Wananchi wakiwa wamefurika katika Banda la Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Naliendele kujifunza teknolojia mbalimbali za kilimo kwenye Maonyesho ya Nanenane 2023 yanayofikia tamati leo Agosti 8, 2023 viwanja vya Ngongo mkoani Lindi.
Na Dotto Mwaibale, Lindi
WANANCHI kutoka Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma wakiwa wamefurika katika Banda la Taasisi ya Utafiti kwa Kilimo Tanzania (TARI) Naliendele mkoani Mtwara kwenye Maonyesho ya Nanenane 2023 Kanda ya Kusini yanayofanyika Viwanja vya Ngongo mkoani Lindi kujionea na kujifunza teknolojia mbalimbali za kilimo.
Katika Maonesho hayo watafiti wa kilimo wa TARI wanaonesha na kutoa elimu za teknolojia za kilimo za kuvutia jambo lililosababisha banda hilo kufurika wakulima na wananchi kwa lengo la kujifunza.
Akizungumza na waandishi wa habari katika banda hilo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Kituo hicho Dk. Fortunus Kapinga kuhusu maonesho hayo Mtafiti wa Kilimo Bakari Kidunda ambaye pia ni Mratibu wa Uhalishaji Teknolojia na Mahusiano alitaja baadhi ya teknolojia ambazo zinaoneshwa na kutolewa kwa wakulima ni za mazao ya korosho, ufuta, karanga, mihogo, viazi vitamu, kunde, choroko, mbaazi, mahindi na uwele.
Kidunda alitumia nafasi hiyo kuwaeleza wakulima kuwa katika kituo chao cha Naliendele wamekuwa hawana msimu bali wameweka teknolojia ambazo zinaonekana kwa mwaka mzima kwa ajili ya wakulima kujifunza hatua mbalimbali za ukuaji wa zao husika kuanzia likiwa kwenye kitalu, shambani, utumiaji wa viatilifu, udhibiti wa magonjwa na uvunaji wake.
Mkulima Mathayo Milanzi kutoka Wilaya ya Nanyumbu alisena amevutiwa na teknolojia zinazofundishwa na TARI na kuwa moja ya teknolojia hizo ni kilimo cha ndizi aina ya Mtwike ambapo awali alipokuwa akilima kwa kutumia kilimo cha mazoea alikuwa akipata mazao kiduchu.
"Zamani ndizi nilizokuwa nikivuna nilikuwa nikizibeba kichwani lakini baada ya kupata mafunzo ya kilimo cha kisasa nimekuwa nikivuna ndizi nyingi hadi nalazimika kukodi pikipiki kwa ajili ya kuzisafirisha kwenda kwenye soko," alisema Milanzi.
Milanzi alisema TARI wamekuwa mkombozi kwa wakulima wa Mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara kwa kuwafanya kukielewa kilimo chenye tija.
Mkulima mwingine, kutoka Kijiji cha Chemchem Wilaya na Nachingwea, Issa Bakari amesema TARI imekuwa mkombozi kwa wakulima wengi katika kandahiyo kwani imesabisha uzalishaji wa mazo yao kuongezeka hususani maeneo ya vijijini.
Mimi natoka Kijiji cha Chemchem wilayani Nachingwea mkoani Lindi nimekuja mahususi katika Banda la TARI ili niongeze uzoefu kutoka kwa wataalam wabobezi ambao wamekuwa ni msaada mkubwa sana kwetu hasa sisi wakulima wa vijijini,” alisema Bakari.
Mtafiti wa mbegu bora za korosho kutoka TARI Naliendele, Joackim Madeni (kushoto) akitoa elimu kwa mkulima kutoka Wilaya ya Nachingwea ambaye alitembelea banda la Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Naliendele katika Maonyesho ya Wakulima Nanenane ambayo yanafikia tamati leo katika Viwanja vya Ngongo mkoani Lindi.
Mtafiti wa mbegu bora ya mihogo, Ndwasi Gambo (kushoto) akiwaelekeza wananchi kuhusu kilimo chenye tija za zao hilo.
Muonekano wa mikorosho kwenye maonyesho hayo
Mtafiti Msaidizi wa zao la Karanga na alizeti, Said Ally, akielekeza kuhusu kilimo cha zao hilo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...