Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV.
MAMLAKA ya Masoko ya Mitaji na
Dhamana (CMSA)imezindua mauzo ya Hatifungani ya Benki ya CRDB yenye
mguso wa matokeo chanya kwa mazingira na jamii.
Akizungumza leo
Agosti 31, 2023 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya uzinduzi wa
mauzo ya hatifungani ya CRDB , Mkurugenzi wa Mamlaka ya Masoko ya
Mitaji na Dhamana CPA.Nicodemus Mkama amesema uzinduzi wa mauzo ya
hatifungani hiyo unathamani ya Sh.bilioni 780 sawa na dola za Marekani
milioni 300.
Akielezea zaidi amesema hatifungani ya CRDB ilipata
idhini ya CMSA Agosti 18, 2023, na 28 Agosti 28, 2023, CMSA ilitoa
taarifa rasmi kwa umma Benki ya CRDB imepata idhini ya CMSA kutoa
hatifungani yenye thamani ya Sh.bilioni 780 itakayowezesha kupata fedha
za kutekeleza miradi ya kuhifadhi mazingira na yenye matokeo chanya kwa
jamii.
Amefafanua hatifungani hiyo inakuwa ya kwanza kwa ukubwa
ikiwa imetolewa katika fedha za aina mbalimbali na yenye mguso kwenye
mazingira, na matokeo chanya kwa jamii Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Amesisitiza
idhini imetolewa na CMSA baada ya Benki ya CRDB kukidhi matakwa ya
Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Sura ya 79 ya Sheria za Tanzania,
Miongozo ya Masoko ya Mitaji na Dhamana ya Utoaji wa Hatifungani.
Pia
uwepo wa Muundo wa Hatifungani ulioandaliwa na CRDB kwa kushirikiana na
Taasisi ya Uendelezaji wa Sekta za Fedha Barani Afrika (FSD Africa) na
kukidhi matakwa ya Kanuni za Jumuiya ya Kimataifa ya Masoko ya
Mitaji(ICMA) na kupata ithibati kutoka kwa kampuni ya Sustainalytics ya
nchini Uingereza, yenye utaalam kuhusu miradi yenye mguso na matokeo
chanya kwa Mazingira na Jamii.
"Utoaji wa hatifungani ya CRDB,
utawezesha utekelezaji wa Sera mbalimbali za kitaifa na Malengo
Endelevu ya Maendeleo ya Umoja wa Mataifa hususan lengo namba saba
linalohimiza upatikanaji wa nishati safi kwa wote.
"Kama
tunavyofahamu, Serikali imeweka mkakati wa kuhamasisha matumizi ya
nishati safi kwa wote ambayo ni rafiki kwa mazingira, hivyo utoaji wa
hatifungani hii utawezesha utekelezaji wa malengo na azma ya Serikali ya
uwekezaji katika nishati safi, " amesema.
CPA.Mkama amesema
utoaji wa hatifungani hiyo utawezesha utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa
Maendeleo ya Sekta ya Fedha 2020/21 – 2029/30 wenye lengo la kuwezesha
upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya
Maendeleo katika sekta ya umma na binafsi ili kujenga uchumi shindani
kwa Maendeleo ya watu.
Pia inawezesha utekelezaji wa Sera ya
Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi yaani kwani fedha zitakazo
patikana zitatumika kutekeleza miradi mbalimbali ya Maendeleo ya jamii,
na wananchi watakao wekeza katika hatifungani hii watalipwa riba, hivyo
kuinua vipato vyao.
"Utoaji wa hatifungani hii katika fedha
mbalimbali za kigeni kutatoa mchango katika jitihada za Serikali za
kukabiliana na upungufu wa fedha za kigeni hapa nchini.CMSA imeidhinisha
utoaji wa hatifungani ya CRDB kutokana na mazingira wezeshi na
shirikishi ya kisera...
" Kisheria na kiutendaji ya Serikali ya
Awamu ya Sita chini ya uongozi madhubuti wa Rais Dk. Samia Suluhu
Hassan. Uchumi wa kidiplomasia na uhusiano wa kimataifa imekuwa chachu
katika maendeleo na ustawi wa sekta ya fedha, husan masoko ya mitaji,
ambapo sasa wanashuhudia uanzishwaji wa bidhaa mpya na bunifu, ikiwa ni
pamoja na Multicurrency Green,
Pia Masoko ya mitaji huchochea
maendeleo ya uchumi kwa kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha na
kuimarisha utawala bora na hivyo kuleta tija kwa kampuni na taasisi.
"Hii
inadhihirishwa na mashirika ya Serikali yaliyouza hisa kwa umma na
kuorodheshwa katika soko la hisa la Dar es Salaam, ambapo kampuni 7 kati
ya 10 ambazo ni walipa kodi wakubwa, ni kampuni zilizouza hisa kwa umma
na kuorodheshwa DSE.
"CRDB ni miongoni mwa kampuni ambazo
zimetumia fursa katika masoko ya mitaji, ambapo mwaka 2009, CMSA ilitoa
idhini kwa Benki ya CRDB kuuza hisa kwa umma na kuorodheshwa DSE.Katika
mauzo hayo, CRDB ilifanikiwa kupata shilingi bilioni 82.6 sawa na
asilimia 439 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 18.8."
Ameongeza
kufuatia mafanikio hayo, Benki ya CRDB imeweza kutekeleza Mkakati
ulioleta mageuzi na mafanikio yenye tija katika utendaji wa benki kwa
wanahisa wake.Bei ya hisa za Benki ya CRDB imeongezeka kutoka shilingi
150 kwa hisa wakati wa mauzo ya hisa ya soko la awali, hadi shilingi 460
kwa hisa, jana tarehe 30 Agosti 2023.
Amefafanua itakumbukwa
CRDB ilikuwa ikipata hasara na ilikuwa haitoi gawio kwa Serikali kabla
ya kuuza hisa kwa umma na kuorodheshwa DSE. Kutokana na mauzo ya hisa
kwa umma na kuorodheshwa DSE, ufanisi wa benki ya CRDB umeongezeka na
sasa benki hii inapata faida, inalipa kodi Serikalini na kutoa gawio kwa
wanahisa, ikiwa ni pamoja na Serikali.
"Kwa mfano, katika mwaka
2022, CRDB ililipa kodi Serikalini jumla ya shilingi bilioni 337.7 ikiwa
ni ongezeko la asilimia 35 kutoka jumla ya kodi ya shilingi bilioni
249.4 iliyolipwa 2021.Pia CRDB ililipa gawio kwa wanahisa Sh. bilioni
94.0...
" Ambapo gawio kwa Serikali lilikuwa shilingi bilioni
32.4, ikiwa ni ongezeko la asilimia 63.6 kutoka gawio la shilingi
bilioni 19.8 lililolipwa Serikalini mwaka 2021.CMSA itaendelea kujenga
mazingira wezeshi na shirikishi ili kuwezesha taasisi katika sekta ya
umma na binafsi kutumia masoko ya mitaji kupata fedha za kutekeleza
miradi."
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...