Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MKUU
wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Dk Suleiman Serera ameongoza
mazishi ya mzee wa miaka 93 Maliake Laizer yaliyofanyika kijiji cha
Naisinyai.
Marehemu mzee
Maliake kwenye kizazi chake amejaliwa kupata uzao wa watu 307 wakiwemo
watoto 41, wajukuu 219, vitukuu 45 na vilembwe wawili.
Akizungumza kwenye mazishi hayo Dk Serera amewapa pole wakazi wa kata ya Naisinyai kwa kuondokewa na mzee Maliake.
"Tulikuwa
na ziara ya kamati ya siasa ya wilaya ikiongozwa na Mwenyekiti wa CCM
wa wilaya Kiria Laizer ndipo tukafika kuhani ili baadaye tuendelee na
ziara yetu," amesema Dk Serera.
Katibu
mwenezi wa CCM Wilaya ya Simanjiro, Mosses Makeseni akisoma historia ya
marehemu Maliake amesema amezaliwa mwaka 1930 kwenye kijiji cha Lorbene
kata ya Naberera.
Makesema amesema wakati wa uhai wake mzee Maliake alikuwa anajishughulisha na ufugaji na kilimo cha kujikimu.
Mbunge
wa jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka amesema marehemu Maliake
ambaye ni muasisi wa chama chao alikuwa mtu mwema mwenye kupenda haki
na asiyeonea mtu.
"Hata
kifo chake kimetokea bila kuteseka kwani walikuwa wanakula nyama naye
akawagawia baadhi ya wageni alipomaliza akatoa taarifa kuwa anaumwa
akapelekwa zahanati ya Moipo Mirerani kisha akafariki dunia," amesema
Ole Sendeka.
Mtoto wa
marehemu huyo mchungaji Joshua Maliake amesema baba yake alioa wake
wanne na mke mmoja alipofariki alioa mwingine ili kutimiza tena idadi ya
wake wanne.
"Tumepanga
baada ya mazishi kesho yake tukutane kwani ndugu tupo wengi na hatujuani
wote, hivyo tutakutana tuwatambue ndugu wa baba wadogo na baba
wakubwa," amesema Joshua.

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...