Na Rahima Mohamed, Asya Khamis Maelezo
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyama Pori Tanzania (TAWA) imewataka wananchi wa Zanzibar kujitokeza kwa wingi katika ufunguzi wa Tamasha la Kizimkazi ili kujionea wanyama pori mbalimbali kutoka Tanzania Bara.
Hayo yamesemwa na Afisa Utalii kutoka Mamlaka ya usimamizi wa wanyama Pori Tanzania (TAWA) Lusanjo Nsweve wakati akizungumza na Waandishi wa habari huko Paje Mkoa wa Kusini Unguja.
Amesema wanyama hao watakuepo kuanzia leo hadi tarehe 31 na wananchi watajionea wanyama hao mubashara ikiwemo nungunungu, simba, chui, fisi, pundamilia, ndege mbalimbali na kupata elimu pamoja na kujua tabia za wanyama hao.
Afisa Lusanjo amesema Wananchi wanaweza kupata elimu ya ufugaji wanyama pori kwa kutumia Mbuga au mashamba Ili kuongeza pato la taifa Nchini.
Aidha amesema sekta ya utalii ni muhimu sana katika nchi yetu hivyo kuwepo kwa wanyama hao Zanzibar kutasaidia kuvitangaza vivutio mbalimbali nchini ili wanachi na wageni wajionee kwa macho yao na kutembelea vivutio hivyo.
Vilevile afisa huyo amesema kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutumia Tamasha hilo kutasaidia kuhamasisha wenyeji na wageni kujionea vivutio hivyo kwa ajili ya kuutangaza utalii na kuongeza wageni.
Hivyo amewasisitiza na kuwatoa wasiwasi wananchi watakaotembelea maonesho hayo kwani wanyama hao wapo katika hali nzuri na wametunzwa kitaalamu na kuekwa kwenye vizimba ambavyo viko imara kabisa.
Nao wakaazi wa Paje wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea fursa za maonesho mbalimbali ikiwemo wanyama pori ikiwa ni kivutio cha utalii.
Muhifadhi wa wanyama pori Mamlaka ya Usimamizi wa wamyama pori Tanzania TAWA Ashraf shemoka akiwaelezea Waandishi wa Habari kuhusiana na wanyama pori wanaopatikana katika hifadhi ya wanyama pori ya Taifa wakati walipotembelea Tamasha la Kizimkazi linalotarajiwa kuzinduliwa Agosti 26 na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi.PICHA NA FAUZIA MUSSA-MAELEZO ZANZIBAR
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...