Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa Wanafunzi ili kurahisisha upatikanaji wa elimu bora nchini.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameyasema hayo wakati akizungumza na Viongozi , wana CCM na Wananchi wa Jimbo la Donge, Mahonda na Bumbwini katika ziara yake ya kukiimarisha Chama Mkoa wa Kaskazin Unguja.
Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria kuwawekea mazingira mazuri Wanafunzi ikiwemo ujenzi wa Skuli za ghorofa, Madarasa, na Vifaa vya kufundishia pamoja na kuzingatia maslahi ya Walimu.
Amesema Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali itajenga Dakhalia kubwa katika Wilaya zote za Zanzibar pamoja na Dakhalia kwa skuli zenye uhitaji ili Wanafunzi waweze kusoma vizuri na kuweza kukuza ufaulu nchini.
Mhe. Hemed ameeleza kuwa Mkoa wa Kaskazini Unguja umebahatika kupata Miradi mingi ya maendeleo inayopelekea kuzalisha ajira kwa Vijana pamoja na kukuza Uchumi wa Zanzibar kupitia shughuli mbali mbali ikiwemo shughuli za kitalii na za kijamii.
Akizungumzia changamoto zinazowakabili Wananchi hao Mhe. Hemed ameeleza kuwa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 imeelekeza kuwaletea maendeleo Wananchi pamoja na kuwatatulia changamoto zinazowakabili hivyo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itahakikisha wananchi wanapata mahitaji yao yote ya msingi ikiwemo maji, barabara, elimu na afya.
Akiwaasa Viongozi na Wanachama wa CCM Mhe. Hemed amewataka Viongozi wa Majimbo hayo kuachana na makundi na kuhujumiana ndani ya Chama hasa Viongozi kwa Viongozi ambapo kufanya hivyo ni kutokukitendea haki Chama Cha Mapinduzi na kwenda kinyume na dhamira ya waasisi wa chama hicho.
Amesema kuwa baadhi ya wanachama wa CCM wameanza kutangaza nia za kutaka kugombea nafasi mbali mbali za Uongozi kabla ya muda sahihi kufika na kuiagiza Kamati ya Siasa ya Jimbo kuwachukulia hatua za kinidhamu wale wote watakaobainika kufanya hivyo.
Amefahamisha kuwa ni jukumu la Kamati ya Siasa na Viongozi kusimamia nidhamu na uwajibikaji ndani ya Chama na ikitokea mikwaruzano ya kibinaadamu itatuliwe kwa kutumia Miongozo ya Sheria na Kanuni za Chama cha Mapinduzi .
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja Ndg, Iddi Ali Ame A ameeleza kuwa wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja wana kila sababu ya kumuunga Mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuelekeza miradi mingi ya maendeleo katika Mkoa huo ikiwemo ujenzi wa Bandari Kubwa Mangapwani pamoja na Uwanja wa ndege wa kigunda.
Amesema Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Kaskazini Unguja kimesajili wanachama wapya na wengine waliotoka vyama vya upinzani zaidi ya 5,500 na watahakikisha ndani ya Mkoa huo hakuna Chama cha upinzani kitakachopeperusha bendera yake.
Nae Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kaskazini Ndg, Ismail Ali Ussi amemuhakikishia Mhe. Hemed kuwa Vijana wa Mkoa huo wataendelea kukipigania Chama Cha Mapinduzi kwa kila hali ili kuendelea kushika Dola ifikapo uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Aidha ameeleza kuwa vijana wa Mkoa huo wataendelea kutangaza mazuri yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi ili kuongeza Imani ya wananchi kwa CCM na Serikali.
Kwa upande wao wabunge na wawakilishi na Madiwani wamesema Ilani ya CCM Mkoani humo inaendelea kutekelezwa na kumuomba Mhe. Makamu Serikali iwasaidie kuwachimbia Visima viwili Vikibwa vya maji safi na salama kwa ajili ya umwagiliaji maji shuhuli za kilimo kwani shuhuli kuwa Jimboni humo ni kilimo
Awali Makamu wa Pili wa Rais wa zanzibar ameweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Tawi la CCM Vijibweni, ameshiriki ujenzi wa Tawi la CCM Kipandoni, kukagua ujenzi wa Tawi la CCM Kidanzini na kukagua Daraja la Pangatupu na kukabidhi Trekta kwa wananchi wa Jimbo la Donge ambalo limenunuliwa kwa fedha za mfuko wa Jimbo, hivyo amewataka wananchi hao kuweza kulitunza pamoja na kuimarisha kilimo chenye tija kwa maslahi yao binafsi na Taifa kwa ujumla.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...