Na Mwandishi Wetu

NCHI za Afrika zimeshauriwa kuwekeza katika utafiti wa mbegu asili kwa kuwa zina lishe bora, uhakika wa chakula na salama kwa afya ya mtumiaji.

Ushauri huo umetolewa na wadau mbegu asili kutoka nchi 25 za Bara la Afrika, Marekani na Ulaya ambao wanakutana jijini Dar es Salaam kwa siku tatu kujadili hatma ya mbegu asili katika nchi zao na dunia kwa ujumla.

Akizungumza katika mkutano huo Mbunge wa Lindi mjini, Hamida Abdallah amesema kilimo cha mbegu asili ndio kinaweza kuleta tija kwenye sekta hiyo, kwani historia inaonesha wazee wa zamani walitumia njia hiyo.

Amesema mbegu asili hazina gharama kwenye kilimo kama ilivyo kilimo cha kisasa, hivyo ni wakati muafaka wa jamii kurejea katika mfumo huo wa zamani.

Ameongeza kutokana na madhara ambayo yanapatikana kwenye kilimo cha kisasa, dunia imeanza kubadilika na kutaka kurejea mifumo ya zamani ambayo ilijikita katika mbegu za asili.

“Naishi na wakulima wa hali ya chini ambao anashirikiana nao kuendeleza matumizi ya mbegu asili, hivyo anaungana na wadau wengine ambao wanataka uwekezaji katika utafiti wa mbegu hizo ambazo ni salama kwa afya ya binadamu,” amesema.

Amesema mkutano huo ni ujumbe sahihi kwa viongozi duniani kuweka mkazo wa kusisitiza kilimo kinachojikita katika mbegu asili ambazo ni salama kwa afya ya binadamu na mazingira.

“Sisi Lindi tumefungua benki ya mbegu asili, hiyo ikiwa ni kuonesha ni namna gani tumejipanga kuachana na mbegu za kisasa ambazo zina madhara mengi kwenye afya ya binadamu,” amesema.

Amesisitiza anatumia nafasi yake ya ubunge kuzungumzia na kushawishi umuhimu wa mbegu asili kwenye kilimo

Kwa upande wake Paul Chilewa kutoka Mwamvuli wa Asasi za Kuendeleza Kilimo Hai Tanzania (TOAM),  amesema mkutano huo ambao umehusisha zaidi ya watu 100 kutoka nchi 25 ni muhimu kwa wadau wote wa mbegu asili kujadiliana namna ya kuzilinda mbegu za asili.

Amesema Afrika kwa sasa ina changamoto kubwa ya mbegu za asili, hali ambayo itachangai kukosekana kwa uhakika wa chakula kwa siku nyingi.

“Mbegu asili zina lisha nyingi na salama kwa afya ya mtumiaji, hivyo ili kuhakikisha zinakuwa endelevu ni lazima kufanyika tafiti ambazo zitaonesha ni namna gani tunaweza kuzilinda."

 Ameongeza iwapo Serikali itafanya utafiti ambao utashirikisha wakulima ambao wanatumia mbegu asili ni wazi kuwa changamoto hiyo itapata jibu sahihi.

"Iwapo hakutakuwa na juhudi za kukabiliana na changamoto ya mbegu asili, ni wazi kuwa wakulima wataingia kwenye mtego wa kununua mbegu ambazo zitahitaji viuatilifu na mbolea ambavyo vina sumu na kusababisha maradhi mbalimbali."

Mratibu wa Mratibu wa Mtandao Baionoai Tanzania (TABIO) Abdallah Mkindi amesema utafiti unaonesha asilimia 80 ya wakulima wa Afrika wanatumia mbegu asili, hivyo ni muhimu kuhamasisha matumizi ya mbegu hizo.

Amefafanu  pia utafiti umeonesha mbegu asili zina virutubisho, hivyo iwapo jamii itahamasishwa kutumia mbegu hizo changamoto ya utapiamlo ambayo inakabili mataifa hayo itapata muafaka.

“Mbegu asili zina nafasi kubwa ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo yameonesha madhara makubwa duniani, hivyo rai yangu ni kuziomba serikali za Afrika kutenga fedha zitakazotumika kufanya utafiti wa mbegu hizi,” amesema.

Amesema TABIO kwa kushirikiana Mtandao wa Uhuru wa Chakula Dunia (AFSA) na SwissAid wamewakutanisha wadau hao ili waweze kujadiliana na kutoka na kauli moja kuhusu hatma ya mbegu asili ambazo zinaonekana kupewa kisogo na watunga sera na sheria.

Mwakilishi wa Wizara ya Kilimo, Beatrice Banzi amesema Tanzania imekuwa ikihamasisha watafiti kufanya utafiti katika sekta hiyo ya mbegu asili na mbegu zingine.

Ameongeza kilio cha dunia ni uwepo wa mbegu bora na salama kwa afya ya binadamu, hivyo utafiti pekee ndio unaweza kutoa jibu.

Ofisa Program wa AFSA, Famara Diédhiou amesema ni wakati muafaka kwa nchi za Afrika kuungana kuhakikisha mbegu asili zinapewa kipaumbele katika sekta ya kilimo.

“Tumekutana hapa Tanzania nadhani ni wakati muafaka kwa sisi kupigania uwepo wa chakula bora chenye lishe, kwa kuhamasisha matumizi ya mbegu asili,” amesema.

Katika mkutano huo nchi zilizoshiriki ni Tanzania, Kenya, Uganda, Ethiopia, Senegali, Burkina Faso, Ivory Cost, Hispania, Norway, Zambia, Zimbabwe, Australia, Togo, Mali, Benin, Chad, Tunisia, Niger, Afrika Kusini, Botswana, Malawi, Misri, Rwanda, DR Congo na Gabon.

Mbunge wa Lindi Mjini Hamida Abdallah akielezea umuhimu wa nchi za Afrika kufanya utafiti katika mbegu za asili kwani zina lishe bora





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...