Na Nasra Ismail ,Geita
WAFANYABIASHARA katika Mamlaka ya Mji mdogo wa Katoro mkoani Geita wamemtuhumu Ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) ambapo wamedai amekuwa akitumia lugha ya Kiingereza wakati akiwahudumia hali inayosababisha kutokuwa na maelewano kati yao na TRA.
Tuhuma hizo dhidi ya Ofisa wa TRA zimetolewa na wabunge waliofanya mkutano wa hadhara katika mji huo mdogo na kudai kuwa wafanyabiashara hao wamekuwa wakipitia wakati mgumu wakati wakienda kulipia kodi na kukadiriwa kutokana na kutokuelewa lugha inayozungumzwa na Ofisa huyo.
Mbunge wa Jimbo la Geita Joseph Musukuma amueleza Mkuu wa Mkoa wa Geita Martin Shigela na kwamba hali hiyo imesababisha sintofahamu kwa wafanyabiashara kukadiriwa kodi na ofisi ya TRA Katoro lakini baadae wanaibuka maofisa kutoka Geita na kukanusha makadirio ya mwanzo.
“Tunayo ofisi ndogo ya TRA hapa Katoro, maofisa wanaenda kukadiria kodi wanakubaliana wanaanza kutoa kodi wiki mbili baadae wanakuja wengine kutoka Geita wanasema ulikadiriwa kidogo.
"Sasa nauliza ni halali au ni feki ili tuisubiri ile ya Geita, hatuwezi kuwa na wahuni ambao wanakadiria leo na kesho tena wanafanya wengine, " amesema Musukuma.
Kwa upande wake Mbunge wa Mbogwe Nicodemas Maganga amemuomba Mkuu wa Mkoa wa Geita kuangalia suala wafanyabiashara wadogowadogo maarufu kama Machinga ambao wapo kwenye soko ambalo halina watu, hivyo wapelekwe eneo lenye watu ili wafanye biashara zao vizuri.
Wakati huo huo Mbunge wa Geita Mjini Costantine Kanyasu amesema katika kutekeleza ahadi Serikali inatarajia kujenga shule bora ya wasichana Geita mjini itakayogharimu zaidi yaSh.bilioni 4.1 kwa ajili kuleta maji na tayari mkandarasi ameanza kazi.
Aidha Mbunge wa Bukombe Dotto Biteko amewaomba wana Katoro kuacha kusikiliza maneno ya uzushi yanayozungumzwa na wapinzani kwani wanatumia uzushi huo kumuangusha Raisi Samia Suluhu Hassani badala ya kumuunga mkono.
“Nataka niwaambie Rais Dk. Samia Suluhu Hassan , mama huyu amefanya kazi kubwa sana, hakuna jambo lolote analotaka zaidi ya kuona Tanzania inabadilika.Inawezekana watu hawaelewi kwasababu ya habari za kusikia, niwaambie nikiwa shuhuda matendo yake yanamtangaza kuliko anavyosema, "amesema Biteko.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita Martin Shigela amewapongeza wabunge wa mkoa huo kwa kazi kubwa wanaoyifanya ya kuhakikisha maendeleo waliyoyahidi yanaendelea kufanyika.
“Niwahakikishie taka katika mkoa wenye viongozi wazuri, katika mkoa wenye viongozi wanaojituma ni katika mkoa wetu wa Geita , wabunge tunaowaona hapa wana uchungu wa maendeleo ya nchi yetu na wanachukizwa na mtu anayekuja kutaka kuwadanganya wananchi wa Geita, ”amesema Shigela.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...