Na Said Mwishehe, Michuzi TV 

MOJA ya tukio kubwa linalokwenda kutokea visiwani Zanzibar hasa eneo la Makunduchi kuanzia  Agosti 26 mwaka huu ni uzinduzi wa Tamasha la Nane la Kizimkazi kwa mwaka 2023.

Tamasha hilo awali lilifahamika kama Samia Day na lilianza rasmi mwaka 2016, hivyo mwaka huu 2023 linatimiza miaka nane.

Limekuwa kivutio kikubwa kwa wananchi wa Makunduchi pamoja na wageni waalikwa kutoka maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya Zanzibar.

Tunafahamu tamasha hilo pamoja na mambo mengine  limekuwa likiwaleta  pamoja na kuwaunganisha Wanakizimkazi na maeneo ya jirani,  kulinda na kudumisha mila na desturi za Kizimkazi kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Pia limekuwa likitumika kuhamasisha shughuli za maendeleo, kutangaza fursa za kiuchumi zilizopo Mkoa wa Kusini Unguja.

Kwa sasa Jimbo la Makunduchi linahusisha Shehia za Mtendeni, Kibuteni na Muyuni na tamasha la Kizimkazi litafanyika Kashangae Kijiji cha Paje Wilaya ya Kusini Mkoa kusini Unguja

 Katika kufanikisha tamasha hilo kumekuwepo na wadhamini mbalimbali lakini Mdhamini Mkuu ni Benki ya Watu wa Zanzibar PBZ na kwa mujibu wa ratiba Rais wa Zanzibar Dk.Hussein Ali Mwinyi atazindua tamasha hilo Agosti 26, 2023.

Na katika kilele cha tamasha hilo kitakuwa Agosti 31, 2023 ambapo Rais Dk.Samia Suluhu Hassan atakuwa mgeni rasmi.Lakini katika kunogesha tamasha hilo timu za mashabiki wa Simba na Yanga wanaoishi Makunduchi watapambana katika bonanza  litakalofanyika Agosti 25, 2023 yaani Ijumaa ya wiki hii.

Pia kutakuwa na shughuli mbalimbali za kijamii  zitakazofanywa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan zikiwemo za kutoa  misaada kwa wazee kuanzia miaka 80 katika Wilaya ya Kusini

Pia kutoa msaada kwa watoto yatima na kutembelea wagonjwa katika hospitali za Wilaya ya Kitogani na Makunduchi, kutoa taulo za kike kwa wanafunzi wa skuli za Wilaya ya Kusini

Kuhamasisha unywaji wa maziwa kwa skuli za wilaya ya Kusini, kutoa gari mbili za wagonjwa kwa kituo cha afya Kizimkazi Dimbani pamoja na gari mbili kwa ajili ya kituo cha Polisi Kizimkazi

Aidha kutakuwa na shughuli zingine za maonesho ambazo ni Maonesho ya mavazi ya Kimasai, Ngoma za Wahaya,Kigoma, Wasukuma pamoja na kuibua vipaji vya wasanii.

Pia kutakuwa na Maonesho ya Wanyama kama fisi, chui na pundamili ili kukuza utalii,  Wasanii wa Bongo Fleva, Singeli na Taarabu za Kizanzibar, Makombora pamoja na kuoneshwa Makala ya Maisha ya Rais Samia Suluhu nje ya urais.

Kupitia tamasha la Kizimkazi kutakuwa na fursa mbalimbali zikiwemo za maonesho ya ujasiriamali, ushiriki wa taasisi Binafsi  na za umma.

Akizungumza kuhusu tamasha hilo Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Rashid Hadid Rashid anasema tamasha hilo limekuwa na mvuto mkubwa lakini linalofurahisha zaidi linajenga umoja na upendo.

 Akatumia nafasi hiyo kumshukuru Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwanamke Initiatives Foundation Wanu Ameir Hafidh kwa kuratibu na kusimamia vema tamasha hilo.

“Niseme ni faraja kubwa kwasababu tamasha hili linatuunganisha  katika kuleta umoja katika nchi yetu. Dhamira ya Dk.Samia ni kubwa katika kuleta umoja na mshikamano katika nchi yetu.”

Amefafanua Rais Dk.Samia na Rais Dk.Hussein Ali Mwinyi wameimarisha umoja na mshikamano na kusisitiza umoja wetu umeendelea kuimarika.

“Tamasha letu litakuwa na wageni wa  kila aina kwa hiyo lazima tuchunge heshima zetu na tumuoneshe Mama(Rais Samia) tuko pamoja naye katika kuleta umoja katika nchi yetu.

“Nawambia watanzania karibuni katika mkoa huu wa Kusini Unguja, mkoa uko salama hauna matatizo yoyote, tunafanya shughuli zetu na mtaondoka mkiwa salama. Hamtasikia lolote.”




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...