Njombe
Mkuu wa mkoa wa Njombe Antony Mtaka ameagiza shule zote zilizopata fedha za ujenzi wa mabweni zifungwe camera za CCTV lengo likiwa ni kuimarisha ulinzi na usalama wa wanafunzi.
Mtaka Ametoa agizo hilo alipotembelea na kukagua shule ya sekondari Yakobi wakati wa kuwapokea wanafunzi wa kidato cha tano ambapo amesema kutokana na kuwapo kwa historia ya ukiukwaji wa maadili ulioripotiwa shuleni hapo mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Njombe pamoja na maeneo mengine wanapaswa kuchukua hatua za kufunga mifumo ya Camera.
"Tuna halmashauri sita, tehama na watu wa TTCL wapite kwenye shule ambazo pesa za mabweni zimetolewa waone namna ya kufunga miundombinu ya kamera ili tuweze kuondokana na matukio ambayo wakati mwingine yamehatarisha watoto"alisema Mtaka
Awali mkuu wa shule ya sekondari Yakobi Mwalimu Editha John amesema tayari wanafunzi wa kike wa kidato cha tano wameshaanza kuripoti kati ya wanafunzi 433 waliopangiwa shuleni hapo.
Afisa elimu mkoa wa Njombe Mwalimu Nelasi Mulungu amesema serikali imeleta shilingi bilioni 4.8 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni kwenye shule 12 za sekondari na hivyo kila mmoja anapaswa kuchukua hatua za kumsaidia mtoto.
Aidha mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Njombe Kuruthum Sadick amesema wakati ujenzi wa mabweni ukitarajia kukamilika katika kipindi cha takribani siku tano tayari wameandaa mazingira mengine ya kuwapokea wanafunzi.
Ahadi ya wanafunzi wa shule hiyo akiwemo Nancy Abraham,Zacharia Kaduma na Carolina Keneth ni kusoma kwa bidii ili waje kulisaidia taifa katika siku za usoni.
Muhula mpya wa masomo kwa wanafunzi wa kidato cha tano umeanza rasmi sasa huku wanafunzi wakiendelea kuripoti shule.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...