Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameitaja huduma ya bima ya kilimo inayotolewa na benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kama mmoja ya suluhisho muhimu katika kuwahakikishia wakulima kipato cha uhakika huku akitoa wito kwa wakulima nchini kutumia vema huduma mbalimbali za kibenki zinazotolewa na serikali pamoja taasisi za kifedha ili kuboresha kasi ya ukuaji wa sekta hiyo.

Raisi Samia alitoa wito huo mapema hii leo alipotembelea banda la NBC lililopo kwenye Maonesho ya Kilimo Nanenane yanayofanyika mkoani Mbeya mara baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Mkurugenzi wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi kuhusiana na fidia yenye thamani ya Dola za Kimarekani 33,537.89 sawa na Tsh 85 Milioni iliyotolewa na benki hiyo kwa wakulima wa zao la tumbaku walioathirika na mvua za mawe katika msimu wa kilimo uliopita.

Kwa mujibu wa Rais Samia serikali na taasisi za kifedha ikiwemo benki ya NBC zimejitahidi kubuni huduma mbalimbali zinazolenga kuwawezesha wakulima ikiwemo mikopo ya fedha na zana za kilimo hivyo ujio wa huduma ya bima ya kilimo utasaidia kuwahakikishia wakulima kipato cha uhakika kutokana shughuli zao badala ya kubahatisha kama ilivyokuwa awali.

‘’Ndugu zangu wakulima mnataka mmepewe nini tena!? Kwasasa mnawezeshwa kwenye kila hatua ikiwemo pembejeo bora, zana za kilimo za kisasa na mikopo mbalimbali. Pamoja na vyote hivyo changamoto ilikuwa imebaki kwenye hasara zitokanazo na majanga mbalimbali ikiwemo mafuriko na mvua za mawe. Hata hivyo NBC wamekuja na huduma ya bima ya kilimo ili kumaliza tatizo hilo ili kuwahakikishia uhakika wa mapato yenu, bado mnataka mpewe nini tena,’’ alihoji Rais Samia.

Hata hivyo Rais Samia aliendendelea kuzisisitiza taasisi hizo za fedha kuhakikisha zinaendelea kushusha riba zao ili kuwavutia zaidi wakulima watumie huduma kifedha kutoka taasisi hizo kwa faida zaidi.

Akifafanua zaidi kuhusu huduma ya Bima ya Kilimo inayotolewa na Benki ya NBC kwa kushirikiana kampuni ya Bima ya Jubilee, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe alisema itasaidia kuondoa changamato ya hasara walizokuwa wakizipata wakulima kutokana na majanga mbalimbali yaliyo nje ya uwezo wao ikiwemo mafuriko, moto na mvua za mawe ambazo kwa kiasi kikubwa zimekuwa zikiathiri ustawi wa wakulima na kusababisha baadhi yao kuhofia kuwekeza kwenye sekta hiyo muhimu.

‘’ Hata hivyo Mheshimiwa Rais hatua hii ya NBC ni mwazo wa kuelekea katika utekelezaji mkubwa zaidi wa pamoja katika kuhakikisha kwamba huduma hii ya bima ya kilimo inawafikia wakulima wengi zaidi…hivyo nawapongeza sana NBC kwa kuanzisha hili,’’ alipongeza Bashe

Awali akizungumza mbele ya Rais Samia, Sabi alisema malipo yatokayo na bima ya kilimo ya benki hiyo ni mwendelezo wa pili kwa kuwa tayari benki hiyo ilikwisha toa fidia ya kiasi cha dola 4000 sawa na kiasi cha 10 Milioni kwa mwaka wa kwanza wa uendeshaji wa huduma hiyo huku akitaja mikoa ambayo wakulima wake wamenufaika na bima hiyo kwa msimu wa pili kuwa ni Tabora, Geita na Shinyanga ambapo jumla ya vyama vya msingi (AMCOS) 10 vimenufaika na malipo hayo.

‘’Malipo haya yanahusisha jumla ya wakulima 140 kutoka AMCOS 10 za mikoa ya Tabora, Geita na Shinyanga ambao mazao yao ya tumbaku yaliathirika vibaya na mvua za mawe ambapo jumla ya eneo la hekari 2,531 liliathirika kwa viwango tofauti na kuathiri mavuno yao. Kupitia Bima ya Kilimo ya NBC inayoendeshwa kwa ushirikiano na kampuni ya Bima ya Jubilee wahanga hawa wamelipwa fidia,’’ alisema Sabi huku akitoa wito kwa wakulima wa mazao mbalimbali kuchangamkia bima hiyo.

Akiwa bandani hapo Rais Samia pia alipata wasaa kufahamu huduma mbalimbali zitolewazo na benki hiyo mahususi kwa wakulima na pia alipata nafasi ya kuzungumza na Mkulima wa zao la mpunga mkoani humo, Alex Chengura mmoja wa wakulima alienufaika na mkopo wa trekta moja kati ya matrekta matatu yaliyotolewa na benki ya NBC kwa njia ya mkopo nafuu kwenda kwa wakulima.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan (katikati) akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi (Kulia) aliekuwa akimuonesha baadhi wakulima (walioshika mfano wa hundi) ambao wamenufaika na fidia ya kiasi cha fedha Dola za Kimarekani 33,537.88 sawa na Tsh 85 Milioni iliyotolewa na benki hiyo kwa kushirikiana na kampuni ya Bima ya Jubilee baada ya tumbaku ya wakulima hao kuathiriwa na mvua za mawe katika msimu wa kilimo uliopita wakati Rais alipotembelea banda la NBC lililopo kwenye Maonesho ya Kilimo Nanenane yanayofanyika mkoani Mbeya mapema hii leo. Wengine ni pamoja na Waziri wa Kilimo Hussein Bashe
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan (kulia) akimsikiliza Mkulima wa zao la mpunga mkoani Mbeya, Alex Chengura (kushoto) ambae mmoja wa wakulima alienufaika na mkopo wa trekta moja kati ya matrekta matatu yaliyotolewa na benki ya NBC kwa njia ya mkopo nafuu kwenda kwa wakulima katika Maonesho ya Kilimo Nanenane yanayofanyika mkoani Mbeya wakati Rais alipotembelea banda la NBC lililopo kwenye Maonesho hayo mapema hii leo. Wengine ni pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi (katikati)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...