja wa wananchi wanaoishi Mtaa wa Ziwani kata ya Makoko aliyenufaika na Huduma zinazotolewa kupitia Mradi wa Afya Kamilifu unaotekelezwa na Amref Health Africa Tanzania kupitia CDC kwa ufadhili wa PEPFAR ametoa wito kwa wananchi kuendelea kupima ili kujua hali zao akisema kuwa na Maambukizi ya VVU siyo mwisho wa maisha na kwamba ukiwa na maambukizi unatakiwa kuzingatia matumizi ya dawa za ARV’s ili kuwa na afya imara.
Huduma za utoaji elimu na upimaji wa VVU zikiendelea kutolewa kwenye hema/banda la Amref Health Africa Tanzania kupitia CDC kwa ufadhili wa PEPFAR katika Mwalo wa Ziwani Manispaa ya Musoma.

“Kabla ya kupima afya yangu nilikuwa naugua mara kwa mara nikijua naumwa Malaria, ilikuwa leo nikiwa mzima kesho naumwa, nikawa najitibu Malaria. Lakini baada ya kufikiwa na watoa huduma ngazi ya jamii, nikabainika nina maambukizi ya VVU, nikaanza kutumia dawa kwa usahihi, afya yangu iko vizuri kabisa siumwi umwi tena kama zamani”,ameeleza Joyce.


“Naishukuru sana Serikali ya Tanzania kukubali PEPFAR kutufikia wananchi, wametupa elimu na Vitepe vya Jipime, kwa kweli bila PEPFAR nisingepata dawa hizi. Naomba waongeze ubunifu zaidi ili kuwafikia wananchi wengi wanaoishi maeneo ya pembezoni na wananchi wapime ili kujua afya zao, wakipima wakabainika wana maambukizi wasikate tamaa, waanze kutumia dawa kwa usahihi”,ameongeza Joyce.


MAENEO YA PEMBEZONI SERENGETI 

Kwa upande wake, Muelimishaji rika, Huruma Paulo Lwila kutoka Kata ya Natta wilaya ya Serengeti anaishukuru PEPFAR kupitia CDC na Amref Health Africa Tanzania kwa namna wanavyoshirikiana na serikali kuwafikia wananchi katika maeneo ya pembezoni ambako siyo rahisi kwa wananchi kwenda kwenye vituo vya afya.

Amesema kwa kutumia mbinu hiyo inayoendeshwa kwa kutumia Jipime (HIVST) na kadi za mwaliko (kuponi), imewezesha kusaidia jamii kutambua hali zao lakini pia kuwezesha kuunganishwa kwa wateja wengine kwenye huduma za kinga.
Muelimishaji rika, Huruma Paulo Lwila kutoka Kata ya Natta wilaya ya Serengeti akitoa elimu ya VVU kwa mmoja wa wananchi katika kijiji cha Nattambiso kata ya Natta.

“Hapa Serengeti kuna shughuli za Utalii, kilimo na ufugaji hivyo kuna mwingiliano mkubwa wa watu, tunapeleka huduma za VVU katika jamii kwa mtu mmoja, mmoja au kupitia mikusanyiko mfano minada. Tumefanikiwa kuibua watu waliokuwa siyo rahisi kufikiwa, hali hii imesaidia kupunguza maambukizi ya VVU”,ameongeza Lwila.

Kwa upande wake, mmoja wa vijana walionufaika na huduma zinazotolewa na watoa huduma ngazi ya jamii kuhusu masuala ya VVU, Samwel Mathayo (22) ambaye ni Kinyozi katika kijiji cha Nattambiso kata ya Natta, Wilaya ya Serengeti, amesema amekuwa akiwahamasisha vijana kupima afya zao ili kujua hali zao na mwitikio umekuwa mkubwa.


Nao wakazi wa Kijiji cha Nattambiso kata ya Natta, Wilaya ya Serengeti ,Mugabo Mang’oha na Gladness Isaya wameishukuru Serikali na PEPFAR kwa kuwapelekea huduma za VVU katika maeneo ya pembezoni kwani wananchi wengi kutokana na mfumo wa maisha walionao siyo rahisi kwenda kwenye vituo vya afya kujua hali zao.
Muuguzi wa Kituo cha Afya Natta Wilaya ya Serengeti, Rosemary Ouma akitoa ushauri nasaha na upimaji wa VVU kwa mmoja wa wananchi.

Muuguzi wa Kituo cha Afya Natta Wilaya ya Serengeti, Rosemary Ouma ameeleza kuwa kupitia upimaji wa makundi ya watu wenye tabia zinazofanana wamefanikiwa kuwafikia wananchi wengi huku akiongeza kuwa katika kipindi cha Mwezi Aprili hadi Juni 2023 jumla ya watu waliopima VVU katika kituo na ngazi ya jamii ni 120 kati yao 42 walibainika kuwa na maambukizi yao ambapo kati hao 42, waliotoka ngazi ya jamii kupitia Jipime ni 22.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dkt. Zabron amesema chini ya Ufadhili wa PEPFAR, kupitia CDC Tanzania, Amref Health Africa Tanzania, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na mamlaka za serikali za mitaa, wamekuwa wakiwafikia walengwa mchana na usiku popote wanapoishi na kutoa elimu na huduma lengo ni kuhakikisha wanajua hali za maambukizi ya VVU kwa wananchi.


“PEPFAR ni wadau wetu katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI, ndani ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwa PEPFAR kumekuwa na mafanikio makubwa ya kujivunia. Tulipoanza huduma upimaji wa VVU ulikuwa chini lakini sasa kuna matokeo chanya kutokana na hatua kubwa zilizochukuliwa na Serikali ya Tanzania na Marekani katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI”,amesema Dkt. Masatu.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dkt. Zabron akielezea namna PEPFAR, kupitia CDC Tanzania, Amref Health Africa Tanzania, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na mamlaka za serikali za mitaa wanavyowafikia wananchi mchana na usiku popote wanapoishi kujua hali zao za maambukizi ya VVU

“Tunapoadhimisha miaka 20 ya PEPFAR hatuna changamoto ya upatikanaji wa dawa za ARV’s. Takwimu za ndani ya miaka mitano iliyopita (THS  -2016/2017) katika mkoa wa Mara maambukizi ya VVU zimepungua kutoka 4.5% hadi 3.6% lakini kwa kipindi cha mwaka 2018 hadi 2022, jumla ya wananchi 1,015,115 wamepimwa VVU  katika ngazi ya kituo na jamii kwa  mkoa wa Mara.  

Mpaka sasa vituo 107 kati ya 358 vinatekeleza mradi wa Afya Kamilifu unaofadhiliwa  na PEPFAR, vituo hivyo vinahudumia WAVIU zaidi ya 62,000 wanaopata huduma bora za VVU/UKIMWI, Kinga, tiba na Matunzo ili kufubaza virusi vya UKIMWI hapa mkoani Mara”,ameeleza Dkt. Masatu.

Aidha amesema tangu mwaka 2014 katika mkoa wa Mara wamefanikiwa kuwafanyia tohara kinga  wanaume 204,188 kwa mujibu wa DHIS2 kati yao 62,089 wanatoka katika wilaya ya Rorya ambako jamii ya hapo haikuwa na utamaduni wa kufanya tohara kwa wanaume hali iliyosababisha maambukizi ya VVU Rorya kupungua kutoka 6.2% hadi 3.8% na wanaume wamekuwa wakihamasika kufanya tohara kinga kupitia kampeni za tohara kinga zinatolewa bure kwenye vituo vya afya na kwenye jamii kupitia mfumo wa Mkoba.


PEPFAR MKOANI MARA

Kwa mkoa wa Mara , PEPFAR kupitia CDC na Amref Health Africa Tanzania na serikali ya Tanzania imeweza kufikia kata takriban 111 na kutoa huduma jumuishi za kina katika jamii ili kuunga mkono malengo ya kimataifa juu ya mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI yaani UNAIDS 95-95-95, ikijumuisha upimaji wa maambukizi ya VVU kupitia, Jipime VVU (HIVST) na upimaji wa kawaida , uanzishwaji wa tiba na dawa za kufubaza Virusi vya UKIMWI baada ya kugundulika ndani ya siku saba, uhamasishaji na ushauri nasaha kwa rika zote, uchunguzi wa kifua kikuu (TB), uchunguzi na utoaji wa dawa kinga pre-exposure prophylaxis (PrEP) za kuzuia maambukizi ya VVU kwa wale wenye tabia hatarishi kabla ya kuambukizwa, utekelezaji na usimamizi wa uunganishwaji wa WAVIU kwenye dawa kwa kudumisha mahusiano na watoa huduma (LCM).

Pia kumekuwa na utoaji wa elimu ya jumla ya afya ya uzazi, uchunguzi na utambuzi wa viashiria vya magonjwa ya ngono kwa kuzingatia dalili (STI) na huduma za uzazi wa mpango (FP), huduma zote hizi hutolewa kwa walengwa kama huduma jumuishi katika jamii.

Shughuli hizo hutolewa popote zinapohitajika zaidi kwa miguu, kwa pikipiki katika mahema, magari, kaya na katika hafla za umma ambapo huduma hizo zote hutolewa kwa mujibu wa miongozo ya Serikali yaani, Mwongozo wa Kitaifa wa Tanzania wa Afua za VVU kwa makundi maalumu yaliyo katika hatari ya VVU (KVP), Mwongozo wa Kitaifa wa Usimamizi wa VVU na mwongozo wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI (NACP) kuhusu uanzishaji wa dawa za kurefusha maisha (ART).

Muelimishaji rika kutoka Kituo cha Afya Nyangoto Wilaya ya Tarime, Cleopatra Daje akionesha namna ya kujipima VVU kwa kutumia kitepe cha Jipime VVU wakati akitoa elimu ya VVU na kuhamasisha upimaji VVU katika Jamii ya Nyangoto wilaya ya Tarime
Muonekano wa sehemu ya Machimbo
Muelimishaji rika, Huruma Paulo Lwila kutoka Kata ya Natta wilaya ya Serengeti akielezea namna wanavyohamasisha wananchi kupima. afya zao
Muuguzi wa Kituo cha Afya Natta Wilaya ya Serengeti, Rosemary Ouma akitoa huduma ya upimaji wa VVU kwa mmoja katika kijiji cha Nattambiso kata ya Natta wilaya ya Serengeti
Muuguzi wa Kituo cha Afya Natta Wilaya ya Serengeti, Rosemary Ouma akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea kijiji cha Nattambiso wilaya ya Serengeti Mkoani Mara
Muuguzi wa Kituo cha Afya Natta Wilaya ya Serengeti, Rosemary Ouma akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea kijiji cha Nattambiso wilaya ya Serengeti Mkoani Mara
Samwel Mathayo , Kinyozi katika kijiji cha Nattambiso kata ya Natta, Wilaya ya Serengeti akielezea namna alivyonufaika na huduma zinazotolewa na watoa huduma ngazi ya jamii kuhusu masuala ya VVU
Samwel Mathayo , Kinyozi katika kijiji cha Nattambiso kata ya Natta, Wilaya ya Serengeti akielezea namna alivyonufaika na huduma zinazotolewa na watoa huduma ngazi ya jamii kuhusu masuala ya VVU
Waandishi wa habari wakifanya mahojiano na Samwel Mathayo , Kinyozi katika kijiji cha Nattambiso kata ya Natta, Wilaya ya Serengeti akielezea namna alivyonufaika na huduma zinazotolewa na watoa huduma ngazi ya jamii kuhusu masuala ya VVU
Huduma za utoaji elimu na upimaji wa VVU zikiendelea kutolewa kwenye hema/banda la Amref Health Africa Tanzania kupitia CDC kwa ufadhili wa PEPFAR katika Mwalo wa Ziwani Manispaa ya Musoma ili kuwafikia wavuvi na wananchi wanaofika katika Mwalo huo.

Kushoto ni hema/banda la Amref Health Africa Tanzania kupitia CDC kwa ufadhili wa PEPFAR, huduma za utoaji elimu na upimaji wa VVU zikiendelea katika Mwalo wa Ziwani Manispaa ya Musoma ili kuwafikia wavuvi na wananchi wanaofika katika Mwalo huo wenye mwingiliano wa watu wengi.
Kushoto ni hema/banda la Amref Health Africa Tanzania kupitia CDC kwa ufadhili wa PEPFAR, huduma za utoaji elimu na upimaji wa VVU zikiendelea katika Mwalo wa Ziwani Manispaa ya Musoma ili kuwafikia wavuvi na wananchi wanaofika katika Mwalo huo wenye mwingiliano wa watu wengi.
Muelimishaji rika kutoka Kituo cha Afya Mwisenge Manispaa ya Musoma, Bi. Nyangeta Lucas akielezea namna wanavyowafikia wavuvi na wananchi kwa ujumla kuwapa elimu na wahamasisha kupima VVU
Muelimishaji rika kutoka Kituo cha Afya Mwisenge Manispaa ya Musoma, Bi. Nyangeta Lucas akielezea namna wanavyowafikia wavuvi na wananchi kwa ujumla kuwapa elimu na wahamasisha kupima VVU
Mmoja wa wananchi akielezea namna aliyenufaika na huduma zinazotolewa kupitia Mradi wa Afya Kamilifu unaotekelezwa na Amref Health Africa Tanzania kupitia CDC kwa ufadhili wa PEPFAR. Kushoto ni Muuguzi katika Kituo cha Afya Mwisenge Manispaa ya Musoma, Aisha Shaban 

Muuguzi katika Kituo cha Afya Mwisenge Manispaa ya Musoma, Aisha Shaban akielezea namna wanavyotoa huduma za Upimaji VVU katika Mwalo wa Ziwani ili kuwafikia wavuvi na wananchi wanaofika katika Mwalo huo wenye mwingiliano wa watu wengi.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dkt. Zabron akielezea namna PEPFAR, kupitia CDC Tanzania, Amref Health Africa Tanzania, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na mamlaka za serikali za mitaa wanavyowafikia wananchi mchana na usiku popote wanapoishi kujua hali zao za maambukizi ya VVU.

Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...