Na Mwandishi wetu, Dodoma.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
imetoa vibali vya kutoa Elimu ya Mpiga Kura katika Uchaguzi Mdogo wa
Ubunge Jimbo la Mbarali na Kata sita za Tanzania Bara kwa asasi tatu za
kiraia.
Taarifa ya Tume iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi
wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Ramadhani Kailima imesema uamuzi huo
umefikiwa baada ya Tume kukutana katika kikao chake leo Agosti 17,2023
jijini Dodoma.
“Tume imefikia uamuzi huo kwa kuzingatia kifungu
cha 4C cha sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura 343 na kanuni ya 3 ya
Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Uchaguzi wa Madiwani) za mwaka
2020, inayoipa Tume jukumu la kutoa elimu ya mpiga kura nchi nzima,
kuratibu na kusimamia taasisi na asasi za kiraia zinazotoa elimu hiyo,”
ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Kailima amezitaja asasi za
kiraia zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura na maeneo
watakayotoa elimu hiyo kuwa ni Alpha and Omega Reconciliation and Peace
Building (AREPEB), itakayotoa Elimu Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali
katika Jimbo la Mbarali, Umbrella of Women and Disabled Organisation
(UWODO) itakayotoa Elimu Halmashauri ya Wilaya ya Madaba katika Kata ya
Mtyangimbole na Bright Child Development Tanzania (BRIGHT CHILD),
Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi katika Kata ya Mwaniko.
Aidha,
Tume imetoa kibali cha utazamaji kwa Asasi ya kiraia ya Bridge
Development Trust Organization (BRIDETO) ambayo iliomba kutazama
uchaguzi mdogo katika Kata ya Mwaniko iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya
Misungwi na Kata ya Nala katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Kailima
amesema katika taarifa hiyo kuwa, Tume imefikia uamuzi huo wa kutoa
kibali hicho kwa kuzingatia kanuni ya 16(5) ya Kanuni ya Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa (Uchaguzi wa Madiwani) za mwaka 2020
Amesema
katika utekelezaji wa jukumu la kutoa elimu ya mpiga kura, asasi hizo
zitapaswa kuzingatia Mwongozo wa Elimu ya Mpiga Kura wa Mwaka 2020
katika kipindi chote cha kutoa elimu hiyo katika uchaguzi mdogo.
Kwa
mujibu wa ratiba ya uchaguzi mdogo iliyotolewa na Tume, uteuzi wa
wagombea katika uchaguzi huo utafanyika Agosti 19, 2023 na Agosti 20
hadi Septemba 18, 2023 kitakuwa ni kipindi cha kampeni kwa vyama vya
siasa na wagombea, na Jumanne ya Septemba 19, 2023 itakuwa ni siku ya
uchaguzi.
"Tume inatumia fursa hii kuzipongeza asasi zote za
kiraia zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura na utazamaji wa
uchaguzi, na inazikumbusha asasi hizo kuzingatia sheria, kanuni,
taratibu, miongozo na maelekezo ya Tume katika kipindi chote cha
utekelezaji wa majukumu yao. " alisema Kailima katika taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa Tume vibali hicho kitatumika kuanzia tarehe Agosti 18, 2023 hadi Septemba 18, 2023.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji (Rufaa) Mhe. Jacobs Mwambegele (kulia) akiongoza Kikao cha Tume kilichokutana leo Agosti 17,2023 jijini Dodoma. Pamoja nae ni Makamu Mwenyekiti wa Tume, Jaji wa Rufaa (Mstaafu), Mhe.Mbarouk Salim Mbarouk. Wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakiwa katika kikao kilichokutana leo Agosti 17,2023 Jijini Dodoma.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...