Na. Dennis Gondwe Dodoma,

WAAJIRI katika Mkoa wa Dodoma wametakiwa kutoa msukumo katika kurahisisha na kusaidia wanawake walioajiriwa kuendelea kunyonyesha watoto wao kwa mujibu wa taratibu ili wawe na lishe bora.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule katika hotuba yake kwenye matembezi ya hiari kuhamasisha unyonyeshaji wa maziwa ya mama na kusomwa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri yaliyoishia uwanja wa Shule ya Msingi Chang’ombe jijini hapa.

Senyamule alisema kuwa lengo kuu la maadhimisho ya mwaka huu ni kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kusaidia wanawake waweze kufanya kazi za uzalishaji pamoja na utunzaji wa watoto wao. Alisema kuwa ili kufanikiwa “lazima kuhamasisha na kutetea utekelezaji wa mikakati inayowezesha waajiri kuwa karibu na familia, walezi au mama wa mtoto na kutoa msukumo katika kurahisisha na kusaidia wanawake walioajiriwa kuendelea kunyonyesha watoto wao. Kuwahimiza waajiri kutenga sehemu maalum kwa ajili ya wafanyakazi wanawake wanaonyonyesha ili waendelee kufanya hivyo mahali pa kazi”.

Alisema kuwa maadhimisho hayo yanalenga kuelimisha umma kuhusu sheria ya kulinda haki za uzazi kwa wanawake na nyingine za kitaifa. “Vilevile, kuwawezesha wanawake kufanya kazi na kunyonyesha watoto wao ipasavyo kwa kushawishi upatikanaji wa aina mbalimbali za msaada kutoka kwa wadau katika sekta zote” alisema Senyamule.

Akioanisha majukumu ya uzalishaji mali, uzazi na maisha ya wanawake na wanaume kwa pamoja, alisema kuwa kutaleta faida kwenye sekta zote katika jamii. “Faida zinazopatikana ni pamoja na uboreshaji tija, kipato cha familia na usalama wa kazi, ustawi na afya ya wanawake na watoto, kufaidika kwa waajiri na kuwepo kwa taifa lenye mfumo imara wa kijamii na kiuchumi” alisema Senyamule.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mradi wa USAID/ Lishe Endelevu unaofadhiliwa na USAID na kutekelezwa na Shirika la Save the Children, Joyceline Kaganda alisema kuwa mchango wa mradi katika kufanikisha juhudi za serikali kuhusu afua ya unyonyeshaji wa maziwa ya mama ikiambatana na ufanyaji kazi kwa ajili ya kujikimu. “Mradi umewezesha mafunzo na vitendea kazi ili kuimarisha lishe ya wanawake wajawazito, wanaonyonyesha, watoto wachanga, wadogo na vijana balehe kwa WAJA wapatao 4,000, Mkoa wa Dodoma peke yake walikuwa WAJA 1,221. Hawa wanatumika kumfikia mlengwa katika elimu ya unyonyeshaji moja kwa moja hadi ngazi ya kaya. Mradi pia ulitoa mafunzo ya unasihi wa lishe kwa watoa huduma wa afya 600 na kwa Mkoa wa Dodoma ni 220 wanaendelea kuimarisha uelewa wa walengwa kila wanapohudhuria kliniki kuanzia ujauzito na ufuatiliaji wa hali ya lishe ya mtoto” alisema Kaganda.

Fursa nyingine ya mradi aliitaja kuwa ni kutoa mafunzo ya mbinu bora za kilimo, mifugo, na uvuvi kwa maafisa ugani 800 kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa chakula mchanganyiko chenye virutubishi vingi katika ngazi ya kaya na kuongeza kipato cha kaya. “Sote tutakubaliana ili mama atengeneze maziwa ya kutosha ni lazima apate mlo wa kutosha na wenye mchanganyiko wa vyakula kutoka makundi yote ya vyakula. Pia awe na mahitaji mengine ya msingi ili kumpunguzia msongo wa mawazo” alisema Kaganda.

Nae Afisa Lisha wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Semeni Eva Juma alisema kuwa mama anayenyonyesha anatakiwa kupunguziwa kazi na msongo wa mawazo. “Siku 1,000 za mwanzo bora wa mtoto ndiyo maisha bora mtoto, ukikosea hapo mtoto anadumaa kiakili na uwezo wa kufikiria unadumaa. Hivyo, tunashauri maziwa ya mama mtoto aanze kunyonya ndani ya saa moja tangu anapozaliwa. Kipindi hiki ndiyo muda maziwa ya kwanza ya njano yanayokuwa na virutubishi vyote muhimu kwa lishe bora ya mtoto yanauhumu kwa mtoto. Baada ya hapo endelea kumnyonyesha mtoto kadri anavyohitaji” alisema Juma.

Maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji tarehe 1-7 Agosti, 2023 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Saidia unyonyeshaji: Wezesha wazazi kulea watoto na kufanya kazi zao kila siku”.  


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...